


Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra), imesema kukithiri kwa vitendo vya upandishwaji nauli kiholela unaofanywa na madereva wa mabasi ya abiria mijini maarufu kama daladala, kunachangiwa na abiria wenyewe.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray, alisema abiria wenyewe wamekuwa chanzo kukubwa cha kukwamisha juhudi zinazofanywa na mamlaka hiyo za kukabiliana na vitendo hivyo vya uvunjaji wa sheria za usafiri barabarani.
Kutolewa kwa kauli hiyo, kunafuatia na gazeti hili kumtaka meneja huyo aeleze namna Sumatra ilivyojipanga kukabiliana na kuongezeka kwa upandishwaji kiholela wa nauli unaofanywa na madereva wanaoendesha vyombo hivyo vya usafri hususani katika vituo vingi katika Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya vituo hivyo ni Mwenge hadi Tegeta, Mwenge-Kimara- Mbezi ambapo nauli yake hufikia kati ya Sh. 500 na 1,000 hasa nyakati za jioni badala ya Sh. 300 iliyoidhinishwa na Sumatra.
Alisema mbali na magari hayo kupandisha nauli, lakini abiria wanakubali kutoa na kufanya vita dhidi ya vitendo hivyo kuwa ngumu.
“Watu wafuate sheria. Siyo kwamba hatufanyi kazi, tunafanya sana kazi. Kwa kweli tunawatoza sana faini.
Kwa mfano tuliweka watu wetu walikuwa wanaandika namba za magari ambayo yanapandisha nauli kiholela. Mmiliki wa gari husika anatozwa faini, lakini vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea kuongezeka kutokana na abiria wenyewe kutoonyesha ushirikiano kwa mamlaka," alisema.
Aliongeza: “Sisi hatuwezi kuwa kwenye kila basi. Kwa mfano, tunapokuwa tunawauliza abiria iwapo madereva hao wanapandisha nauli katika kituo fulani, wanakataa kwa kuwatetea huku wamewaona wanapandisha nauli, huvyo watu wafuate sheria.”
Kufuatia hali hiyo, Sumatra imeanzisha utaratibu wa kuwataka wamiliki wote wa vyombo hivyo vya usafiri kuwa katika kampuni zenye magari mengi ambao kwa mujibu wa Mziray, usajili unatarajiwa kuanza rasmi Julai, mwaka huu.