Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Msiba wa Kanumba waleta ukombozi kwa wasanii

11th April 2012
Print
Comments
Makamu wa rais, Gharib Bilal, akitoa heshima zake za mwisho mbele ya jeneza lililobeba mwili wa muigizaji namba moja wa filamu nchini, Steven Kanumba, kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.(Picha: Selemani Mpochi)

Licha ya kifo cha muigizaji Steven Kanumba aliyezikwa jana kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kuacha majonzi makubwa kwa Watanzania na mashabiki wake wa nje ya nchi, msanii huyo nyota anaelekea kuleta ukombozi wa aina yake kwa wasanii wenzake nchini.

Hilo limefahamika jana baada ya Serikali kutangaza kwamba kuanzia Julai, wizi wa kazi za wasanii nchini utafikia mwisho kwa vile tayari suala hilo litapatiwa ufumbuzi.

Serikali imeongeza kwamba itasimamia mchakato wa kuhakikisha kuwa wasanii wote nchini wananufaika na jasho la kazi zao, lakini ikawataka watoe ushirikiano ili kumaliza kilio hicho cha muda mrefu kutoka kwa wadau wa sanaa.

Akizungumza kwa niaba ya serikali jana kabla ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Kanumba, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa kufikia Julai, zoezi rasmi la kuhakikisha kuwa haki za wasanii zinalindwa litaendeshwa baada ya kuanza kwa kikao cha bunge la Tanzania.

Nchimbi alisema kuwa anaamini zoezi hilo litasaidia wasanii kulipwa fedha kutokana na jasho lao na kukomesha unyonyaji dhidi yao.

"Mwaka huu ndio mwisho, tunataka kuona kuwa kuibiwa kazi za wasanii kunamalizika, sasa tunataka kuona wasanii wanalipwa fedha zinazolingana na jasho lao," alisema Waziri huyo.

Alisema kuwa serikali imepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na inaona kuwa kifo chake kimetokea mapema sana kutokana na umri mdogo aliokuwa nao.

Aliongeza kuwa Kanumba alikuwa mahiri na alifanya kazi hiyo kwa kupambana vyema na mazingira ya kila aina aliyokutana nayo.

"Mamilioni ya watu wanaomlilia yanaonyesha kwamba walitambua kazi ya sanaa aliyokuwa akiifanya, alijituma na alijitahidi, ametoa filamu zaidi ya 40 na aliendelea kufanya hivyo wakati wengine wakiandaa filamu moja wanadai kuwa (tayari) wameshatoka (wametajirika)," aliongeza.

Aliwataka wasanii waendelee kufanya kazi kwa bidii, wapendane na wamalize migogoro baina yao ili zoezi la kudhibiti wezi wa kazi zao litakapoanza mwezi Julai lifanyike kwa tija.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Mr II - Sugu', alisema kuwa mafanikio ya marehemu Kanumba yawe changamoto kwa vijana wengine na hiyo ilitokana na msanii huyo kutokata tamaa.

Sugu alisema kuwa maelfu ya watu waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa msanii huyo ni ishara kuwa alikubalika, hivyo kilichobaki ni kuenzi mafanikio yake.

Alisema kuwa baada ya kualikwa kwenye jumba la Big Brother nchini Afrika Kusini, yalisemwa mengi lakini msanii huyo hakukata tamaa na aliendelea kuandaa filamu mbalimbali, zikiwemo alizowashirikisha wasanii kutoka Ghana na Nigeria kama Ramsey Nouah.

Salamu zilizotolewa na Shirikisho la Wasanii wa Filamu Tanzania (TAFF) zilisema kuwa wamepoteza 'komandoo' wao na wameumia sana kwa kifo hicho.

Walisema kuwa marehemu Kanumba alikuwa ni balozi pekee ndani na nje ya nchi na uwezo wake aliouonyesha wataendelea kuutambua katika maisha yao yote huku pia wakiongeza kwamba aliweza kukitangaza vyema Kiswahili, hadi nje ya mipaka ya Tanzania.

Nyota wa bongofleva, Diamond, alisema kwamba alipata mshituko kusikia kifo cha msanii huyo ambaye kama si mashambulizi ya Al Shabaab, alipaswa kusafiri naye Ijumaa kuelekea Mombasa katika mwaliko maalum waliokuwa wameupata.

Diamond alisema kwamba marehemu Kanumba alikuwa ni kioo na hata wao waliweza kutumia jina la msanii huyo kujitambulisha kwamba wanatoka Tanzania ambako ndiko msanii huyo wa filamu (Kanumba) alikozaliwa na anakoendelea kuishi.

Mwili wa marehemu Kanumba uliwasili kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni saa 4:05 asubuhi na kupokelewa kwa vilio kutoka kwa maelefu ya wakazi waliofika kutoa heshima zao za mwisho na wa kwanza kuaga alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohammed Gharib Bilal. Wengine waliofuatia walikuwa ni mawaziri na viongozi wengine wa serikali, wabunge na pia familia yake.

Hata hivyo, mashabiki wa Kanumba walishindwa kumuaga kipenzi chao kutokana na uwingi wa watu na hivyo wakatakiwa kujipanga barabarani kuelekea makaburini huku gari lililobeba mwili wa marehemu likipitishwa katikati kwa mwendo wa taratibu.

DILI
Katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, maelfu ya wananchi waliokuwa wakienda katika mazishi ya Kanumba, kwenye viwanja vya Leaders na baadaye katika makaburi ya Kinondoni walikumbana na adha ya aina yake iliyotokana na wingi wao.

Waombolezaji kutoka katika maeneo mengi walitozwa nauli kubwa ya daladala badala ya Sh. 300 hadi 500 iliyozoeleka. Baadhi ya daladala kutoka Temeke, Tandika na Mbagala zilitoza nauli ya ya Sh. 1,000 kwenda kwenye viwanja vya Leaders, huku wale wa maeneo kama ya Magomeni, Mwenge, Sinza, Manzese na Ubungo wakitozwa Sh. 500 badala ya nauli ya kawaida ya Sh. 300 na 400.

Kuanzia mishale ya saa 4:00, kulikuwa na foleni ndefu ya magari kutoka Magomeni Hospitali kuelekea Kinondoni na hivyo, baadhi ya waombolezaji walionekana wakiandamana kwa miguu kwenda kuhuhudhuria mazishi ya Kanumba.

Wenye pikipiki na bajaji walipata wateja wengi zaidi kutoka Magomeni kwani wao walikuwa wakitumia barabara ya waendao kwa miguu kupitisha vyombo vyao. Hata hivyo, kwenye bonde la Mkwajuni, baadhi ya vijana walitumia fursa hiyo kujiingizia kipato kwa kuziba njia ya watembeao kwa miguu kwa mawe na magogo, wakiwalazimisha wenye bajaji kulipa kati ya Sh. 300 na 500 kabla ya kuwaruhusu kupita.

Kanumba alizaliwa Januari 8 mwaka 1984. Alifariki usiku wa Jumamosi ya Aprili 7 wakati akiwa nyumbani kwake Sinza Vatican.

Mungu ailaze roho ya marehemu Kanumba mahali pema peponi. Amina!

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment