Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wananchi wawezeshwa kudhibiti ukataji wa mikoko

11th February 2013
Print

Wananchi wa vitongoji vitatu vya Kata ya Magomeni, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wameanza kuwezeshwa kwa lengo la kudhibiti kasi kubwa ya ukataji wa mikoko.

Mikoko imekuwa ikikatwa kwa ajili ya mkaa na kuni na kusafirishwa kwenda Zanzibar, hali inayochangia uharibifu mkubwa  wa mazingira hususani  kuharibu mazalia ya samaki.

Shirika lisilo la kiserikali la Kupambana na  Ukimwi, Umaskini na Uhifadhi wa Mazingira (Faapeco) limeanza kutoa elimu kwa wakazi hao kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Akizungumza juzi wakati wa warsha ya kujenga Uelewa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi na Uhifadhi wa Mazingira kwa wakazi wa vitobgoji hivyo katika Kijiji cha Makurunge, Kata ya Magomeni, Mkurugenzi wa Faapeco, George Tegule, alisema kuwa katika kukabiliana na ukataji wa mikoko kandokando ya bahari, shirika lake litawawezesha wakazi hao kupanda  mikoko ekari 50. “Tunakusudia kupanda mikoko ekari 50 katika Kata ya Magomeni.

Kitongoji cha Mji Mpya ekari 10, kitongoji cha Lazaba eakari 15 na Kitame ekari 25,” alisema Tegule na kuongeza kuwa lengo la Faapeco pia ni kuimua kipato cha jamii katika vitongoji hivyo hususani kuendeleza miradi ya ufugaji nyuki.

Alisema: “Mfano, Kitame wanafanya mradi wa nyuki na tayari wana mizinga 24, lakini wameuanzisha kwa njia za kienyeji na sisi tutawawezesha kwa mafunzo ya ufugaji. Baadaye mradi utawawezesha mizinga 50 kwa vitongoji vyote.”

Lengo la mradi huo wa miaka miwili unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kwa Sh. milioni 56 na Faapeco Sh. milioni 15, ni kuwafanya wakazi hao wapate kazi mbadala ili waaache kukata miti na mikoko.

Cosmas Peter, mkazi wa Lazaba, alisema amefurahishwa na mafunzo hayo na kwamba wako tayari kulinda na kusimamia mazingira.

Shamim Kamuhabwa, Afisa wa Maendeleo ya Jamii Kata ya Magomeni, alisema mikoko ikipandwa kando ya bahari itasaidia upatikanaji wa samani na kwamba ufugaji wa nyuki utaongeza kipato kwa jamii.
 

SOURCE: NIPASHE