

.jpg)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema kampuni 22 zimejiunga na Mpango wa Kupambana na Malaria kupitia sekta binafsi na sekta ya michezo (Malaria Safe Companies) ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kushirikiana na sekta binafsi kumaliza kabisa ugonjwa huo.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akishiriki mjadala kuhusu juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa malaria uliofanyika kwenye kituo cha mikutano cha Sandton, kilichopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Alisema si jambo rahisi kuiachia Serikali peke yake iendeshe mapambano dhidi ya ugonjwa huo, ndiyo maana Serikali ya Tanzania iliamua kutumia mfumo wa kushirikisha sekta binafsi ili kuongeza chachu katika kampeni hiyo.
“Ugonjwa wa malaria hauna mipaka. Huwezi kusema mbu ataishia Tanzania, Zimbabwe, Malawi au Afrika Kusini tu. Tunapaswa kuungana pamoja, na mimi natamani kuona nchi zetu zikiungana kupambana na ugonjwa huu,” alisema.
Alisema mpango huo ulianza miaka mitatu iliyopita, lakini ulizinduliwa rasmi mwishoni mwa mwaka jana. Alizitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni Bakhresa, Kampuni za Bia za SBL na TBL, SONGAS, NSSF, PPF na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Tanzania ni nchi ya pili kati ya nchi 12 barani Afrika zilizojiunga na Mpango huo.
Alilitaka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kutumia fursa ya mashindano hayo yaliyofikia kilele jana lichukulie mapambano haya kama changamoto ya kuziunganisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika mapambano dhidi ya malaria kwani katika ngazi ya Umoja wa Afrika (AU) suala hilo limekwishapiga hatua.
Mjadala huo uliwashirikisha Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dk. Aaron Motsoaledi na Naibu Waziri wa Afya wa Msumbiji, Dk. Nazira Vali Abdulla ambao walihojiwa na mtangazaji wa habari za michezo wa kituo cha televisheni cha SuperSport, Carol Tshabalala.
Mjadala huo uliandaliwa ili kuzihimiza serikali za nchi za Afrika kuongeza juhudi katika kupambana na malaria ambao unaongoza kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takwimu za mwaka 2011 zinaonyesha kuwa kati ya vifo 655,000 vinavyotokana na malaria kila mwaka, asilimia 91 ya vifo hivyo inatokea barani Afrika. Na asilimia 86 ya vifo hivyo, huwakumba watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.