


Beki wa kati wa Yanga, raia wa Rwanda Mbuyu Twite, huenda akakosa mechu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya African Lyon itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi.
Jana asubuhi, Twite alikuwa ni mchezaji pekee ambaye hakufanya mazoezi na kikosi hicho wakati wachezaji wenzake wa kigeni, Haruna Niyonzima na Hamisi Kiiza, walirejea nchini juzi na kujumuika na wenzao kufanya mazoezi chini ya kocha Mholanzi, Ernest Brandts.
Msemaji wa timu hiyo, Baraka Kizuguto, alisema jana kwamba wachezaji wako kambini na wanaamini kuwa wataendeleza kasi ya ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwavua ubingwa watani zao Simba.
Alisema kuwa ushirikiano na umoja wa wanachama uliopo sasa ndiyo siri ya mafanikio ya timu yao.
"Tunajua ligi ni ngumu lakini tunakiamini kikosi chetu kwamba kiko tayari kupambana na kuhakikisha kinatwaa ubingwa...tunajua bado ni mapema kujihakikishia licha ya kuongoza kwenye msimamo," alisema Kizuguto.
Yanga ndiyo vinara katika msimamo wa ligi hiyo ambapo wana pointi 33 sawa na Azam lakini Yanga ikiwa na magoli mengi ya kufunga kulinganisha na ‘wauza koni’ hao.