Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tume ya Katiba Mpya kuanza kazi leo

1st May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba.

Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania inaanza rasmi kazi yake ya miezi 18 leo.

Kwa maana hiyo tume hiyo inaweza kuanza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maoni hayo yatatolewa ama kwa tume kuwaendea wananchi moja kwa moja au kwa kutumia barua, au baruapepe au kwa njia nyingine zozote itakazoona zinafaa.

Baada ya tume kukusanya maoni ya wananchi, itawasilisha ripoti kwa rais na zitafuatia hatua mbili mambazo ni kuundwa kwa Bunge Maalum la katiba ambalo litachambua rasimu hiyo, kisha wananchi watapiga kura ya maoni kuikubali au kuikataa. Katiba Mpya inatarajiwa kupatikana ifikapo Aprili 26, 2014, ambayo itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, aliliambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kuwa watatoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kazi inayoanza kufanywa na tume leo mara tu watakapomaliza kukutana.

“Ngoja tukishakaa tutawaambia,” alisema Jaji Warioba alipotakiwa na NIPASHE kueleza nini tume yake inaanza kufanya leo.

Tume hiyo yenye wajumbe 30, ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 6 na kuapishwa naye Aprili 14, mwaka huu. Itafanya kazi kwa miezi 18.

Tume hiyo inaongozwa na Jaji Warioba akisaidiwa na Makamu wake, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhan.

Wajumbe wengine kwa upande wa Tanzania Bara, ni Profesa Mwesiga Baregu na Dk. Sengondo Mvungi. Wengine Profesa Palamagamba Kabudi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Yahya Msulwa.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Maria Kashonda, Mwantumu Malale, Esther Mkwizu, Humphrey Polepole, Jesca Mkuchu, John Nkolo, Riziki Mngwali, Richard Lyimo na mwanasheria maarufu, Said El- Maamry.

Kwa upande wa Zanzibar, wamo Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU, sasa AU), Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Salim Hamadi na mwanahabari Ally Saleh wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Wengine ni Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed na Abubakar Mohammed Ali.

Tume hiyo iko chini ya Katibu Assaa Ahmad Rashid na msaidizi wake, Casmir Sumba Kyuki ambaye ni Mwandishi Mkuu wa Sheria katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Mara baada ya kuiapisha, Rais Kikwete aliitaka tume hiyo kuhakikisha inafanya kazi kwa maslahi ya wananchi kwa kufuata maadili na kuepuka shinikizo lolote kutoka kwenye makundi. Alisema tume hiyo inatakiwa kufanya kazi yake kwa umakini na kuheshimu maoni ya wananchi wote.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles