Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

JWTZ lacharuka

26th May 2012
Print
Comments
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Jenerali Davis Mwamunyange

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, amecharuka na  kusema kuwa jeshi hilo limeanza kuchunguza tuhuma kuhusu baadhi ya wanajeshi wake kuingia kwenye jeshi hilo kwa kutumia vyeti vya watu wengine kwa lengo la kujipatia ajira.

Jenerali Mwamunyange alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya wakuu wa wizara, idara na taasisi mbalimbali za serikali katika masuala ya ulinzi na usalama yaliyofanyika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Kunduchi jijini Dar es Salaam.

 “Baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kutufahamisha kuhusu baadhi ya kasoro za waajiriwa wetu jeshini kuhusiana na vyeti, basi tumeanza kuchukua hatua na iwapo itabainika wapo waliofanya udanganyifu, basi hatua zinazostahili zitachukuliwa kwa walengwa,” alisema Jenerali Mwamunyange.

Alisema jeshi lake halitawafumbia macho watumishi watakaobainika kutumia vyeti ambavyo si vyao, kwani kufanya hivyo ni kulidhalilisha jeshi.

Hata hivyo, Jenerali Mwamunyange alitoa wito kwa vijana wanaohitaji kujiunga na jeshi hilo kuwa lazima wawe wazalendo na nchi yao, kulinda usalama wa raia na mali zao na wala wasiingie jeshini kwa minajili ya kujitafutia pesa pale wapatapo ajira.

“Lazima wazazi wahakikishe wanawalea vijana wao katika mazingira mazuri ya kinidhamu ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), liwe na heshima na nidhamu kubwa,” alisema.

Mkuu huyo wa Majeshi amezungumza hayo baada ya hivi karibuni NIDA kudai Jeshi la Wananchi limeajiri vijana 248 na lile la Polisi likiwa limeajiri vijana 700 ambao majina ya vyeti vyao yanafanana na watumishi wengine serikalini.

Lakini baada ya kauli hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu, kutangazwa na vyombo vya habari, mamlaka hiyo ilikanusha na kuonekana kusahihisha kauli hiyo kupitia matangazo mbalimbali kwenye vyombo vya habari.

Wakati huohuo, akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo yaliyojumuisha washiriki 30 toka mikoa mbalimbali nchini, Jenerali Mwamunyange alisema kimsingi hayakuwa mafunzo bali ni kikao cha kutafakari madhumuni ya chuo hicho ambacho kitaanza kufanyakazi Septemba mwaka huu.

Alisema lengo ni kukusanya viongozi mbalimbali toka idara, taasisi za mashirika ya umma kujifunza masuala ya usalama wa taifa.

 

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles