


.jpg)
Mwenyekiti wa Yanga aliyekalia kiti moto, Lloyd Nchunga amekubali kuitisha mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa klabu hiyo mwezi ujao.
Akizungumza na NIPASHE jumapili jana, Nchunga alisema wanachama wa Yanga wana haki ya kikatiba kudai mkutano mkuu na yuko tayari kuitisha mkutano huo.
Juzi baadhi ya wanachama wa Yanga na Baraza la Wazee wa klabu hiyo wakiogozwa na Ibrahim Akilimali walisema wamegundua kuwa hakuna kizuizi cha mahakama cha kufanyika kwa mkutano mkuu wa Yanga kama ambavyo uongozi wa Nchunga ulikuwa ukidai.
“Kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kinatukwamisha kama vongozi kuitisha mkutano mkuu, lakini kwa sasa suala hilo halipo," alisema Nchunga.
"Tunaanza mara moja mchakato wa kuitisha mkutano mkuu."
Alisema kuwa mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu leo, atatoa notisi ya siku 30 ya kuitisha mkutano huo siku yoyote kuanzia kesho.
“Kwa sasa siwezi kutaja siku rasmi ya kufanyika mkutano huo, lakini ninachoweza kusema ni kwamba mchakato wa kuitisha mkutano utafanyika kuanzia Jumatatu baada ya kumalizika kwa ligi kuu,” alisema Nchunga.
Alisema kuwa baada ya kutoa notisi hiyo ya siku 30, ataziagiza kamati ndogo ndogo kuandaa mambo muhimu ya mkutano huo.
Wanachama na viongozi wa Baraza la Wazee walimtaka Nchunga kuitisha mkutano huo kwa kuwa waligundua zuio la mahakama lilotolewa baada ya baadhi ya wanachama kwenda Mahakamani kupinga kufanyika mkutano mkuu wa klabu hiyo Septemba mwaka jana limepita muda wake.
Katika hatua nyingine, Nchunga amewajia juu baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wanaopotosha ukweli juu ya klabu hiyo huku wakimshambulia yeye.
Nchunga alisema kuwa mashabiki hao wanaeneza propaganda na kuwataka kuacha mara moja.
Alisema kuwa yeye si sababu ya klabu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Bara.
“Hizi ni propaganda tu, timu kushika nafasi ya tatu haina maana kuwa mimi nimeshindwa kuiongoza," alisema.
"Wengi wanajua Yanga wamepoteza ubingwa kutokana na mambo ya nje ya uwanja ikiwemo kitendo cha kupokonywa pointi tatu na kamati ya ligi kuu baada ya ushindi wetu dhidi ya Coastal Union.
"Lakini watu hawataki kusema ukweli na kuamua kunisakama mimi.”
Aidha, alisema kuwa hata kabla yeye hajakalia kiti cha uongozi, klabu hiyo imewahi kumaliza ligi katika nafasi ya tatu na kuna mwaka ilimaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tano na kuhoji kwa nini mwaka huu Yanga imeshika nafasi ya tatu wanaandamwa viongozi; hususani yeye.
Alisema mkutano huo mkuu utasaidia kuweka mambo sawa na kurudisha umoja wa klabu hiyo.