Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wakati ni huu wanachama Yanga

7th July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Kampeni za uchaguzi mdogo wa Yanga zilianza jana kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi, za viongozi, kufuatia kujiuzulu kwa wajumbe wengi wa kamati ya utendaji waliochaguliwa na mmoja kufariki dunia.

Uchaguzi huu unakuja miaka miwili baada ya uchaguzi mkuu na kimsingi, tunaona Nipashe, kadhia hii ni jambo la kujitakiwa kwa Yanga kama klabu.

Ni jambo la kujitakia kurudia 'kazi' ya miaka miwili tu iliyopita; iliyotakiwa kudumu kwa miaka minne kwasababu palikuwa na kila dalili kwamba wanachama wa Yanga hawakuwa makini katika chumba cha uchaguzi mwaka 2010.

Hawakuwa makini kwasababu safu ya uongozi iliyochaguliwa ilikuwa ni tofauti na ile iliyokuwa ikizungumzwa zaidi wakati kampeni za miaka hiyo miwili iliyopita zikielekea ukingoni.

Hatuna uhakika, Nipashe, ni kipi hasa kilipelekea wanachama wa Yanga kutoka ukumbini na safu ambayo ilianza kukwaruzana muda mfupi baada ya upigaji kura za viongozi hao.

Lakini ambacho tuna hakika nacho Nipashe ni kwamba wanachama wa Yanga wamepata nafasi ya pili ya kuwaweka upya ofisini mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.

Si mara nyingi kwa wanachama kupata nafasi hizi za pili, shukrani kwa katiba mpya za klabu zenye msingi wa shirikisho la kimataifa la soka (FIFA), Yanga ni lazima wakumbuke.

Yanga ni lazima wakumbuke kwasababu ni moja ya klabu zenye historia ndefu ya migogoro ya uongozi na iliyodumu kwa muda mrefu kiasi cha kufikia kuigawa mara moja mwishoni mwa miaka ya 1970, na kunusurika kugawanyika safari ya pili kwenye miaka ya katikati ya 1990 mpaka mwanzoni mwa karne hii.

Hivyo wakati zikiwa zimebaki siku saba za kampeni, ni wakati wa wanachama wa Yanga kuwapima kwa makini wagombea wote na kugundua uwezo wao katika KUONGOZA.

Ni uwezo wa mwanachama katika kuongoza tu unapaswa kuwa kigezo kikuu cha kuchaguliwa kwake kwani kuna mengi zaidi ya cheo cha kiongozi katika klabu kubwa kama ya Yanga ambayo inapaswa kuwa dira la maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.

Aidha, Yanga ni klabu ya wanachama iliyoanzishwa kwa lengo la kupigania vikombe na kuleta raha kwa wanachama wake na tunataraji, Nipashe, itabaki kuwa hivyo.

Ili lengo hili la kupigania vikombe litimie, mikakati makini ya muda mrefu hasa ndiyo nguzo. Hivyo patahitajika viongozi ambao wana uono wa mbali katika kuijenga klabu tangu chini ili kuja kuwa na timu tishio endelevu baadaye.

Badala ya wanachama kuangalia ahadi za mafanikio ya muda mfupi yanayoweza kuletwa na karama yoyote iliyopo miongoni mwa wagombea, tunawashauri wanachama wa Yanga kutumia busara yao katika kupima na kisha kupata viongozi bora ifikapo Julai 15.

Waamuzi wake makini Kagame

Baraza la vyama vya soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetangaza orodha ya waamuzi 15 watakaochezesha michuano ya wiki mbili ya Kombe la Kagame ya klabu bingwa ya ukanda huo itakayoanza jijini Jumamosi ijayo.

Kutangazwa kwa waamuzi hao ni hatua nyingine ambayo inasogelea kuanza kwa michuano yenyewe ya 38 uwanjani wakati huu timu shiriki zikisubiriwa kuanza kuwasili nchini.

Lakini kutangazwa kwa orodha hiyo ya waamuzi pia kunatukumbusha jinsi kiwango cha maamuzi katika michuano ya miaka ya karibuni ya Kombe la Kagame kilivyo cha chini kiasi cha kuwepo kwa hisia ya timu wenyeji kubebwa dhahiri.

Si nia yetu, Nipashe, kurudia matukio ya udhaifu katika uamuzi yaliyojitokeza katika miaka ya karibuni na hasa sasa ambapo michuano hii inafanya nchini kwa mwaka wa pili mfululizo.

Si nia yetu kwasababu, tunafahamu Nipashe, makosa ya kibinadamu ni sehemu ya mchezo wa soka na ni moja ya mabo yanayofanya mchezo wenyewe uwe wa kusisimua zaidi.

Lakini itakuwa ni makosa kama waamuzi watapinda sheria makusudi kuzibeba timu wenyewe kwa kivuli cha uwepo wa uvumilivu katika makosa ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na muamuzi husika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment