Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Brandts aipania Lyon

11th February 2013
Print
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts

Kocha wa Yanga, Ernie Brandts, amesema kwamba kesho kutwa anatarajia kushusha kikosi kitakachocheza kwa kasi dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini akaongeza kwamba kasi ya Azam iliyo kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inawalazimisha kupigania ushindi katika kila mchezo.

 
Brandts alisema kwamba ili kufanikiwa, ni vyema kujiandaa kwa ushindi katika kila mchezo na pia kujua kasi ya mpinzani anayewakaribia.
 
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema kwamba ligi bado ni ngumu na lolote linaweza kutokea kwa sababu kila timu inashuka dimbani ikiwa na mipango tofauti.
 
"Ligi ni ngumu na kila mechi lazima ina mipango yake ya kukabiliana nayo. Kwangu nataka wachezaji wawe na kasi na wawe makini wanapokuwa na mpira. Kasi ni kitu muhimu katika kuanzisha mashambulizi," alieleza kocha huyo aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom  Saintief.
 
Yanga ndiyo vinara katika msimamo wa ligi kuu ya Bara wakiwa na pointi 33 wakati watani wao wa jadi, Simba wakiwa nyuma kwa pointi tano. Hata hivyo, Yanga wana mechi moja mkononi.  
 
African Lyon ambayo sasa iko chini ya kocha mpya, Salum Bausi kutoka Zanzibar, ndiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa ligi kutokana na kuwa na pointi 9 tu baada ya kucheza mechi 16.
SOURCE: NIPASHE