Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Bunge kuchunguza kina cha udhaifu

3rd February 2013
Print
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia

Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia, ameiwasilisha ya kutaka Bunge liunde Kamati Teule itakayochunguza udhaifu uliopo katika sekta ya elimu na kupendekeza hatua za kuchukua ili taifa liondokane na aibu ya udhaifu huo hatarishi katika mfumo wa elimu hapa Tanzania.

Hii ni sehemu ya hotuba yake bungeni mjini Dodoma:

Kwa kuwa tangu Taifa letu lipate uhuru wake mwaka 1961 (kwa Tanganyika) na mwaka 1964 (Mapinduzi ya Zanzibar) tulitambua umuhimu wa kufuta ujinga, kwa kuelimisha wananchi ili tujiletee maendeleo, na hadi sasa kazi kubwa imefanyika katika kukuza elimu hapa nchini;

Kwa kuwa, katika Dira ya Taifa ya 2025 tunataja, pamoja na mambo mengine kwamba, ifikapo mwaka 2025 tuwe tumejenga taifa la watu walioelimika kwa upeo wa juu katika nyanja mbalimbali;

Kwa kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambao una malengo nane ya milenia, lengo la pili likiwa ni upatikanaji wa elimu bora kwa wote (achieving universal primary education);

Kwa kuwa, ifikapo mwaka 2015 (takribani miaka miwili toka sasa) tutalazimika kama taifa kupima utekelezaji wa malengo hayo ya milenia ili kuendana na viwango vya kimataifa;

Na kwa kuwa, kwa muda mrefu kumekuwepo na viashiria vingi vinavyoonesha kwamba ubora wa elimu itolewayo hapa nchini katika ngazi zote hauridhishi;

Hivyo basi, ipo haja ya kutathmini kwa undani hali ya elimu nchini na kuchukua hatua stahiki.

OMBI NA UHALALI WA KUTOA HOJA HII

Kwa mujibu wa kanuni ya 56(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007, naomba kutoa hoja binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu hapa nchini na haja ya kukomesha udhaifu huo.

Pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo Serikali, kupitia Wizara yenye dhamana ya Elimu imefanikiwa kuifanya kwa muda mrefu, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba hivi sasa elimu itolewayo katika taifa letu ina udhaifu mkubwa sana. Udhaifu huo unajidhihirisha katika sura mbalimbali ambazo miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

Tabia ya Watanzania wengi kutothamini matumizi ya muda, kupotoka kwa mila, desturi na utamaduni wa jamii ya Watanzania,kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma na kada nyinginezo, kuporomoka kwa uwajibikaji.

Kuporomoka kwa kiwango cha utii wa Sheria na Kanuni mbalimbali, Kutokuthamini rasilimali za taifa,kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, kukua kwa utamaduni wa ukupe, kupungua kwa uzalendo kwa baadhi ya wananchi.

Kutojiamini kwa Watanzania wanaohitimu elimu katika ngazi mbalimbali na kukua na kukomaa kwa migogoro ya mara kwa mara katika sekta ya elimu.

Sura tajwa hapo juu ndizo chanzo kikuu cha matatizo tuliyonayo nchini, katika utoaji wa huduma na shughuli za uzalishaji. Matatizo hayo ni kama yafuatayo :

Uduni wa elimu (yenyewe) itolewayo katika ngazi mbalimbali za elimu nchini, unaojidhihirisha katika viwango vya chini, ufaulu wa wanafunzi katika mitihani, pamoja na uelewa mdogo wa wahitimimu, huduma mbovu zitolewazo katika sekta mbalimbali na viwango duni vya ubora wa bidhaa za viwandani, majengo, na miundombinu.

Uzalishaji usiotosheleza, tena usioridhisha wa bidhaa za mashambani, uharibifu na uchafuzi wa mazingira,udhaifu katika kukabiliana na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na tetemeko la ardhi, udhaifu katika kuzuia na kudhibiti ajali zinazoweza kuzuilika, kama vile ajali za vyombo vya usafiri, moto na milipuko ya silaha;

Udhaifu katika kukabiliana na hatari za kiafya kwa binadamu na wanyama zitokanazo na uchimbaji migodini na usafirishaji au uhifadhi wa kemikali, migomo ya Waalimu, Wanafunzi, Wanataaluma pamoja na makundi ya kijamii inayojitokeza katika ngazi mbalimbali.

Ukosefu wa nidhamu ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) mfano matumizi ya simu nururu (mobile phones) na mitandao ya kijamii wakati wa kazi bila kuzingatia umakini kwenye kazi mtu anoyafanya.

UDHAIFU KATIKA MFUMO RASMI WA ELIMU

Udhaifu uliopo katika sekta ya elimu hususan mfumo wa utoaji elimu ndicho kirusi kilichoambukiza udhaifu kwenye sekta nyingine zote katika taifa letu. Sababu za msingi za kusema haya ni hizi zifuatazo:

Maendeleo ya taifa lolote (kijamii, kiteknolojia, kiuchumi na kisiasa) ni tunda la mfumo wake wa elimu, uhai wa taifa lolote hutegemea wingi na matumizi ya wananchi wake walioelimika vyema. Kwa lugha nyingine, upo uhusiano sababishi kati ya elimu duni na ukengeufu katika jamii na hatimaye utendaji dhaifu katika uchumi na siasa za nchi. Uhusiano huu umethibitika kitaalamu.

Kwa ajili ya kuokoa muda, nitazungumzia sehemu ndogo tu ya udhaifu uliopo katika mfumo wetu rasmi wa elimu.

Hoja kwa kielelezo:

Matokeo ya Utafiti niliofanya, kwa takribani miaka 18 sasa, yanaonesha ya kwamba udhaifu wa mfumo wetu rasmi wa elimu unatokana na mambo makuu matatu, ambayo hapa nchini imekuwa ni nadra kuyaangalia kwa undani tunapoendelea kutafuta ni kwa nini tumekwama katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Mambo hayo ni:

Sera ya Elimu ya Taifa ya tangu mwaka 1995 na sera nyinginezo, mitaala ya elimu ya shule za msingi na sekondari na mihtasari ya masomo na vitabu vya kiada na ziada vitumikavyo katika shule za msingi na sekondari.

TATIZO LA SERA YA ELIMU TAZANIA

Sera ya Elimu ya Taifa inayotumika kwa sasa imekuwepo kwa muda mrefu. Ukweli huo tu watosha kuwa na haja ya kuifanyia tathmini kubwa sera hiyo, ili licha ya kuangalia nini tumetekeleza na nini hatukutekeleza tuifanye iendane na mahitaji yetu ya sasa. Ninatambua hatua zilizokwisha chukuliwa na wizara husika, lakini kusudio la kuwa na sera mpya ambayo inajenga kizazi cha Watanzania katika misingi iliyo bora halijafanikiwa.

Aidha, miongoni mwa mambo yaliyo bayana kwa sasa ni kwamba masuala mengi ya kisera katika elimu, tunayoyafuata hapa nchini, yametokana na masharti na/au maelekezo tuliyopewa na vyombo vya kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Hata hivyo, maelekezo ya vyombo hivi badala ya kutusaidia kuinua ubora wa elimu hapa Tanzania yametuletea matokeo yasiyokuwa mazuri na yanayotuyumbisha.

Mathalani, miaka ya 1980 vyombo hivi vilitutaka tupunguze matumizi ya rasilimali za umma katika kugharamia huduma za jamii ikiwemo Elimu, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa uduni wa shule za umma nchini.

Kana kwamba haitoshi, vyombo hivi viliwahi kututaka tuelekeze zaidi rasilimali katika elimu ya msingi tu na kutuambia kwamba elimu ya juu ni anasa. Lakini miaka ya hivi karibuni vimebadili ushauri huo na kudai rasilimali zaidi zielekezwe katika elimu ya juu.

Ni kana kwamba tumegeuzwa kuwa sampuli ya kufanyiwa majaribio katika maabara za sera za elimu bila kujali athari mbaya zitokanazo na majaribio hayo.

Kama taifa tunapaswa kutumia sera ambazo zimethibitika kitaalamu kwamba zinaleta matunda yanayotakiwa. Tusiendelee kuyumbishwa na vyombo ambavyo sera vinazozisimamia si za maslahi kwetu, kwa sababu tu sisi ni wahitaji wa misaada yao.

TATIZO LA MITAALA

Sanjari na matatizo hayo ya sera ya elimu nchini, ni jambo la kusikitisha sana kwamba hadi mwaka 2011, nchi yetu haikuwahi kuwa na mitaala rasmi ya kitaifa kwa ajili ya Elimu ya shule za msingi au sekondari.

Ijapokuwa wanasiasa, wanaharakati na wanataaluma wamekuwa wakiilalamikia wizara ya elimu kuwa na mitaala mibovu, lakini ukweli ni kwamba mitaala hiyo haikuwahi kuwepo. Hatujawahi kuwa na andiko mahususi la mtaala wa elimu kwa Taifa la Tanzania. Kwa mantiki hiyo, kwa miaka mingi tumekuwa na chombo ‘ mfumo wa elimu’ lakini kisicho na usukani.

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imekuwa ikiajiri wakuza mitaala kwa zaidi ya miaka 15, bila ya kutoa mitaala yoyote katika namna ya andiko mahsusi. Mitaala ipi inayokuzwa? KulikoniI?

Nitoe angalizo pia, kwamba nyaraka za wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi zina ainisho la dhana ya mitaala ambalo kwa kiasi fulani ainisho hilo nalo linatoa mtazamo usiotuwezesha kutambua mitaala tunayotakiwa kuwa nayo kwa mapana yake. Ukiangalia kwa mfano, rasimu ya pili ya sera mpya ya elimu inaeleza mtaala kama ifuatavyo :

‘Mtaala wa Elimu ni jumla ya mambo ambayo mlengwa anatakiwa kuyapata katika mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa lengo la kufikia matarajio ya jamii na taifa’

Ainisho hili lina ukweli kiasi, lakini lugha yake ni ya jumla jumla sana. Mathalani, maneno yaliyotumika ; ‘ mtaala … ni jumla ya mambo …’ sio maelezo mahsusi, maana hayaelezi ni mambo gani hasa ambayo mlengwa anatakiwa kuyapata.

Aidha, ainisho halitaji madhumuni hasa (purpose) ya utoaji elimu, halifafanui mchakato wa utoaji elimu hiyo (unafanyikaje na unafanyikia wapi), halielezi vigezo na namna ya kupimwa kwa ufikiaji malengo ya elimu, na wala halitaji wazi wazi matokeo tarajiwa ya elimu itarajiwayo.

Laiti kama nyaraka zetu zingetaja kuwa mtaala ni jumla ya maarifa, maadili, ujuzi na uzoefu anaotakiwa kuupata mwanafunzi katika mazingira ya kufundishwa na kujifunza, ainisho hilo lingekuwa wazi zaidi.

Tunapaswa kuzingatia pia kwamba mtaala ni mchakato (mchakato huo ni lazima tuuseme). Mtaala ni jitihada ya kutokeza mazao fulani (mazao hayo ni lazima tuyataje, tusiishie kusema tu kwamba ni ‘matarajio ya jamii na taifa…’,

Bali matarajio mahsusi ambayo ni stadi, uwezo na mitazamo tunayotaka wanaofundishwa maarifa na ujuzi fulani wawe nayo). Mtaala ni ‘praxis’, yaani maarifa na ujuzi vionekane katika vitendo na mienendo ya waliopata elimu (yawepo mabadiliko chanya ya kitabia).

Katika nchi nyingi Duniani, wazazi au walezi wa kila mtoto aendaye shule, wana haki ya kujua mitaala ya masomo husika ya shule hizo.

Kwa kuzingatia haki hiyo, vyombo vya elimu huwajibika kumpatia kila mzazi au mlezi nakala ya mtaala inayoonesha wazi sababu za mwanae kupatiwa elimu ya kiwango husika, elimu hiyo itapatikana katika mchakato gani, ni nini kinachotarajiwa kuwa badiliko la mtoto baada ya kupatiwa elimu hiyo na badiliko hilo litapimwa namna gani.

Utaratibu wa namna hiyo huwapatia wazazi na walezi ushiriki wa moja kwa moja katika utekelezaji wa mtaala. Hapa kwetu hayo hatufanyi, si tu kwa sababu hatujawa na uwezo huo, bali hata mtaala wenyewe (kama nilivyokwishaeleza) hatukuwa nao tangu uhuru (hadi mwaka 2012 ambapo nimeelezwa kuwa kuna andiko ambalo hata hivyo halijatolewa kwa umma).

TATIZO KATIKA MIHTASARI

Kwa kuwa mitaala ndiyo inayotaja malengo ya elimu yanayoongoza uandaaji wa mihtasari ya masomo yote, licha ya kwamba mitaala hatuna, Mihtasari iliyopo (ambayo kwa maana hiyo inatokana na mazoea tu ya uwepo wa mfumo wa elimu) hivi sasa haina malengo yanayoeleweka vyema na imekosa viwango vya kitaaluma vinavyokubalika kitaalam.

Mihtasari yote iliyopo, inaonesha kwamba, kama taifa tumeshindwa kutofautisha madhumuni na malengo ya elimu ya Mtanzania. Aidha, Mihtasari hiyo inaonesha kwamba tumeshindwa kutumia vyema lugha rasmi za taifa (Kiswahili na Kiingereza) katika kubainisha malengo hayo.

Kwa mfano :

A. Katika nyaraka za wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi (mihtasari) iliyoandikwa kwa lugha ya kiswahili, malengo ya elimu yapo kumi, wakati iliyoandikwa kwa kiingereza malengo ya elimu yapo tisa.

B. Katika malengo hayo, kuna sentensi za kiingereza zenye kiunganishi ‘and’ mara ‘sita’ na sentensi hizo zimekuwa zikitumiwa hivyo tangu mwaka 1995 zilipoandikwa katika sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo.

C. Malengo ya elimu ya msingi, kwa lugha ya Kiswahili, yapo 18 wakati katika lugha ya kiingereeza yapo 10 tu.

Ni aina gani basi ya elimu tuliyo nayo, kama malengo yake yamebainishwa kwa namna ya ubabaishwaji kiasi hicho ?

 

UDHAIFU KATIKA VITABU VYA KIADA NA ZIADA

Licha ya matatizo ya kimkakati tuliyo nayo katika nyaraka zinazoongoza elimu, kuna udhaifu mkubwa katika utendaji kiuwezo na kimaadili.

Naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, kitengo kilichopo chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, kinachotoa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada - Educational Materials Approval Committee (EMAC), kimeshindwa kutekeleza wajibu wake kama ipasavyo.

Kitengo hiki kimesababisha mafuriko ya vitabu vinayopotosha dhana ya elimu kwa taifa letu.

Kwa mfano, sio tu kwamba vitabu vingi vya kiada vilivyopewa ithibati na EMAC vina makosa mengi ya kitaaluma, bali hata mfumo wa uandaaji na usambazaji wa vitabu hivyo una harufu ya rushwa.

Ninapenda kutoa mfano kuhusu hayo niliyoeleza hapo juu.

Mnamo mwaka 2009 kupitia mpango uitwao ‘Teaching and Learning Materials Programme (TLMP)’ Taifa letu lilipata msaada wa dola za kimarekani 13,000,000.00) ambazo ni takribani shilingi 20,400,000,000 kutoka shirika la United States Agency for International Development (USAID).

Kwa ajili ya kuandika na kuchapisha vitabu na kugharamia vifaa vya kufundishia masomo ya hisabati, Fizikia, Kemia na Biolojia kwa idadi ya vitabu isiyopungua 2,250,000.

Makosa lukuki yaliyomo katika vitabu vilivyochapishwa kutokana na mradi huo yanatisha na kusikitisha, hasa ikizingatiwa kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilipata uwezeshwaji wa jopo la wataalamu kutoka South Carolina State University.

Mathalani, katika vitabu vya ‘Mathematics for Secondary Schools, Volume I, II, III and IV’ vilivyoratibiwa na EMAC; kama inavyoonekana kwenye utangulizi wake, mwandishi mkuu ndiye huyo huyo mhariri mkuu na mhakiki mkuu. Taaluma na maadili ya uandishi wa vitabu, inazuia mtu kuandaa, kuhariri na kuhakiki andiko lake mwenyewe.

Wataalamu walioshiriki kuandaa vitabu hivyo walikuwa na majukumu mengi ikiwamo kuandika, kuhariri na kuhakiki vitabu walivyoandaa wenyewe chini ya uratibu wa EMAC.

Utaratibu huu kengeufu ulitumika pia kwa wataalamu wa masomo mengine yote yaliyoandaliwa wakati huo chini ya uratibu wa EMAC. Dosari hii haikubaliki popote Duniani, ajabu ni kwamba vitabu hivyo takribani vyote tayari EMAC ilivipatia vyeti vya ithibati.

Harufu ya rushwa iliyoghubika jambo hili, imejikita katika mambo matatu :

Mgongano wa kimaslahi. Mgongano huu unajitokeza moja kwa moja kwa watendaji wa EMAC kushiriki kuratibu na kuandika vitabu ambavyo baadae wao wenyewe walivipatia ithibati, utayarishwaji wa andiko (Typesetting) ya vitabu husika kufanyikia nchini Malaysia na upigaji chapa kufanyikia nchini Kenya. Kazi hizi zingeweza kufanyika hapa nchini kwa maslahi ya taifa letu.

iii. Hakuna uwiano mzuri wa waandishi wa vitabu hivyo baina ya watanzania na wageni kutoka nje. Hata hivyo machapisho ya vitabu hivyo yanadhihirisha mapungufu makubwa ya kitaaluma, lugha na muktadha wa elimu inayotakiwa kwa mtanzania wa sasa. Hili ni jambo ambalo linapotosha wanafunzi na kuwafanya wasielewe mada au maudhui yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha isiyo rasmi ya kiingereza katika vitabu hivyo.

Hii ni mifano michache tu inayothibitisha udhaifu mkubwa ulioighubika sekta ya elimu hapa nchini.

HOJA

Baada ya maelezo hayo ya awali, naomba kwa moyo mkunjufu niwasilishe hoja yenyewe kwa mujibu wa kanuni ya 54(1) na ya 56(1) ya Kanuni za Bunge 2007 za lako tukufu.Kwa kuwakuzorota kwa elimu Tanzania kumesababishwa na mambo yafuatayo:

Mosi, udhaifu wa mfumo rasmi wa elimu unaotokana na sera, mitaala na mihtasari ya elimu;

Pili, kupitwa na wakati kwa Sera ya Elimu ya Taifa na sera nyinginezo, mitaala ya Elimu ya shule za Msingi na Sekondari na mihtasari ya Masomo na vitabu vitumikavyo katika shule za Msingi na Sekondari;

Tatu, kukosekana kwa mitaala rasmi ya kitaifa ya Elimu ya msingi na sekondari;

Nne, Mihtasari iliyopo ni ya mazoea tu ya uwepo wa mfumo wa elimu na haina malengo yanayoeleweka vyema; na hivyo kukosa viwango vya kitaaluma vinavyokubalika kitaalam na kupelekea taifa kushindwa kutumia vyema lugha rasmi za kitaifa za Kiswahili na Kiingereza katika kubainisha malengo hayo; na

Tano, udhaifu katika vitabu vya kiada na ziada ambao umetokana na udhaifu mkubwa katika utendaji; kiuwezo na kukiuka maadili kwa kuidhinisha vitabu vyenye makosa kutumika mashuleni na hivyo kuleta hisia kuwa uidhinishaji huo una harufu ya rushwa.

Kwa kuwa , matokeo ya udhaifu na matatizo ya sera za elimu, mitaala, mihtasari na vitabu vya kiada na ziada ni:-

Tabia ya watanzania wengi kutothamini matumizi ya muda, kupotoka kwa mila, desturi na utamaduni wa jamii ya watanzania, kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma na kada nyinginezo

Kuporomoka kwa uwajibikaji, kuporomoka kwa kiwango cha utii wa sheria na kanuni mbalimbali, kutokuthamini rasilimali za taifa, kukuthiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu , kukua kwa utamaduni wa ukupe, kupungua kwa uzalendo kwa baadhi ya wananchi

Kutojiamini kwa watanzania wanaohitimu elimu katika ngazi mbalimbali na kukua na kukomaa kwa migogoro ya mara kwa mara katika sekta ya elimu.

Kwa kuwa, kuporomoka kwa kiwango cha elimu kumechangiwa na kiasi kikubwa na kitengo kilichopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kinachotoa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada – Educational Materials Approval Committee (EMAC) kimeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kusababisha mafuriko ya vitabu vinavyopotosha Elimu ya taifa letu.

Kwa mfano, vitabu vingi vya kiada vilivyopewa ithibati na EMAC vina makosa mengi ya Kitaaluma na mfumo wa uandaaji na usambazaji wa vitabu hivyo una harufu ya rushwa.

Kwa kuwa, mnamo mwaka 2009 kupitia mpango uitwao ‘Teaching and Learning Materials Programme(TLMP)’ Taifa letu lilipata msaada wa dola za kimarekani milioni 13 ambazo ni takribani shilingi za kitanzania 20,400,000,000 kutoka shirika la United States Agency for International Development ( USAID), kwa ajili ya kuandika na kuchapisha vitabu na kugharamia vifaa vya kufundishia masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na Biolojia kwa idadi isiyopungua 2,250,000.

Pamoja na wizara kupata uwezeshwaji wa jopo la wataalamu kutoka South Carolina State University mathalani katika vitabu vya ‘Mathematics for Secondary Schools, Volume I, II, III and IV’, vitabu hivyo vina mapungufu mengi,

Kwa kuwa utungaji wa vitabu haukufuata kanuni za kiuandishi, kwani mwandishi mkuu ndiye huyo huyo mhariri mkuu na mhakiki mkuu.

Kwa kuwa, kitaalamu na kimaadili mtu haruhusiwi kuandaa, kuhariri na kuhakiki andiko lake mwenyewe, utaratibu huu kengeufu ulitumika pia kwa wataalamu wa masomo mengine yote yaliyoandaliwa wakati huo chini ya uratibu wa EMAC.

Dosari hii haikubaliki Duniani hasa ukizingatia kwamba vitabu hivyo takribani vyote tayari EMAC ilivipatia vyeti vya ithibati.

Kwa kuwa, udhaifu wa EMAC umesababisha madhara yatuatayo:

i. Mgongano wa kimaslahi. Mgongano huu unajitokeza moja kwa moja kwa watendaji wa EMAC kushiriki kuratibu na kuandika vitabu ambavyo baadae wao wenyewe walivipatia ithibati.

ii. Utayarishwaji wa andiko (Typesetting) ya vitabu husika kufanyikia nchini Malaysia na upigaji chapa kufanyikia nchini Kenya. Kazi hizi zingeweza kufanyika hapa nchini kwa maslahi ya taifa letu.

iii. Kukosa uwiano wa waandishi wa vitabu hivyo baina ya watanzania na wageni kutoka nje. Hata hivyo machapisho ya vitabu hivyo yanadhihirisha mapungufu makubwa ya kitaaluma, lugha na muktadha wa elimu inayotakiwa kwa mtanzania wa sasa.

Hili ni jambo ambalo linapotosha wanafunzi na kuwafanya wasielewe mada au maudhui yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha isiyo rasmi ya kiingereza kwenye vitabu hivyo.

Kwa kuwa, elimu iliyopangwa kwa sera bora na mitaala bora pekee, yenye mihitasari na vitabu vilivyotayarishwa kwa umakini mkubwa na uadilifu, ndiyo yenye uwezo wa kujenga Taifa la watu waadilifu, wazalendo, wachapakazi, watambuzi wa haki na wajibu wao katika jamii.

Na kwa kuwaeimu ndio mapigo ya moyo ya Taifa letu. Mapigo ya moyo yakienda kinyume na asilia yake, uhai huweza kupotea! Tunao wajibu wa kuokoa uhai huo.

Hivyo basi kwa mujibu wa Kanuni ya 117(1) na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ninaliomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza kina cha udhaifu huo wa kimfumo katika sekta ya elimu hapa nchini na kupendekeza hatua za kuchukua ili taifa liondokane na aibu ya udhaifu huo hatarishi katika mfumo wa elimu hapa Tanzania.

James Mbatia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais. Aliwahi kuwa Mbunge wa Vunjo kwa kipindi cha 1995-2000.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI