Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya TFDA, Gaudensia Simwanza
Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), imekanusha taarifa za uvumi za kuwapo na kuzagaa kwa dawa bandia, za kutibu ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) katika Jiji la Dar es Salaam.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza, amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote kwani TFDA ina utaratibu wa kufuatilia dawa katika soko na kwamba dawa za kifua kikuu hutolewa bure katika vituo vya afya.
Alisema kuwa dawa za kifua kikuu zimechukuliwa sampuli Tanzania nzima Novemba na Desemba, 2012, na uchunguzi wa maabara ulikamilika Januari 2013 na hakuna dawa zozote zilizogundulika kuwa ni bandia.
Hivi karibuni Shirika moja la utangazaji la kimataifa, liliripoti kuwa Dar es Salaam ni miongoni mwa miji 19 katika Bara la Afrika ambayo zimetapakaa dawa bandia za kutibu kifua kikuu kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika moja la afya nchini Marekani.