Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Faustine Shilogile
Watu wawili, mama na mwanawe, wakazi wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wameteketea kwa moto wakiwa ndani ya kibanda chao kilichokuwa shambani.
Kibanda hicho kiliangukia kwenye moto wa kupikia chakula kutokana na upepo mkali.
Waliokufa katika tukio hilo ni Alaga Hamza (26) na mwanawe Ali Hamza (5).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Faustine Shilogile, tukio hilo lilitokea Februari 9, mwaka huu saa 2:15 usiku eneo la Gomela mashambani wilayani Kilosa.
Kamanda Shilogile alisema upepo mkali ulivuma na kuangusha kibanda hicho cha nyasi mali ya Hamza Standi (37), na kuangukia kwenye moto.
Hata hivyo, alisema baba wa mtoto huyo, Hamza, hakuwamo ndani ya kibanda hicho wakati tukio hilo likitokea.
Wakati huo huo, Potner Andrew (17), amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia upande wa khanga katika chumba alichokuwa akilala eneo la Shule ya Sekondari Reginald Mundi Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.
Kamanda Shilogile alisema tukio hilo lilitokea Februari 9, mwaka huu, saa 7:00 mchana katika kijiji cha Makunganya wilayani humo.
Hata hivyo, alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika.