Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Benki ya Stanbic yatajwa kuthaminiwa zaidi Afrika

8th February 2013
Print
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bashir Awale

Ripoti ya mwaka huu ya tathmini ya mabenki 500 bora duniani, imeitaja benki ya Stanbic kuwa benki inayothamaniwa zaidi barani Afrika kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Benki hiyo pia inafanya biashara kama Benki ya Standard.

Ripoti ya benki bora 500 duniani huandaliwa na kufanyiwa tathmini na wataalam wa masuala ya kibenki na fedha na kuchapishwa na gazeti kubwa duniani la masuala ya kibenki la The Banker.

Tuzo ya benki bora 500, ikiwa katika mwaka wake wa nane, ni tuzo ya kipekee inayoshindanisha ubora wa huduma za benki katika sekta ya kibenki duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, benki ya Stanbic kwa sasa ina thamani ya zaidi ya dola bilioni 1.5 za Marekani na kujiimarisha katika nafasi yake ya kuwa benki yenye bidhaa na huduma bora barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bashir Awale, alisema hatua hiyo kubwa inaonyesha dhahiri dhamira ya benki hiyo kufanya shughuli zake za kibenki Afrika kimkakati zaidi na kujenga biashara ya ushirikiano wa hali ya juu barani Afrika.

"Tunajivunia kuwa benki yetu inaendelea kutambuliwa kama benki bora na yenye thamani kubwa Afrika. Kutambuliwa huku kunatokana na sababu nyingi, kubwa ni jitihada za watu wetu na huduma ambazo tunatoa kwa wateja wetu Tanzania na Afrika nzima. Kutambuliwa huku kunadhihirisha thamani iliyopatikana kutokana na kuwapa wateja wetu huduma inayolingana na mahitaji yao katika sekta na nyanja mbalimbali, tukiamini kwamba hii ndiyo hutofautisha benki yetu na mabenki mengine,” alisema Awale.

Aidha, benki ya Stanbic ya Tanzania ambayo ni sehemu ya benki ya Standard, ilikuwa ni benki ya 103 miongoni mwa benki 500 bora duniani.
 

SOURCE: NIPASHE