Mkunga Agripina Sikanyika (kulia) akimkabidhi mtoto mama aliyejifungulia chumbani kwake.
Umbali wa kufikia vituo vya afya, ukosefu wa barabara ,kuvuka mito iliyojaa maji majira ya masika ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakazi wa kata ya Bukundi, wilayani Meatu, Simiyu.Makala haya yaeleza
.
Wakunga wa jadi wamekuwa nguzo muhimu wananchi walioko pembezoni, ambako hakuna zahanati, vituo vya afya wala dawa za kutosha.
Gidahalija Gamariri, 60, mfugaji wa jamii ya Wataturu ana wake watano na watoto 20. Hata hivyo, hawajawahi kupata huduma katika kituo cha afya au zahanati.Hivi karibuni, mke wake mdogo amejifungulia nyumbani mtoto mchanga.
Mfugaji huyo ni mkazi wa kitongoji cha Gasara,kijiji cha Lukale, kata ya Bukundi, wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.Ana ng’ombe 3,000.
Anasema kituo cha afya kipo umbali wa takriban kilometa zaidi ya 50 kutoka eneo analoishi ni sababu nyingine inayowalazimisha wake zake kujifungulia nyumbani kwa msaada wa wakunga jadi ambao ni tegemeo lao kubwa.
Tangu alipobahatika kuoa mke wa kwanza miaka mingi iliyopita wakati, Mwalimu Julius Nyerere akiwa rais wa Tanzania kwenye miaka ya 70 hadi sasa,mfugaji huyo ambaye hajui kusoma wala kuandika ana idadi kubwa ya wake na watoto ambao hawajawahi kupata huduma ya hospitali.
Anasema karibu asilimia 99.9 ya jamii hiyo, wanatumia huduma ya wakunga wa jadi (Amatawasi) wanaotumia tiba za asili ili kumsaidia mama anayejifungua na mtoto mchanga.
Wakunga wanaotegemewa ni wazee wanaoaminika kuwa wana ujuzi mkubwa walioupata kutokana na malezi na urithi toka katika familia zao.
Dawa zao za mitishamba na nyinginezo zimekuwa msaada mkubwa kwao.
"Amatawasi ni akina mama wenye umri mkubwa,pengine si chini ya miaka 50 na kuendelea.Tunawaheshimu sana kwa jinsi wanavyoisadia jamii.
Huku hakuna barabara za kuaminika wala hosoitali,” anasema Mke wake wa kwanza ana watoto sita, wa pili watoto watano, wa tatu watoto wanne, wa nne anayekumbuka kumuoa wakati rais Benjamin Mkapa akiwa anaingia madarakani naye ana watoto wane.
Na mke wake wa tano amejaliwa mtoto mmoja aliyezaliwa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wakati rais Jakaya Kikwete akigombea urais mwaka 2010. Anafurahi kwamba watoto wake wote 20 wapo hai na wana afya njema.
Gamariri anasema, kwa sasa hana mpango wa kuongeza mke mwingine licha ya kuwa na nguvu na uwezo wa kumtunza.
Mfugaji huyo hajui matatizo gani wanayokumbana nayo wake zake wakati wa kujifungua kwa sababu wanaume hawaruhusiwi kuwepo katika eneo wanalojifungulia au kuwa karibu ya nyumba au shughuli hiyo inapofanyika.
Anakiri kuwa, angefurahi na kufarijika siku moja, kama angebahatika kumpeleka mkewe katika kituo cha afya, kupata huduma ya afya, lakini anasikitika kwamba huduma hiyo iko mbali sana.
"Sasa hata kama uwezo upo lakini hakuna barabara, gari hakuna nitafanya nini au sisi tutafanya nini katika maeneo yetu
huku? Nitampelekaje mke wangu huko nikiwaacha Amawatasi," anasema.
Inaposhindikana mama anapojifungua na kuwa katika hali mbaya anasema kuwa hupiga yowe kuomba msaada, wa kumbeba mgonjwa mabegani kwa kutumia machela ya kutengeneza machela.
Yowe hilo huashiria kwa watu kuwa kuna tatizo kubwa au dharura kubwa inayohitaji msaada wa watu wengi tena kwa haraka.
Wakati huo anasema kuwa, wazee wa jinsi zote wake kwa waume, hulazimika kuomba mizimu iwaondolee balaa hilo.
Changamoto nyingine wanayokabiliana nayo wanapombeba mgonjwa kwenda hospitali ni miundo mbinu mibovu ya barabara mito hujaa maji na kusababisha hali kuwa ngumu ya kumuwahisha mgonjwa akapate huduma, hasa kipindi cha msimu wa mvua.
Hulazimika kutua machela chini na kusubiri maji yapugue ndio wavuke.
"Hali hiyo inapojitokeza wengi wetu, huanza kukata tamaa, kwani ukimwona mgonjwa unamwachia Mungu. Ni huzuni na mara nyingi wajawazito wengi hupoteza maisha yao katika mazingira kama hayo.
Ikitokea akafariki, hulazimika kubeba mwili wa marehemu na kuurudisha nyumbani kwa ajili ya msiba na mazishi,” anafafanua.
Anasema magari katika eneo lao mara nyingi wanayaona wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuombwa kura na baada ya hapo kila mmoja anaishi anavyojua
Pamoja na hali hiyo anasema wamezoea, kwa kile anachoamini kuwa Mungu na mizimu yao inawasikia na kuwajali,hasa wanapokua katika kipindi kigumu cha wake zao
kujifungua.
Hujifungua salama kwa msaada wa wakunga wao ‘Amatawasi’ Utaratibu wa familia hizo, mke anapojifungua salama mkuu wa kaya huamuru kuchinjwa kwa mtamba mkubwa au dume la ng'ombe kama heshima kwa mama huyo huku mkunga wake na wasaidizi wake,wanaendelea kumhudumia, ikiwa ni pamoja na kumpaka mafuta ya ng'ombe kwenye tumbo la mama huyo.
Mafuta hayo ni mbadala ya dawa za kupunguza maumivu au maji ya moto yaliyozoeleka kumkanda mjamzito. Pia mama huyo hupewa supu ya moto kwa wingi.
Kuhusu familia zisizo na uwezo, anasema kuwa jirani huchangia bila ya masharti kama ishara ya upendo na shukrani kwa mizimu yao.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Tabibu wa daraja la kwanza, James Lushinge, aliyewahi kufanya kazi
katika kituo cha afya cha Bukundi, kilichopo umbali wa kilometa zaidi ya 50 toka eneo hilo. Alifanya kazi hapo kwa muda wa miaka saba.
Anasema, wananchi walioko pembezoni, wanakabiliwa na changamoto nyingi za kupata huduma za afya ikiwa pamoja na wataalamu wanaofanya kazi katika maeneo hayo kukabiliwa na changamoto nyingi.
Zikiwemo za kuwahudumia wananchi hao, hasa akina mama wajawazito na watoto wanaofikishwa kituoni wakiwa na hali mbaya kutokana na kuchelewa kupata huduma yeyote hata ile ya kwanza katika zahanati.
Wanapofika wakati mwingine hawakuti dawa au vitendea kazi hakuna na kama vipo ni duni.
"Wakati mwingine mama mjamzito anahitaji damu baada ya kuvuja damu nyingi anapopelekwa hospitalini, tena kwa machela.
Anapofika kituoni hakuti damu, na hata kama ndugu na jamaa wako tayari kutoa damu,lakini hakuna vifaa na pengine hata vile vya kupimia kundi la damu ya anayemtolea damu. Inakuwa ngumu, na unajikuta mama anakufa hivihivi ukiwa huna msaada wa kuokoa maisha yake,” anasema kwa masikitiko.
Hata inapotokea unatoa rufaa kwa mgonjwa huyo kupelekwa hospitali ya wilaya, changamoto kubwa ni gari la kumuwahisha mgonjwa . Wakati mwingine gari linakuwepo lakini halina mafuta, au bovu.Wakati ndugu na jamaa wanajipanga kutafuta huduma mgonjwa anaendelea kuteseka, na hata wanapofanikiwa wakati mwingine humkuta mama amekata roho, anasema Lushinge.
"Ndugu yangu, hata kama angekuja mama, dada, shangazi shemeji yangu angefia mikononi.Ninasema hivyo kwa sababu wananchi walioko pembezoni wamesahaulika na hata vituo vya afya na zahanati kadhalika vimesahaulika,” anasema Lushinge.
Lushinge kwa sasa anafanya kazi katika hospitali ya wilaya ya Meatu, anasema tatizo kubwa ni vitendea kazi vinakwamisha hata kama watu wenye ujuzi wapo.
Lushinge anasema wamekuwa wakiuliza ngazi za juu,lakini wamekuwa wakiambiwa kuwa tatizo la vifaa ni la MSD.
Diwani wa kata ya Bukundi, Joseph Masibuka anasema,kata yake ina vijiji vya Bukudi, Lukale,Mwabagimu na
Witamiya anasema ipo pembezoni na imesahaulika, takribani katika kila sekta ya huduma muhimu ya kijamii ikiwemo afya.
Anasema eneo hilo linapakana na Ziwa Eyasi, Hifadhi ya
Ngorongoro na lina mito mingi ambayo wakati wa masika hujaa maji na haipitiki kiurahisi. Watu wengi wakiwemo wagonjwa na wanafunzi hushindwa kupata huduma kwa sababu mito hiyo mara kadhaa husomba watu.
Anasema mito hiyo ya Ndushi na Mwangadule ina tabia
ya kuhama hama na mto mwingine wa Sangaichima yote huingiza maji katika mto mkubwa wa Sibiti unaogawa mikoa ya Simiyu na Singida. Humwaga maji katika ZiwaEyasi.
Diwani huyo anasema, eneo hilo halina barabara ya kueleweka zaidi ya njia za mifugo maarufu kama (mapanda ya ng'ombe), yanayotumiwa na magari wakati wa kiangazi ambayo wakati mwingine hupotea njia, kwa sababu hayana alama za barabarani, madaraja au makalavati.
Mkuu wa wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Meatu,Isaya
Moses wote wanaunga mkono kuwepo kwa hali mbaya ya miundo mbinu katika eneo hilo na kutaka ziwepo juhudi za makusudi kuondoa hali hiyo.
Rosemary anasema usafiri wa kumsafirisha mgonjwa hasa wajawazito hufanywa na watu kwa kutumia machele au ngozi maarufu kama (mshuta) ambayo mgonjwa hulazwa na kubebwa kue;ekwa kwenye huduma.
Dkt John Sanyiwa ni Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Meatu, anakiri kuwepo na changamoto lukuki hasa katika maeneo ya pembezoni.
Wilaya hiyo ina zahanati 38 za serikali na zahanati tatu za watu binafsi, vituo vya afya viwili.Pia kuna changamoto nyingi zikiwemo za watoa huduma na watumishi wa afya hasa wahudumiaji wajawazito vijijini.
Anasema, watumishi wapya wanaopangiwa kazi kufanya kazi wilaya ya Meatu,wengi wao hawaripoti, na kuwa katika kipindi cha julai hadi Desemba 2012, watumishi 61 walipangiwa kazi wilayani humo, lakini walioripoti ni 45 tu.
Dkt, Sanyiwa anasema, kuna upungufu mkubwa wa utoaji wa huduma wa afya, ikiwemo ya wajawazito hasa maeneo ya pembezoni vijijini kwa asilimia 56, na kutopatikana kwa baadhi ya dawa na vifaa tiba katika Bohari ya Kanda ya Dawa (MSD),na kuchelewa kupeletwa kwa dawa katika zahanati na vituo vya afya, licha ya kuwepo mgao mdogo.
Tatizo jingine alisema ,kuna mapungufu hata katika majengo ya kutolea huduma za afya, na kusababaisha ufanisi wa kazi
kupungua wakati wa utoaji wa huduma, ikiwemo hospitali ya wilaya ambayo ina uwezo wa kuwa na vitanda 108.
Lakini hadi Desemba 2012 ilikuwa na vitanda 60 tu, hali hiyo husabisha msongamano wa wagonjwa waliolazwa wodini.
Mkurugenzi Moses anasema " wakati umefika kwa maeneo kama hayo kupewa kipaumbele muhimu hasa katika bajeti zetu".
Mkuu wa wilaya hiyo Rosemaryi anasema kuwa,pamoja na
kuwepo changamoto nyingi za maendeleo, lakini upo umuhimu wa kuyapa kipaumbele maeneo yaliyoko pembezoni na kuimarisha huduma za jamii.