Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba yazidi kupaa Afrika

30th April 2012
Print
Comments
Felix Sunzu (katika) akimbeba Haruna Moshi `Boban` kumpongeza kwa goli lake la kwanza alilofunga baada ya kutengewa pasi na Mzambia huyo wakati a mechi yao ya hatua ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan kwenye uwanja Taifa jana.Simba ilishinda 3-0.

Ikicheza kwa uelewano wa hali ya juu kuelekea mwishoni mwa mchezo, Simba ilipata ushindi iliostahili wa 3-0 katika dakika zilizofuatana za 66, 77 na 88 dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Haruna Moshi 'Boban', Patrick Mafisango na Emmanuel Okwi aliyekuwa nyota wa mchezo wa jana, kila mmoja alifunga goli moja katika kipindi cha pili baada ya dakika 45 za kwanza kumalizika bila ya goli na kuipa Simba mwanzo mzuri kabla ya mechi yao ya marudiano ugenini Sudan wiki mbili zijazo.

Baada ya kipindi cha kwanza ambacho mizani ya mchezo ilionekana imelingana, Simba walirejea wakiwa wakali zaidi katika kipindi cha pili na wakapata goli la kuongoza katika dakika 66 kupitia kwa Boban aliyemalizia kirahisi kazi kubwa iliyofanywa na Sunzu aliyempokonya mpira beki wa Shandy ambaye alionekana hajui afanyie nini mpira uliokuwa miguuni mwake jirani na lango lao.

Mafisango alirekebisha makosa ya kudakwa kwa penalti yake ya kipindi cha kwanza, kwa kuifungia Simba goli la pili katika dakika ya 77 kufuatia juhudi binafsi za Okwi aliyewatoka kiufundi mabeki wa Shandy kabla ya kumtengea mfungaji aliyekuwa akipita kwa kasi kuelekea katika lango la wageni.

Penalti ya Simba ilipatikana baada ya kipa wa Shandy, Abdelrahman Ali, kudaka miguu ya Okwi aliyekuwa akielekea kufunga.

Kipa Ali ambaye alikuwa na bahati kutopewa kadi nyekundi katika tukio hilo alilopewa ya njano, aliruka upande sahihi wa kushoto na kudaka penalti hiyo na kulipa fadhila za wachezaji wenzake waliomzunguka kumpa matumaini kabla ya kupigwa kwa adhabu hiyo.

Okwi aliyeonekana kuwa hakabiki na hivyo kuchezwa faulo mara kwa mara, alikamilisha ushindi mnono kwa Simba katika dakika ya 88 kutokea nje kidogo ya boksi baada ya kukanyagiwa mpira na Boban na kufumua shuti lililotinga wavuni na kumwaka kipa Ali akiwa amekaa chini asiamini kilichowakumba katika dakika za mwisho.

Hata hivyo, wageni watajilaumu kwa kupoteza nafasi kadhaa ikiwemo shuti lililoenda nje kutokea jirani na lango wakati wenyeji wakiongoza mbili 2-0, na wangeweza pia kupata bao la kufutia machozi wakati Sadam Abu Talib alipokaribia kufunga goli kama la Diego Maradona baada ya kukimbia na mpira kutokea mbele ya boksi lao na kuchanja mbuga katikati ya uwanja huku akiwapita wachezaji wa Simba waliounga tela nyuma kumfukuza hadi alipofika nje ya boksi na kupiga shuti kali la juu lililookolewa na Kaseja na kuwa kona.

Mchezaji mwingine aliyeng'aa wa Simba kama kawaida yake licha ya kuchezeshwa katika namba tofauti, alikuwa ni yosso Shomari Kapombe, ambaye alicheza kama beki wa kati kuchukua nafasi ya Juma Nyosso aliye majeruhi, na kufanya sasa kuwa amecheza na kung'aa katika nafasi zote uwanjani isipokuwa nafasi ya kipa na mshambuliaji wa kati.

Endapo itaing'oa Shandy, Simba ambayo tayari imezitoa Kiyovu ya Rwanda na ES Setif ya Algeria katika hatua za awali, itakuwa miongoni mwa timu 8 zitakazoungana na timu 8 zitakazotolewa katika Ligi ya Klabu Bingwa, ambapo kila moja itapangiwa nyingine katika mechi mbili za mtoano nyumbani na ugeni, na nane zitakazopita zitacheza hatua ya makundi.

Vikosi vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Nasoro Said 'Chollo', Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Patrick Mafisango, Uhuru Selemani/ Machaku Salum (dk. 88), Mwinyi Kazimoto, Emmanuel Okwi, Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu.

Shandy: Abdelrahman Ali, El Nour Altigani, Issacc Seun-Malikh, Sadam Abu Talib, Fareed Mohammed, Zakaria Nasu, Razak Yakubu, Faris Abdalla, Hamouda Bashir, Nadir Altaueb na Bassiro Ubamba.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles