Meneja Matawi Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya Afrika Tanzania, Nelson Mgonja (katikati), akisisitiza jambo wakati wa shindano la droo ya tatu ya `Weka na Ushinde' inayoendeshwa na benki hiyo iliyochezwa katika tawi la benki hiyo la Msimbazi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wengine ni Mkuu wa tawi hilo, Claudia Samaka (kushoto) na Mkaguzi toka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Bakari Maggid (kulia).
Washindi wa shindano la droo ya tatu ya `Weka na Ushinde' inayoendeshwa na Benki ya Afrika Tanzania kwa wateja wake, wamepatikana na kujinyakulia zawadi mbalimbali.
Washindi hao 10 ni kati ya washiriki 306 walioingia katika droo hiyo.
Meneja Matawi Kanda ya Dar es Salaam wa benki hiyo, Nelson Mgonja, alichezesha droo hiyo katika tawi la Msimbazi la benki hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na washindi hao walitangazwa.
“Washiriki wengi wenye vigezo waliingia katika shindano la droo hii lakini kumi ndiyo waliokuwa na sifa za kushinda,” alisema na kuongeza kuwa washindi hao ni wa aina mbili yaani wateja wa rejereja na kampuni za wajasiriamali.
“Washindi wa rejareja wa benki ili ashinde walitakiwa kuwa na salio kwenye akaunti si chini ya Shilingi milioni moja na katika mwezi mmoja awe ameweka Shilingi milioni tatu,” alisema.
Aliongeza kuwa mteja wa kampuni ya wajasiriamali (SMEs), alitakiwa awe na salio si chini ya Sh. milioni 50 katika akaunti yake na kuweka Sh. milioni 100 katika mwezi mmoja.
Alisema washindi wote watapigiwa simu katika matawi ya benki zao kwa ajili ya kupatiwa zawadi zao.
Msimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Bakari Maggid, alisema shindano la droo hiyo liliendeshwa vizuri na washindi walipatikana kihalali.
Naye mmoja wa washindi aliyejinyakulia zawadi ya I- Phone 4S, Gharib Khamis, alisema amefurahi kuibuka mshindi katika droo ya tatu na kujipatia zawadi hiyo.
Droo hiyo itafikia ukingoni wiki ya kwanza ya Machi, mwaka huu na mshindi wa jumla atapatikana akiwa amejishindia samani za nyumbani zenye thamani ya Sh. milioni 10 au kwenda kati ya nchi ya China ama Dubai.