


.jpg)
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, amemtaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam aingilie kati kuwezesha matengenezo ya haraka ya barabara zenye kupunguza msongamano na kero kwa wananchi
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mnyika alisema, barabara hizo ni zile ambazo manispaa ya Kinondoni imeshindwa kuzikarabati katika mwaka wa fedha 2011/2012 kwa kukosa ruzuku ya kutosha toka serikalini jambo lililopelekea kupungua kwa mapato ya ndani.
Aidha, Mnyika aliitaka Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam kutuma timu yake ya ukaguzi wa barabara kufuatia ujenzi wa njia ya mabasi yaendayo kasi katika barabara mbadala za kupunguza foleni kwenye barabara ya Morogoro
Katika taarifa hiyo, Mnyika, aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kufanya ukaguzi na kudhibiti ongezeko holela la bei na adha kwa wasafiri kwa visingizio vya ubovu wa barabara ambao kwenye baadhi ya maeneo imefikia kiwango cha nauli ya Shilingi 1,000 kwa abiria mmoja kwa umbali mfupi.
“Baadhi ya barabara hizo zilizo katika hali mbaya ni pamoja na barabara ya Kibangu mpaka Makoka, barabara ya Maziwa mpaka External, na barabara ya Kimara mpaka King’ongo,” alisema Mnyika.
Alisema, Barabara ya Makoka ilitengewa Sh. milioni 100 katika mwaka wa fedha 2011/2012 kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo, lakini mpaka sasa ikiwa imebaki miezi miwili mwaka husika kumalizika zabuni ya matengenezo ya barabara husika haijatangazwa kwa kuwa serikali kuu bado haijatoa fedha kiwango husika kama ilivyoahidi.