Timu ya taifa ya soka (Taifa Stars) iliwapa raha Watanzania kwa mara nyingine tena baada ya kupata ushindi wa goli 1-0 katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika, timu ya taifa ya Cameroon (Indomitable Lions).
Ushindi huo katika mechi iliyochezwa Jumatano katika siku maalum ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ni muendelezo wa kasi nzuri ya Stars katika siku za hivi karibuni.
Iliwahi pia kuibuka na ushindi wa 1-0 katika mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya waliokuwa mabingwa wa Afrika, timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo).
Kilichofuwarahisha wengi wanaoitakia mema Stars ni namna walivyokuwa wakicheza kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho. Walionekana kujiamini huku wakigongeana pasi safi dhidi ya Cameroon iliyoundwa na nyota kadhaa, akiwamo beki wa kushoto wa Tottenham Hotspur ya England, Benoit Essou Akotto.
Tunadhani kwamba ushindi huu wa pili mfululizo Stars si wa kubeza. Ni ushindi ambao mwishowe utaliongezea taifa alama na kukwea zaidi katika viwango vya ubora wa soka duniani vitakavyotolewa mwezi ujao na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Benchi la ufundi la Stars na wachezaji wanastahili pongezi kwa kazi nzuri iliyowapa raha Watanzania dhidi ya timu (Cameroon) iliyodhaniwa kuwa kamwe tusingeweza kuikimbiza mchakamchaka katika muda mwingi wa mechi, kukosa goli jingine baada ya penati yetu kutojaa wavuni na mwishowe kuifunga.
Hata hivyo, tunaona kuna haja ya kuwakumbusha wachezaji kuwa safari yao ya kuelekea kilele cha mafanikio bado ni ndefu sana. Hawapaswi hata kidogo kubweteka kutokana na ushindi wa Jumatano dhidi ya Cameroon na wa Desemba 22 dhidi ya Zambia. Zote hizo zilikuwa ni mechi za kujipima nguvu tu.
Ikumbukwe kuwa lengo kuu la Stars ni kutwaa mataji katika kila michuano au walau kufuzu kwa fainali za michuano mikubwa kama ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na pia Kombe la Dunia.
Kwa kutambua dhamira kuu ya Stars, ndipo tunapoona kuwa wachezaji wa timu hii wanapaswa kujua kuwa bado wana kazi kubwa mbele yao.
Kwa mfano, Stars inakabiliwa na mechi dhidi ya Morocco mwezi ujao na pia nyingine za marudiano dhidi ya Ivory Coast na Gambia katika kundi lao la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazili mwaka 2014.
Wachezaji wa Stars wanapaswa kujiepusha na ulevi mbaya wa sifa tele wanazopata sasa kutokana na ushindi wa mechi za kirafiki. Badala yake, waongeze juhudi zaidi katika mazoezi yao binafsi na kwenye klabu zao ili kudumisha makali yao; na ikibidi wayaongeze maradufu kabla ya kukabiliana na Morocco.
Wadau wote wa soka nchini, hasa viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) wanatekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa timu inaendelea kupata maandalizi mazuri na pia kupewa mechi za kutosha za majaribio kabla ya kuwavaa Morocco na pia kumalizia vyema mechi za kundi lao katika kuwania kufuzu kwa fainali za Brazil 2014.
Baadhi ya kumbukumbu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba Stars, wakati ikiwa chini ya kocha Mbrazili, Marcio Maximo, iliwahi kuwa na mwenendo mzuri na kuonyesha dalili kama za sasa za kocha Mdenmark Kim Poulsen.
Hata hivyo, inakumbukwa kuwa enzi hizo za Maximo, Stars ilishindwa kizembe nyumbani baada ya kukubali kipigo kisichotarajiwa cha bao 1-0 kutoka kwa Msumbiji, licha ya kwamba awali walishawamudu nyumbani kwao Msumbiji kwa kutoka nao sare ya 0-0.
Huo ni mfano mmoja tu wa namna Stars inavyoweza kuonyesha kiwango cha juu wakati fulani na ‘kuchemsha’ vibaya wakati wanapoaminiwa na kutarajiwa kupata matokeo bora zaidi.
Kama tumeshindwa tangu mwaka 1980 kufuzu kwa fainali walau za Afcon, sasa tuna kila sababu ya kuendelea kuongeza nguvu katika kuimarisha kikosi cha sasa cha Stars ili kurejea mafanikio yetu ya miaka 30 iliyopita na ikibidi, tutimize ndoto isiyotarajiwa na wengi kwa sasa ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia. Tunaweza!