Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Papa ang’atuka

12th February 2013
Print
Papa Benedict XVI, akitoa Baraka baada ya kuzungumzia uamuzi wake wa kustaafu wadhifa wake ifikapo Februari 28, mwaka huu kutokana na umri na pia hana nguvu za kumuwezesha kutimiza majukumu yake ya kiofisi.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa 16, ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake kuanzia Februari 28, mwaka huu.

Papa Benedict ameliongoza kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2 ulimwenguni kwa kipindi cha karibu miaka minane baada ya kuchukua uongozi wa kiti hicho Aprili 19, 2005 kufuatia kufariki dunia kwa mtangulizi wake, Papa Yohana Paulo wa Pili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Vatican jana, Padri Federico Lambardi, Papa ameamua kujiuzulu nafasi ya kuliongoza kanisa kutokana na kupungukiwa nguvu za kiakili na kimwili kulikosababishwa na uzee.

Papa Benedict aliwaambia makardinali kwamba ili kuliongoza kanisa katika ulimwengu wa sasa wenye changamoto mbalimbali ikiwamo ya umuhimu wa maisha ya imani, Papa anatakiwa awe na nguvu za kiakili na kimwili, mbali ya moyo wa sala, matendo mema na majitoleo.

Alisema vigezo hivyo vya msingi vya kuiongoza mashua ya Mtakatifu Petro na kuihubiri Injili, vimepungua kwake kwa kipindi cha miezi michache iliyopita kiasi cha kumfanya atambue kuishiwa uwezo wa kutosha kukitumikia kiti hicho kitakatifu.

“Kutokana na sababu hiyo na nikitambua kwa ufasaha uzito wa hatua yangu hii na kwa uhuru wangu wote, natangaza kujitoa kwenye  utume wa Askofu wa Roma na Mrithi wa Mtakatifu Petro,” alisema.

Papa Benedict alisema kwamba kuanzia siku hiyo ya Februari 28, saa nne usiku atakuwa amekiacha wazi kiti cha Roma, kiti cha Mtakatifu Petro na kwa hali hiyo itabidi jopo la makardinali wenye sifa liitishwe kwa ajili ya kumchagua Papa mpya.

ALIKOTOKEA

Papa Benedict alizaliwa Aprili 16, 1927, akiitwa Joseph Aloisius Ratzinger, nchini Ujerumani. Ni papa wa 265 katika mtiririko wa Mapapa wa Kanisa Katoliki tokea enzi ya Mtume Petro.

Ni profesa wa theolojia kuanzia mwaka 1958, akifundisha vyuo mbalimbali huko Ujerumani. Alipata daraja la upadri Juni 29, 1951. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Munich na Freising na wakati huo huo akapewa ukardinali na Papa Paulo wa sita mwaka 1977.

NYADHIFA ALIZOWAHI KUSHIKA
Askofu Mkuu wa Munich na Freising (1977-1982), Kardinali wa Santa Maria (1977-1993), Rais wa Tume ya Kimataifa ya Theolojia (1981-2005), Mkuu wa Kongrogesia ya Mafundisho ya Imani (1981-2005), Rais wa Tume ya Kipapa ya biblia (1981-2005),Kardinali-Askofu wa Velletri-Segni (1993-2005), Mkuu wa Chuo cha makardinali (2002-2005),Papa (April 19, 2005-Februari 28, 2013). 

WANAZUNGUMZIAJE KUHUSIANA NA HATUA YA KUNG’ATUKA

Kanisa Katoliki nchini limepokea uamuzi wa kutangaza kujiuzulu kwa baba Mtakatifu Benedict wa 16 kama ishara ya ujasiri wa kuyaacha madaraka kwa mujibu wa taratibu za Kanisa hilo. Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, aliiambia NIPASHE jana kuwa ingawa hatua hiyo imechukuliwa ghafla, lakini imeacha funzo kwa Kanisa na taasisi nyingine za kijamii.

“Tunachokiona kwa hatua hiyo ni ujasiri, huyu ni mwana teolojia ambaye amelitumikia Kanisa na kufikia mahali, ameamua kwa hiari yake apumzike,” alisema Askofu Kilaini.
Askofu Kilaini alisema ingawa ni takribani miaka 700 tangu kujiuzulu mara ya mwisho kwa Baba Mtakatifu Gregory XII, wapo (Mapapa) wanne waliowahi kufikia hatua kama hiyo.

UTARATIBU WA KUJIUZULU

Alisema awali, utaratibu wa Kanisa Katoliki ulitoa fursa kwa Maaskofu wa Jimbo na Baba Mtakatifu kutumikia hadi wanapofariki, lakini ukabadilishwa na kuwekewa ukomo wa miaka.

Kwa mujibu wa Kilaini ambaye ana taaluma ya Historia ya Kanisa, Askofu wa jimbo anapaswa kustaafu katika umri wa miaka 75 wakati Baba Mtakatifu ni miaka 80.

Hata hivyo, alisema kustaafu huko (hasa kwa Baba Mtakatifu) hakutokani na shinikizo la mamlaka yoyote ya Kanisa isipokuwa uamuzi wake binafsi.

“Uamuzi wa kuweka miaka ulifikiwa kwa sababu za msingi zikiwamo kuchoka kwa ubongo na nguvu za mwili, hivyo ni jambo la kawaida linalokubalika kwa mujibu wa taratibu za Kanisa,” alisema.

Aliongeza: “Kwa hiyo ni uamuzi binafsi usiotokana na shinikizo lolote, ingawa kuna fursa ya kushauriwa, lakini uamuzi unabaki kwake.”

MTIKISIKO WA KANISA

Askofu Kilaini alisema kuwa mtikiso ndani ya Kanisa unaotokana na hoja kadhaa zinazotolewa isivyo rasmi, hauna nafasi katika sababu za kujiuzulu Baba Mtakatifu Benedict wa 16.

Alisema Baba Mtakatifu ana historia ya kukabiliana na mitikisiko tangu akiwa Askofu wa Munich nchini Ujerumani, na miaka ya mwanzo ya utawala wake Vatican.

Pia Askofu Kilaini alisema hata akiwa ofisi ya mafundisho ya dini, Baba Mtakatifu alikabiliana na mitikisiko ukiwemo wa ‘kuliasi’ kanisa kwa aliyekuwa kiongozi wa kanisa Katoliki nchini Zambia, Askofu Mkuu Emmanuel Milingo (83).

Milingo alitengwa mwaka 2006 kwa kuoa na kujaribu kuwatawaza mapadri wanne kuwa maaskofu.

“Hata alipoanza katika wadhifa wa Upapa, ilikuwa ni kilele cha matatizo ya mapadri wenye watoto, ikatofautiana na Waislamu na baadaye tafsiri ya kitabu chake…lakini hakujiuzulu,” alisema Askofu Kilaini.

HATAHUSIKA KUMCHAGUA PAPA MPYA
Askofu Kilaini alisema ingawa hii ni mara ya kwanza kwa ‘miaka ya karibuni’ kufikiwa hatua hiyo, lakini utaratibu wa kumpata Baba Mtakatifu mwingine, hautamhusisha Papa Benedict wa 16.

“Utaratibu ni ule ule, tofauti ni kwamba utafanyika wakati aliyepo yupo hai, lakini hakuna kitakachobadilika,hatahusika kwa vyovyote vile,” alisema.

Ingawa hakuingia kwa undani zaidi, Askofu Kilaini alisema kwa mujibu wa Kanisa Katoliki, mchakato wa kumpata Baba Mtakatifu ‘mpya’ utaongozwa na Kardinali Kiongozi aliyepo Vatican.

MAISHA YAKE BAADA YA KUJIUZULU

Askofu Kilaini alisema hakuna maelekezo maalum yanayotolewa kuhusu mahali na kazi anazopaswa kuzifanya Baba Mtakatifu anayejiuzulu, isipokuwa zile zinazomgusa yeye binafsi.
“Kwa mfano, ameshasema kazi yake itakuwa ni kusali, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Baba Mtakatifu Selestine V aliyejizulu mwaka 1296, kwa hiyo atabaki kusali na kuliombea kanisa,” alisema Askofu Kilaini.

MAKAZI YAKE BAADA YA KUJIUZULU

Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, hakuna mamlaka inayoweza kumchagulia Baba Mtakatifu Benedict wa 16 makazi yake baada ya kujiuzulu, isipokuwa yeye mwenyewe.

“Tukio hili linagusa utashi wa Baba Mtakatifu mwenyewe, anaweza kubaki Roma ama mahali popote anapoona panamfaa,”

SERIKALI YA UJERUMANI YANENA
Msemaji wa Serikali ya Ujerumani nyumbani kwa Papa Benedict wa 16, alisema ameguswa na uamuzi wa ghafla wa kujiuzulu kwa Papa.

“Serikali ya Ujerumani ina heshima kubwa kwa Baba Mtakatifu kwa kile alichokifanya na kwa mchango wake mkubwa katika utumishi wa Kanisa Katoliki,” alisema.

Alisema ameacha chapa kama mbunifu katika kiti cha Kanisa na pia kama mchungaji.

ITALIA YANENA
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Italia, Mario Monti, alinukuliwa akisema: “Nimepatwa na mshtuko mkubwa kwa habari ambazo hazikutegemewa.”
 

SOURCE: NIPASHE