


Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba jana waliendelea kutoa misaada ya kijamii katika kituo cha watoto yatima cha Maunga Centre jijini Dar es Salaam huku mshambuliaji wao Mganda Emmanuel Okwi akigombewa na watu mbalimbali waliofika kituoni hapo.
Okwi, ambaye juzi alitangazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Simba wakati wa tamasha la klabu hiyo, Simba Day, lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, aligombewa na mashabiki waliokuwa wakitaka kupiga picha naye, kushikana naye mikono au kumpongeza.
Akiongea na viongozi na watoto wa kituo hicho, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alisema klabu yake imeamua kutembelea kituo hicho ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuwa karibu zaidi na jamii ya Watanzania iliouanzisha katika kuadhimisha wiki maalum ya klabu hiyo 'Simba Week', ambayo itakuwa ikifanyika kila mwaka kuanzia Agosti 5-10.
“Simba inatambua matatizo yanayowakabili watoto, hususan watoto waliopoteza wazazi wao. Leo (jana) tumekuja kuwafariji na tutawapatia mchele, mafuta sabuni na vifaa vingine vingi tu,” alisema Kaburu.