Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Barua yangu kwa Takukuru

12th February 2013
Print

Salaam Aleikhum ndugu wote wa Takukuru na hasa, Mkurugenzi Dk. Edward Hosea. Nawatakia mwaka mpya wenye heri na fanaka katika harakati zenu za kuondoa kama sio kutokomeza rushwa na aina zote za ufisadi katika jamii yetu.

Sisi wananchi tunaoathirika kwa mifumo hii onevu ya kifisadi, tunawakumbusha kuwa tunateseka sana na tunahitaji sasa mfanye upembuzi yakinifu katika kudhibiti na kutokomeza tatizo hilo sugu. Kama Mtanzania, ningependa kuwakumbusha yafuatayo kuhusu rushwa.

Ndugu wa Takukuru, rushwa haitokei kwa bahati mbaya, ni zao la mfumo wa kiuchumi, na kusimamiwa na siasa (au wana siasa). Na kama mfumo unaozalisha ufisadi hauwezi kutokomezwa kwanza basi nashauri kuwa taasisi hiyo isimamishwe kazi kwanza kwa muda mrefu ili kodi zetu zitumike kwa mambo mengine.

Ndugu wa Takukuru, unapoona kuwa uchumi wa nchi unadorora kiasi kwamba uhakika wa nchi kujiendesha kwa uhuru haupo. Na kuwa asilimia kubwa ya bajeti ya nchi haitegemei pato la ndani inayotokana na kilimo viwanda na huduma, bali mikopo na misaada kutoka nje na ndani. Na kuwa uwezo wa serikali kukusanya mapato unaathiriwa na uzalishaji mdogo katika sekta.

Kwa sababu ya usimamizi mbaya, wa  kutegemea teknolojia ya zamani (hasa katika kilimo),  kushindwa kuwa na sera nzuri za usimamizi wa mapato yanayotokana na maliasili zetu.
Na kwa sababu ya kushindwa kusimamia nguvu kazi(vijana wengi hawana ajira inayoeleweka na kwa hiyo tuna idadi kubwa ya watanzania wasiotoa kodi yoyote serikalini na huduma wanazipata), maana yake ni kuwa nchi haiwezi kuwa na uchumi mzuri.

Nchi hii inategemea uagizaji bidhaa za walaji toka nje zaidi kuliko kutoka ndani. Maana yake ni kuwa uwezo wa serikali sasa kujiendesha kwa kimaendeleo unapungua. Serikali inajiendesha kwa kujikimu.

Na kuendesha kwa kujikimu maana yake ni kuwalipa mishahara wafanyakazi wake tu; kulipa gharama za uendeshaji serikali, na hakuna uwekezaji mkubwa katika sekta ya maendeleo.
Ndugu wa Takukuru, madhara ya kudhoofika kwa pato la serikali ni kujenga hisia potofu za kuwa nchi ni maskini na haina uwezo wa kujiendesha Na hili humtia kila mtu tumbo joto na kuona sasa ni wakati wa kuwahi kuchukua chako kabla ya rasilimali hizo hazijaisha. Ishara ya msimamo huo ni katika chaguzi za vyama. Ndugu  wanaingizana kwenye madaraka, kwenye serikali na sekta binafsi. Ndugu wanaingizana kwenye ajira.
 
Wote wanahisi kuwa ukikaa nje ya mfumo, uhaba wa rasilimali uliotengenezwa kutokana na mfumo mbaya, utawaathiri.  Lakini kumbe sio kweli, rasilimali hazijaisha, ila zinasimamiwa vibaya, zinatumika kwa faida ya watu wachache ambao pia wamezihodhi (wa ndani na wa nje), na kama hilo hamtaweza kulisimamia, mjue kuwa hakutakuwa na mafanikio katika mapambano ya rushwa. 
 
Nitataka kusisitiza hapo ndugu wa Takukuru, kuwa katika nchi yoyote ambao uchumi unalegalega na hakuna uhakika wa kesho, mapambano dhidi ya ufisadi yanakuwa magumu sana na pengine hayawezi kufanikiwa kabisa.

Ninawahakikishia ndugu wa Takukuru kuwa mapambano yenu hayawezi kufanikiwa kama pia hamtaishughulikia ekolojia yote inayozalisha na kuulinda mfumo wa ufisadi.

Kwanza mimi mwathirika wa ufisadi inanishangaza kuona kuwa baadhi ya watumishi wa sekta nyeti wamejiingiza katika biashara kama wafanyabiashara wengine tu. Wana makampuni ya utalii, magari, wanaendesha baa, mahoteli na kadhalika.
                                  
Sasa kama ofisa wa jeshi, polisi, Takukuru au usalama wa taifa wanabiashara zao. Na biashara huwa ni moja ya kivutio cha kukwepa rushwa , nyie Takukuru mnawezaje kuidhibiti rushwa. Kama mimi ni mfanyakazi wa TRA ninafika ofisini (biasharani) kwako mheshimiwa sana wa Takukuru, na ukaniambia kuwa ni mheshimiwa sana wa huko, ninaweza kuwa na ujasiri wa kukudai kodi yangu?.                                                                                             
Nikikukamata umepitisha muda wa leseni ya gari lako la biashara na wewe unatoka usalama wa taifa, ninaweza kukukamata kweli? Na kwa sababu hiyo hata sisi ambao kaka zetu wako jeshini na vyeo vyao, wako serikalini na vyeo vyao, wako Takukuru na vyeo vyao, tunalindwa dhidi ya kodi za TRA. Nasema tu kaka yangu ni mkuu wa idara ya ulinzi wa kijiji, TRA wanatetemeka. Wanaondoka.     
                      
 Siwalaumu hawa wanaofanya hivyo kutoka idara nyeti. Nilidhani serikali ingewatengenezea mazingira mazuri sana ya kazi na ajira kiasi cha wao kuwa wanafikiria kazi tu, kwani kipato kingetosha. Sasa kama hili halipo ni wazi wataingia wasikotakiwa na sidhani Takukuru mnaweza kuwazuia wasijiingize katika shughuli na tabia zitakazowasaidia kuongeza faida hata kama njia hizo ni za kifisadi.  

Ndugu wa Takukuru, hivi mnaweza kunikamata mimi kama mtu fisadi kama chama cha siasa kilikuja kwangu kuomba fedha ya ruzuku ya uchaguzi ndani ya chama, au kutumia magari yangu kusafirishia wajumbe, au wajumbe walilala hotelini kwangu bure? Ni wazi hapa kuna nikune mgongo wangu nami nitaukuna wako.

TRA wakija nitawaambia subirini, napiga simu kwa mkuu wa chama, naye anawaambia TRA, subiri subiri, rafiki yetu wa chama hajajipanga, subiri subiri.
 
Wanasubiri na silipi tena. Takukuru mnaweza kuruhusu vyama vya siasa, na hasa kimojawapo kikiwa madarakani, kinafanya mambo ya hivi, mkaacha kukikemea, halafu eti ufisadi utakwisha.                       
                                                                   
Ndugu wa Takukuru, hii ni mifano michache tu ya kwa nini hamuwezi kuutokomeza ufisadi. Wiki ijayo nitaendelea zaidi na mifano mingine.


 

SOURCE: NIPASHE