Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanasheria walumbana mbele ya Shein kuhusu ubakaji Z’bar

11th February 2013
Print
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Taasisi za sheria zimejikuta zikitupiana lawama mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika mkutano wa hadhara wa kuadhimisha Siku ya Sheria Duniani.

Lawama hizo zilianzishwa na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) wakati wa maadhimisho hayo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwavuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Jaji Mkuu wa Zanzibar kutumbukia katika malumbano huku kila kiongozi akielekeza lawama zake kukosoa utendaji wa taasisi nyingine.

Lawama hizo ziligusa utendaji   wa Jeshi la Polisi, Ofisi ya DPP, AG na Mahakama katika kutekeleza majukumu la kesi za unyanyasaji na ubakaji visiwani Zanzibar.

Akizungunza katika mkutano huo  Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisema ukosefu wa mbinu  za kisasa za upelelezi, polisi kutotumia kikamilifu jamii kupata ushahidi wa kesi na ukosefu wa ushirikiano baina ya waendesha mashitaka na polisi ni mambo yanayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji.

Alisema udhaifu mwengine mtindo wa waendesha mashitaka kusubiri kuletewa majalada ya kesi mahakamani  na danadana za shahidi hapatikani pamoja na wananchi kukubali kusuluhisha majumbani makosa ya ubakaji.

Rais wa ZLS, Awadh Ali Said, yeye alizishambulia idara za upelelezi, waendesha mashitaka na idara ya mahakama kuwa zinafanya kazi kwa ulegevu katika kusimamia hatua za kisheria ikiwamo kuchunguza kesi, uendeshaji wa mashitaka na utoaji wa hukumu mahakamani.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema pamoja ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, Zanzibar kwa sasa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wapelelezi mabingwa wa makosa ya jinai.

Alisema kwa upande mwengine, wananchi pia ni kikwazo kwa waendesha mashitaka kwa sababu hawataki kutoa ushahidi. Hata hivyo, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, alisema kwamba vitendo vya unyanyasaji kijinsia ikiwamo ubakaji vimekuwa vikiongezeka visiwani Zanzibar kila mwaka.

Alisema udhaifu wa polisi katika upelelezi na utoaji wa hukumu umekuwa ukichangia kuenea kwa vitendo vya ubakaji na kuathiri maendeleo ya wanawake na watoto Zanzibar.

 

SOURCE: NIPASHE