Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Biashara ya watoto hawa ni Utumwa halisi!

3rd February 2013
Print

Hali ngumu ya maisha na ukali wa gharama za kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku vinaweza kuwa ni vigezo vilivyoanza kushamiri kwa biashara iliyoibuka kwa kasi hivi karibuni ya kuwauza wasichana wadogo kwenda nchi za nje kutumika katika kazi mbalimbali.

Kwanza tujikumbushe kidogo historia ya biashara ya utumwa katika karne ya 16, wakati wananchi wengi walisombwa kutoka mikoa mbalimbali nchini na walipelekwa Zanzibar na Bagamoyo na kuuzwa kwa Waarabu kabla ya kusafirishwa kwenda nchi za Uarabuni, wengine Marekani, na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya.

Wakati wa enzi ya biashara ya Utumwa, viongozi wa jadi walitumiwa kwa kurubuniwa na vitu kama shanga, visu, nguo nk na wao wakawalipa kwa gharama ya kuwakamata mababu na bibi zetu na kuwaandalia misafara ya kwenda Bagamoyo, Zanzibar kulikokuwa na maeneo maalumu ya soko la kuwauza babu na bibi zetu ili wakatumike kama watumwa katika nchi mbalimbali duniani.

Inawezekana kabisa viongozi wa enzi hizo walitawaliwa na masuala magumu yaliyowahusu wao na mazingira ya wakati huo, na hayo yakawashawishi kuona urahisi wa kuwauza wananchi wao kwa thamani ya shanga za kuvaa, matokeo yake heshima ya Mwafrika ikashuka na tukaonekana ni watu wa kutawaliwa na kufanyishwa kazi za nguvu kwa ujira kidogo na wakati mwingine bila hata malipo.

Na ndio maana hata leo hakuna anayedai kwa uhakika kama Marekani ni nchi ya taifa la watu gani, kama ni ya wazungu, waasia, waafrika au wahindi! Huko kuna mchanganyiko wa kila taifa, na sehemu kubwa ya wakazi wazawa wa Marekani ni wenye asili ya U-afrika, na asili ya hao Waafrika namna walivyofika Marekani ni historia inayofanana na utumwa.

Wengi wa Waafrika walibebwa kutokea Afrika Magharibi na kupelekwa Marekani na nchi nyingine kama watumwa kwa ajili ya kulima katika mashamba ya miwa, mahindi nk. Nia yangu siyo kuelezea historia ya utumwa, kilichonisukuma zaidi ni namna hali ya utumwa-mamboleo unavyojipenyeza kwa mbinu tofauti ya kuwauza watoto kutoka baadhi ya mikoa iliyotajwa hapa nchini.

Imeandikwa kuwa "Serikai wilayani Temeke itafanya uchunguzi ili kuwabaini baadhi ya wenyeviti na serikali za mitaa wanaoshirikiana na mawakala wanaosafirisha watoto kwenda nje ya nchi kutumikishwa", gazeti moja limetoa habari hiyo mbaya. Mkuu wa wilaya Temeke, Sophia Mjema alipotakiwa kuthibitisha hayo, alisema hawezi kukataa kama wapo baadhi ya wenyeviti wanaofanya hivyo, lakini alisema ili kupata uhakika wa jambo hilo, serikali itafanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

Uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kuwa watoto wanaonunuliwa na mawakala maalumu kutoka mikoani wakifikishwa Dar es Salaam kabla hawajavushwa kwenda Zanzibar, mawakala hao huwatafutia barua kutoka kwa wenyeviti hao ili wasisumbuliwe bandarini kwa kuwa wakati huo wanakuwa hawana vitambulisho.

Imebainika kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa na mawakala kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchi za Uarabuni kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za ndani ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora, Ruvuma, Tanga na Shinyanga.

Watoto wakifikishwa Zanzibar inadaiwa wako watu maalum ambao huwapokea na kuwafanyia mipango ya usafiri wa ama ndege au meli kwenda nchi za Uarabuni! Sina uhakika kama msukumo wa kuwauza watoto unatokana na mchakato wa wazazi hao kujiongezea kipato, au labda ni moja ya njia za kuwatafutia ajira vijana hao wadogo, lakini kwa vyovyote vile huo ni ukiukwaji wa haki za msingi za mtoto.

Wazazi wanaowauza watoto kwa hakika hawatofautiani na baadhi ya wazazi wa kabila la wafugaji ambao huko nyuma walikuwa wakiwazuia mabinti zao wasiende shule bali waolewe ili kuongeza idadi ya mifugo katika familia.

Nimeelezea kidogo utaratibu unaofanywa wa kuwapata hao watoto kwenda Uarabuni, utaratibu ambao unafanana sana na ule wa karne ya enzi za utumwa, ingawa kwa hakika miaka hiyo maeneo mengi ya Afrika hapakuwepo na serikali ya kuingilia kati. Upo msemo wa vijana wa mitaani unaodai kuwa katika kipindi hiki cha Sayansii na Teknolojia, kila kitu ni biashara, machupa ya maji yaliyotumika...biashara...vyuma vichakavu...biashara...magazeti yaliyosomwa...biashara, lakini sasa hali imevuka mpaka wanapotaka kuhalalisha kuwa hata watoto...biashara!

Ni wajibu wa serikali kuanzia za mitaa na vitongoji kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao bila kupindishwa! Inapofikia wazazi kuona watoto kama kitegauchumi kwa maslahi yao hilo ni kosa kubwa.

Inatakiwa wazazi wenyewe watambue wajibu wao kwa watoto, si jambo jema karne ya leo ikaturejesha kukumbuka namna machungu waliyopitia babu zetu, na kama unataka kuona mfano halisi nenda Zanzibar ukazuru maeneo yaliyotumika kama soko la watumwa!

Hawa watoto wanaopelekwa huko Uarabuni kinyemela kufanya kazi, lazima ieleweke bayana kama ni kazi gani ambazo zinawapa kipaumbele watoto wa kike zaidi kuliko wanaume. Isitoshe ni kwa nini hao Waarabu pamoja na mawakala wao wasiamue kufuata taratibu za kisheria za kuwapata hao watumishi wanaowataka?

Nina imani kuwa serikali itaweka utaratibu mzuri wa kuwabana wote wanaojihusisha na biashara hii mbovu ili dhamira ya serikali ya kulinda haki za kila raia, ikiwa ni pamoja na kuzuia biashara ya watoto nchini isiendelee. Wale wazazi waliojihusisha na kuwauza watoto sheria ichukue nafasi yake na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Maoni: 0715-047304 na 0762-233116   

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI