Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Uwe mwaka wa kuimarisha utawala wa sheria nchini

7th February 2013
Print
Maoni ya Katuni.

Jana ilikuwa ni siku ya sheria nchini maadhimisho ambayo hufanyika kote nchini kwa majaji kutoa hotuba mbalimbali kwenye maeneo yao ya kikanda, lakini kitaifa sherehe zilifanyika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ambazo Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

Mbali na Rais, pia zilihudhuriwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Waziri wa Sheria na Katiba, majaji, mahakimu, mawakili na wanasheria mbalimbali wanaotekeleza wajibu wa kusimamia sekta ya sheria nchini.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika sherehe hizo ambazo huashiria mwanzo wa shughuli za mahakama kwa mwaka mpya baada ya mapumziko ya mwisho wa mwaka, ni utawala wa sheria: Umuhimu wa uimarishaji wake nchini. Hapana shaka utawala wa sheria ni msingi wa uendeshaji wa serikali na mfumo mzima wa maisha katika taifa linalofuata mfumo wa utawala bora.

Miongoni mwa hoja zilizotolewa katika sherehe za jana ni juu ya uhuru wa mahakama katika kutenda kazi zake za kusimamia haki, kuwezeshwa muhimili huo ili utekeleze majukumu yake sawasawa kwa maana ya watumishi kama majaji na mahakimu, suala la fedha za kuendesha kesi na mambo mengine ambayo yatasaidia kesi kusikilizwa kwa muda mfupi kuliko ilivyo sasa kwa watuhumiwa kukaa mahabusu kwa miaka mingi bila kesi zao kusikilizwa.

Kadhalika, pamoja na hoja nyingine nyingi za maana zilizowasilishwa jana, angalizo lilitolewa kwamba ni lazima mahakama zifanye kazi kwa uhuru na haki ili kujiepusha na dhana ambayo imeanza kujengeka miongoni mwa wananchi kwamba mwenye fedha au nafasi kubwa kicheo katika jamii ndiye anapata haki.

Angalizo hili halikutoka bure tu wala halijazuka tu, ila linaakisi hisia na pengine mambo ya kweli ambayo yametokea katika mfumo wetu wa utawala wa sheria. Utawala wa sheria ni dhana pana, utekelezaji wake unahusisha makundi mengi katika jamii.

Ili mtuhumiwa wa kesi ya jinai afikishwe mahakamani anaanzia kwanza polisi, wajibu wa polisi ni kufanya upelelezi na kujenga kesi kabla ya kuanza kwa mchakato wa kushitakiwa.

Kwa maana hiyo, msingi mkuu wa kuhakikisha kuwa haki ndani ya jamii inatendekea ni kwenye uundwaji wa kesi zenyewe. Kwamba kama polisi watakuwa wanabambikizia watu kesi, basi ni dhahiri hata kama watafikishwa mahakamani na kushinda kesi hizo, watakuwa wameathirika na kwa uhakika watajenga hasira au hisia nyingine zozote dhidi ya mfumo mzima wa utoaji wa haki katika nchi yao.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwako na vitendo vingi vya wananchi kujichukulia sheria mkononi, hivi ni pamoja na kuvamia vituo vya polisi, kuvichoma moto, kuua askari na hata mahali pengine kuwakataa askari wanaofika kwenye matukio ya uhalifu. Kwa kifupi kuna tabia ambayo imeanza kuota mizizi ya wananchi kuwakataa polisi kwa kuamini kwamba wao ni kikwazo kimojawapo cha wao kupata haki.

Kwa mfano, zipo kesi nyingi ambazo ziko mahakamani zikiendelea kutajwa kwa miaka na miaka bila upelelezi wa kipolizi kukamilika; zipo kesi ambazo zipo mahakamani ambazo washitakiwa wanashangaa wamefika je mahakamani ilhali hawakuhusika kwa vyovyote na tuhuma wanazobebeshwa.

Ukiweka kando suala la polisi kuanza kuonekana kama kikwazo cha wananchi kupata haki, kwa maana ya kushindwa kufanya kazi za upelelezi sawasawa, kubambikizia watu kesi na mara nyingine kuonekana kuegemea upande wa wenye nguvu za fedha katika kutimiza wajibu wao, kwa maana hiyo kujiondoa kwenye njia ya uwajibikaji wa kiweledi, mahakama nazo zinatazamwa kwa jicho hilo hilo la kutiliwa shaka.

Kwamba ni kweli kuna upungufu wa majaji na mahakimu; kwamba ni kweli bajeti inayotolewa na serikali kwa mahakama ni finyu kuiwezesha kutimiza majukumu yake sawasawa, lakini bado zimeonekana dalili kuwa wenye nguvu za fedha kesi zao hazikawii sana mahakamani; hata kama wanatuhumiwa kwa kesi kubwa kiasi gani.

Tunatambua kwamba kiwango cha uelewa ndani ya jamii ya Kitanzania kinazidi kukua siku hadi siku, watu wanatambua haki zao zaidi pia kuhoji juu ya maamuzi mbalimbali yanayotolewa na wenye mamlaka mbalimbali ambayo yanagusa maisha yao moja kwa moja, kumekuwa na mwamko mkubwa zaidi wa kutaka uwajibikaji zaidi wa watumishi wa umma kwenye ngazi zote, kwa maana hii hatuoni kama mahakama nayo itakwepa darubini ya umma katika kukua kwa uelewa wa wananchi juu ya haki zao.

Ni kwa maana hii basi tungependa kuona mahakama zetu zikizidi kuwa kimbilio la wananchi kupata haki na kwa kweli waone wakizipata haki husika, ni kwa njia hiyo tu jamii itaendelea kujenga imani na mahakama, lakini wakati huo vitendo vya watu kujichukuliwa sheria mkononi vikipungua kwa elimu zaidi kutolewa kwa wananchi na wakati huo huo Jeshi la Polisi nalo likijitazama kwa darubini kali ili liwe chombo cha kulinda maisha na mali za wananchi na si kuwabambika kesi.

SOURCE: NIPASHE