


Uongozi wa Yanga umesema ujenzi wa Uwanja wa Kaunda wa klabu hiyo utaanza Mei mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema taratibu za awali za kufanya tathmini ya ujenzi wa uwanja huo zimekamilika na wanasubiri kampuni ya Beijing Construction ya China ianze ujenzi huo Mei.
Baraka alisema masuala mengine juu ya ujenzi huo ikiwa ni pamoja na fedha za ujenzi huo zitakakopatikana, yataelezwa baadae na Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga.
"Mambo mengine ya ujenzi yataelezwa na Makamu Mwenyekiti (Sanga) na yeye atafafanua ujenzi huo utaendaje na ataeleza fedha za ujenzi huo zitatoka wapi," alisema Kizuguto.
Alisema hafahamu kama uongozi utachukua mkopo kwa ajili ya ujenzi huo ama la na kusisitiza kuwa Makamu Mwenyekiti, Sanga ambaye yupo nje ya mkoa wa Dar es Salaam atafafanua katikati ya wiki.
Yanga imeingia mkataba na kampuni hiyo ya Beijing Construction ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa, kwa ajili ya kufanya tathmini pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kaunda utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.
Kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutafanya idadi ya timu zinazomilika viwanja vyake kuwa tatu pamoja na Mtibwa, lakini Yanga na Azam zikiwa na viwanja vya kisasa.
Azam imejenga uwanja wake Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kuanza kwa ujenzi wa Uwanja wa Kaunda kutahitimisha danadana za muda mrefu za ujenzi wa uwanja huo kutokana na ahadi za awamu mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo kongwe zaidi nchini.
Kwa kutokuwa na uwanja wake, Yanga imekuwa ikilazimika kucheza kwenye Uwanja wa Taifa mechi zake za nyumbani ambako makato ni makubwa.
Pambano moja linalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa hutozwa asilimia 15 ya mapato yote kama gharama za kufanyika kwa mchezo huo hapo.