Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Werrasa: Vikapu vya kufuma vyamjengea nyumba na kuboresha maisha

8th February 2013
Print
Mjasiriamali Werrsa Ndosi anaonyesha vikapu anavyosuka na kuuza kwa wateja

 Mjasiriamali  Werrasa Ndosi,  alianza biashara kwa kuuza maharage kwenye vibakuli kijijini kwao Masame Mbweyela mkoani Kilimanjaro.  Baada ya kufanya majaribio ya biashara mbalimbali na kupata mikopo amefanikiwa kujenga nyumba jijini Dar es Salaam na kuanzisha kampuni yake iitwayo Mbwerania Family Group Kimara jijini Dar es Salaam. Anatengeneza na kuuza vikapu, mabegi, mikanda na bidhaa nyinginezo.  Makala haya yanaeleza.

 
Wakati Werrasa Ndosi,51,  alipoanza kufanya biashara ya kuuza maharage kwa kipimo cha vibakuri katika kijiji vya Masama Mbweyela mkoani Kilimanjaro  baada ya kushindwa   kuendelea na elimu ya  sekondari hakufahamu kuwa ameanza safari  ya kuelekea kwenye mafanikio ya uhakika.
 
Sasa anamiliki nyumba ya vyumba vinne  aliyoijenga katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam, mzunguko wa fedha umeongezeka na kuwawezesha watoto wake wawili,Godwin kuhitimu elimu ya sekondari na kujifunza teknolojia ya kompyuta na Joyce aliyehitimu kidato cha nne  sasa  wanamsaidia  mawasiliano  ya kibiashara na usimamizi wa mambo mengineyo.
 
Werrasa alichukua uamuzi huo wa kufanya biashara baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 1979.  Wazazi wake hawakuwa tayari kuona anaendelea na masomo ya sekondari.
 
“Nilikuwa na akili sana darasani. Nashika  nafasi ya kwanza na ya pili…lakini wazazi wangu  pengine  kwa sababu ya mwamko hawakuwa tayari kuona naendelea na elimu ya sekondari,” anasema Werrasa.
 
Safari hiyo kuelekea kwenye mafanikio ya sasa  haikuwa rahisi hata kidogo. Alifanya biashara ya maharage aliyonunua na kuuza rejareja  katika vibakuri.  Mtaji ulipoongezeka akaanza kununua kwa ujazo wa  madebe na kisha magunia.
 
“Nilikuwa  napakia mizigo yangu na kusafiri kwa malori yanayobeba mafuta toka kijijini na kupeleka  Dar es Salaam. Wakati huo ukibeba mzigo mkubwa tafsiri yake ilikuwa ni mlanguzi. Miaka hiyo, usafirishaji ulikuwa mgumu sana na biashara ngumu lakini nilijitahidi. 
 
Dar es Salaam nikawa nafikia kwa mama yangu mdogo na kuwauzia wenye maduka. Nikilipwa  narudi tena kijijini kubeba mzigo mwingine. Mama mdogo hakupendezewa sana kuona nafanya biashara hiyo lakini alipoona napiga hatua naye akaanza biashara,” anafafanua.
 
Werrasa aliolewa mwaka 1987 na kupata watoto wawili, anasema baada ya kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu akaamua kupanua biashara kwa kununua ng’ombe.
 
“Nilinunua ng’ombe kanisani kwa sh.300,000. Sikuwa na banda la kumtunzia na kumuomba aliyemtoa ng’ombe huyo aendelee kumtunza kwa muda wakati najenga banda. Ajabu ya Mungu usiku wa siku hiyohiyo niliyomnunua alizaa mtoto. Mama yangu, alipoona nimepiga hatua hiyo akaniunga mkono kwa kunipa ng’ombe mwingine. Kuanzia hapo nikawa mfugaji,” anasema.
 
Hata hivyo, alishindwa kuendelea na changamoto ya ufugaji kwa  sababu ya ukosefu wa banda la kutosha kwa ajili ya kufugia, tatizo la upatikanaji wa  majani  na maji kwa ajili ya chakula chao ukamfanya aamue kuachana na mradi huo kwa  kuwauza ng’ombe wake watano.
 
“ Niliamua kujikita katika mradi huu baada ya kuona  akina mama wengi  wanatumia  majani ya aina mbalimbali toka msituni na kutengeneza vitu vyenye thamani  na kuviuza ili kujiongezea kipato  na kupambana na umaskini katika familia zao,” anasema.
 
Baada ya kuuza ng’ombe, mwaka 2009 akaamua  kuanzisha biashara nyingine.  Alijifunza mwenyewe ufumaji vikapu kwa kutumia majani ya miyaa sebuleni kwake na kuvipeleka SIDO kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kama zinafaa kuingia sokoni na kupata mafunzo zaidi.
 
Makao makuu ya SIDO, alikutana na Happines Mchomvu, Janet  Minja na Henrick  Mdede  na kuwafahamisha kuhusu ndoto zake za kuwa na mradi huo.
 
“Waliviangalia vikapu hivyo  na kuvutiwa navyo. Wakaamua kunipeleka   SIDO mkoani.Huko nilipokelewa na Meena  na viongozi wengine  walionipa ushirikiano wa karibu zaidi na fursa ya kuhudhuria mafunzo ya mwezi mmoja bure,”anasema.
 
Baada ya mafunzo hayo, alianza mradi huo akiwa na mtaji wa sh. 750,000   kununulia malighafi  za  utengenezaji wa bidhaa hizo,  kuwalipa mafundi waliokuwa  wakimsaidia  kutengeneza bidhaa  na kukodisha mashine ya kufumia  toka kwa mtu binafsi .Alikuwa akimlipa sh. 15,000 kwa mwezi.
 
Werrasa  baada ya kuona mtaji huo haumuwezeshi kupanua biashara yake, aliomba mkopo SIDO  wa sh.milioni moja  na kufanikiwa kupata. Mkopo huo aliurudisha baada ya mwaka mmoja huku mradi wake ukipanuka taratibu. 
 
Kupanuka kwa mradi wake, kukamfanya aongeze bidhaa anazotengeneza zikiwemo  vikapu, mikanda, viatu vya wazi, mikoba ya akina mama na akina baba na nyinginezo.
 
“Nikawa nafuata malighafi  Mtwara, wilaya ya Tunduru,  katika kijiji cha Ulumesule. Pia nilienda kutafuta malighafi zaidi katika maeneo ya Njombe na Tanga. Huko Njombe nikapata aina nyingine ya vikapu na kuniwezesha kuongeza utaalamu zaidi katika kazi yangu,” anasema
 
Maendeleo ya mradi wake na uaminifu aliouonyesha  kurudisha mkopo kwa wakati ulimfanya akubaliwe kupewa mkopo mwingine wa sh.milioni tano. 
 
"Kupitia mikopo hii, mradi umepanuka. Mzunguko wa fedha umeongezeka. Pia nimeweza kurejesha mikopo,  kutunza familia yangu, kula vizuri tofauti na miaka ya nyuma. 
 
Kugharamia elimu ya watoto,  kujenga nyumba na kufungua duka na sehemu ya kuuzia bidhaa zangu  Mbezi beach na Mabibo sokoni jijini Dar es Salaam." alisema.
 
Anasema, amekuwa akishiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya wajasiarimali  jijini Dar es Salaam na mikoa mingine. Katika maonyesho ya  Jumuia ya Ushirikiano wa  Maendeleo ya Uchumi wa   Kusini mwa Afrika (SADC) mkoani Arusha alibahatika kupata oda ya vikapu anayoamini kuwa ingemuwezesha kumnyenyua kiuchumi lakini bahati mbaya alishindwa kuitimiza kwa sababu ya upungufu wa malighafi .
 
Kutokana na tatizo la upatikanaji wa malighafi ya majani ya miyaa na matete, Wessara ameamua kusuka vikapu na bidhaa zake kwa kutumia malighafi ya mkonge  inayopatikana kwa wingi na kwa uhakika zaidi.
 
Kwa upande wa masoko,  anaendelea kutafuta  masoko ya nje ingawa soko la ndani anafanya biashara na  wateja mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa jumla jijini  Dar es Salaam na mikoa mingine.
 
Mjasiriamali huyo, amepata mkopo mwingine wa sh milioni sita  unaomfanya apanue zaidi  biashara yake
 
Kwa kujiunga na  alama ya kibiashara (barcode) anaamini  inasaidia kuainisha ubora wa bidhaa, kuitambulisha vyema kwa wateja na kuaminika. Mazingira hayo mapya ya kibiashara anaamini kuwa yatasaidia sana kumtambulisha kimataifa na kupata wateja zaidi 
Kupitia mradi huo, ameweza   kutoa mafunzo kwa  watu mbalimbali mkoani  Dar es Salaam na Zanzibar pia ameelimika na kupanuka kimawazo hata kumudu kuzungumza vyema na wateja tofauti na alipoanza.
 
Pia amefanikiwa kukutana na wajasiriamali wengine chini ya mwavuli wa  SIDO, vyombo vya habari, wabunge, na  kutoa mafunzo kwa watanzania wenzangu na  wafanyabiashara wa toka kisiwa cha Mafia  kuhusu usukaji wa vikapu na kushona na kuwafundisha hatua kwa hatua.
Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo, anasema upatikanaji wa malighafi na uhakika wa soko bado ni tatizo.
 
"Kipindi cha nyuma tulikuwa tunapata oda ya vikapu na bidhaa nyingine, lakini tunashindwa kutengeneza kwa muda unaotakiwa  kutokana na ukosefu wa umeme," anasema
Changamoto nyingine ni  ushuru  mkubwa unaotozwa kwenye vikapu vya miyaa  hata kama vikapu ni vidogo kuliko faida inayopatikana.
 
Pia majani ya miyaa yanatozwa  ushuru kubwa katika barabara kutoka Mtwara na Same (Kilimanjaro).
 
Kwa sababu ya mvuto wa  vikapu hivyo,  baadhi ya  wafanyabishara  toka Kenya wanakwenda vijijini kununua vikapu vya miyaa na kudai kuwa wamevitengeneza wao na kuwadanganya wateja.
 
Ushuru unaotozwa kwa kikapu kimoja ni  sh. 700 na Wizara ya Maliasiri na Utalii  na kusababisha baadhi ya  wajasiriamali waliokuwa wanatengeneza na kufanya biashara hiyo kuamua kuachana nayo.
 
SOURCE: NIPASHE