Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Azam yaishika Yanga

11th February 2013
Print
Timu ya Azam FC.

Azam jana iliifikia Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuisambaratisha Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa magoli 4-1 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Ushindi huo unamaanisha kwamba Azam sasa ina pointi 33, sawa na vinara Yanga ambao hata hivyo wanaendelea kukaa kileleni kwa tofauti nzuri ya magoli. Yanga imefunga magoli 29 na imefungwa 12 wakati Azam imefunga mabao 27 na imefungwa 14. Mabingwa Simba ambao waling'ang'aniwa katika sare ya 1-1 dhidi ya JKT Oljoro jijini Arusha juzi, ni wa tatu wakiwa na pointi 28.

Yanga watacheza mechi yao ya mkononi keshokutwa Jumatano dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche alifunga mara mbili katika dakika mbili za mwisho na kufikisha mabao 10 na kuongoza chati ya wafungaji wa ligi hiyo huku Mkenya Joakins Atudo na Mganda Brian Umony wakikamilisha kipigo hicho kikubwa.

Wageni Azam walitangulia kupata goli kupitia Atudo aliyeunganisha krosi iliyopigwa na Abdi Kassim 'Babi' katika dakika ya 14.

Hata hivyo, dakika saba baadaye wenyeji walisawazisha goli hilo kupitia kwa Vincent Barnabas aliyefunga kwa kichwa akiwazidi ujanja David Mwantika na Joakins walioshindwa kumdhibiti.

Azam walirejea kipindi cha pili wakiwa wakali zaidi na walihitaji dakika moja tu kupata goli la pili lililofungwa na Umony aliyemalizia vyema pasi fupi ya Humphrey Mieno.
 
Mtibwa ambayo imekuwa ikikumbana na vipigo vikubwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kutoka kwa Azam, ilijaribu kucharuka ili kusawazisha goli hilo katika dakika za lala salama lakini ilijikuta ikifungwa goli la tatu na Tchetche, ambalo lilikuwa ni lake la tisa katika dakika ya 89.

Wakati mashabiki wa nyumbani wakiamini kwamba angalau matokeo yangebaki hivyo, Tchetche tena alifunga goli lake la 10 na la nne kwa Azam katika dakika za majeruhi.
Kikosi cha Azam kilikuwa: Mwadini Ali, Himid Mao, Malika Ndeule, David Mwantika, Joakins Atudo, Humprey Mieno, Salum Abubakar 'Sure Boy', Abdi Kassim 'Babi', Kipre BalouBrian Umony na Khamis Mcha.



 

SOURCE: NIPASHE