Saturday May 7, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Azam yaipumulia Simba ubingwa

1st May 2012
Print
Comments
Winga wa Azam, Mrisho Ngassa (kulia) akiwania mpira dhidi ya Ladislaus Mbogo wa Toto African wakati wa mechi yao ya ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye uwanja wa Chamanzi jijini Dar es Salaam jana.

Azam ilitoa kipigo cha magoli 3-1 dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam na kuacha nafasi ya ubingwa kuwa wazi ikisubiri kuamuliwa katika mechi za mwisho wa msimu Mei 5 wakati timu zote 14 za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zitakaposhuka viwanjani kote nchini.

Kama Azam watashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi watafikisha pointi 59, sawa na walizonazo sasa vinara Simba, ambao itawalazimu kushinda mechi ngumu dhidi ya watani zao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi.

Ushindi kwa Azam na kipigo kwa Simba utawapa Azam ubingwa wao wa kwanza wa Bara katika historia miaka minne tangu wapande ligi kuu, lakini Simba inahitaji japo pointi moja tu kutoka kwa Yanga ili kubeba taji lao la 18 tangu ligi hiyo ya juu ilipoanzishwa mwaka 1965, huku ikiwa ndiyo timu ya kwanza kihistoria kutwaa ubingwa huo.

Yanga inayoongoza kwa kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa huo (mara 23), imevuliwa ubingwa msimu huu na haina nafasi hata ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika msimu ujao kwa sababu haitaweza kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu, ikiwa imekwamia kwenye nafasi ya tatu.

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche alifunga magoli mawili na kinara wa mabao John Bocco alipachika goli lake la 17 la ligi msimu huu wakati wenyeji walipoenda mapumziko wakiongoza kwa magoli 3-0 jana.

Tchetche aliunganisha kwa kichwa mpira wa krosi ya Ibrahim Mwaipopo na kuipatia Azam bao la kwanza katika dakika ya 10 na dakika tisa baadaye, Tchetche tena alifanya matokeo yao 2-0 kwa kufunga goli lililotokana na mabeki wa Toto kushindwa kuokoa mpira uliopigwa na Bocco.

Bocco ambaye hatarajiwi kuifikia rekodi ya jumla ya ufungaji mabao katika ligi hiyo ya juu zaidi nchini ambayo inashikiliwa Abdallah Juma ya magoli 25, alipatia Azam goli la tatu katika dakika ya 37 baada ya ushirikiano mzuri na Tchetche. Baada ya goli hilo, Toto walimtoa kipa wao Mustapha Mabrouk na kumuingiza Sunga Ramadhani.

Huku timu tatu za Mgambo Shooting ya Tanga, Polisi Morogoro na Prisons ya Mbeya zikiwa zimeshapanda daraja kwa ajili ya kucheza ligi kuu msimu ujao, Polisi Dodoma na Moro United zimeshateremka huku nafasi moja zaidi ya kudondoka ikiziandama timu tatu za Toto African, Villa Squad na African Lyon.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles