Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Vifo vya wajawazito , watoto Simiyu ni janga

12th February 2013
Print
Wanawake wajawazito katika baadhi ya maeneo nchini wanaendelea kujifungua kwa kutegemea huduma ya wakunga wa jadi amabo baadhi yao hawana hata elimu ya shule ya msingi.

 Kuna njia nyingi za kukabiliana na tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na vichanga  huko Vijijini. Mojawapo  ni elimu ya afya ya uzazi, mafunzo na vitendea kazi  kwa wataalamu wa afya na wakunga wa jadi katika maeneo ya pembezoni. Huko kuna tatizo kubwa la miundombinu duni kama kwamba siyo sehemu ya Tanzania iliyopata uhuru karibu miongo mitano sasa. Yaani miaka 50 iliyopita.

 
Huko kuna upungufu au hakuna vituo vya kutolea huduma kwa wajawazito na watoto. Pia kuna uhaba mkubwa wa watumishi wenye taaluma, upungufu wa zana muhimu ya kukabiliana na utoaji wa huduma kwenye mazingira kama hayo  na umbali mrefu wa kwenda kupata huduma za rufaa. 
 
Miongoni mwa wilaya zenye  uhaba mkubwa wa utoaji na upatikanaji wa  huduma za afya alizozitembelea mwandishi wa makala haya katika mkoa wa Simiyu ni Bariadi, Meatu na Itilima. Matatizo ya huduma za afya ya jamii yanafanana na hasa kwa akina mama wajawazito na watoto.
 
Paschal Mabiti ni mkuu wa mkoa wa Simiyu. Anatoa wito kwa viongozi wa serikali katika ngazi zote, wadau wote  wa sekta, asasi mbalimbali na wananchi kushiriki kikamilifu  kuboresha afya ya mama na watoto na wachanga huko vijijini ikiwemo  kuchangia kwa hali na mali kwa kutumia raslimali watu na utajiri uliopo mkoani humo hasa mifugo.
 
“Katika malengo yanayoonyesha maeneo ya vipaumbele, vya kushughulikia sekta ya afya ambayo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya jamii, ni pamoja na elimu na huduma ya afya ya uzazi na mtoto, ikiwemo na magonjwa mengine ya malaria,Ukimwi na vifo vya watoto  wenye umri wa siku 0 hadi miaka 5.
 
Zacharia Magembe mkulima  wa kijiji cha Mwasengela na mfanyabiashara katika mji wa Mwanhuzi makao makuu ya wilaya ya Meatu,  anasema, kuwa wananchi wengi nchini wanajua kuwa Malengo ya Milenia yanaonyesha maeneo ya vijijini kupewa kibaumbele hasa yale ya pembezoni.
 
 Anaendelea kusema “licha ya serikali kuwa na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2005, inaelekeza kuboresha huduma za afya  bado mkakati huo ni wa kusuasua, katika baadhi ya maeneo vikiwemo vijiji  vingi vilivyoko pembezoni vinavyoendelea kutegemea wakunga wa jadi, katika suala zima la uzazi salama kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.
 
Kuna umuhimu sasa wa kujielekeza kwa vitendo huko vijijini  kuliko kipindi chochote, kama kweli lengo ni kufikia Malengo ya Milennia 2025.
 
Millembe Ng’wanakabi, mkazi wa kijiji cha Longalonegha, anasema pamoja na kuwepo miradi na juhudi zinazofanywa na serikali na wadau wengine lakini wanawake bado wanafia  majumbani, na kama kuna juhudi zinafanyika basi ni za kusuasua mno hakuna mpango na mkakati wa makusudi wa kumkomboa mwanamke wa kijijini hasa sisi waishio pembeni anasema mama huyo kwa kauli ya kukata tamaa.
 
Dkt Beatus Sambili  ni Mratubu wa Mradi  wa  “UZAZI UZIMA” katika mkoa wa Simiyu , anasema watoto chini ya miaka mitano wapatao milioni sita (6,000,000) hupoteza maisha kila mwaka kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania. 
 
Na akina mama  280,000 hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi. Katika kila kundi la akina mama thelathini na moja (31), mmoja wao hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi,vifo vya mama na mtoto husababishwa na huduma duni za afya, magonjwa ya kuambukiza,  mipango dhaifu kuhusu  huduma za afya katika kaya, vipaumbele butu juu ya huduma za afya, na mfumo duni wa afya wenye tatizo sugu la upungufu wa wataalamu wa afya ya mama na mtoto.
 
Anasema mkoa wao  hauna tofauti na maeneo mengi ya nchi ambako  akina mama wengi wanapoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi,  watoto chini ya miaka mitano  hupoteza maisha kutokana na matatizo yanayoweza kuzuilika.
 
“Kulingana na takwimu kutoka  Mfumo wa Taarifa za uendeshaji  Huduma za Afya (MTUHA-2010), Simiyu pekee ilikuwa na vifo vya watoto chini ya miaka mitano 1696.
 
Takwimu za mwaka 2010 zinaonyesha kuwa kwa nchi ya Tanzania, kwa kila kina mama laki moja kuna akina mama 450 wanaokufa kwa matatizo ya uzazi, hii ni pungufu kutoka vifo 578 kwa takwimu za 2004
 
Dkt Saambili anasema, kupungua kidogo hivi kunatuweka katika tahadhari ya kufanya kazi ya ziada ili tuweze kufikia Malengo ya Milennia ifikapo 2015 ( ambayo ni kupunguza vifo vya akina mama maeneo ya pembezoni, vinavyotokana na matatizo ya uzazi kwa theluthi mbili, ambayo ni takribani kina mama 193  kwa kila kina mama100,000).
 
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mabiti, anasema kuna haja ya jamii kushirikishwa kikamilifu na kujielekeza , hasa kupitia serikali za mitaa na serikali kuu ili kuboresha utoaji wa huduma bora ya mama,watoto na vichanga katika mkoa huo.
 
Sallu Shigella ni ofisa mtendaji wa  kata ambaye amefanikiwa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ndani ya tarafa ya Nyalanja na Kimali wilayani Meatu.
 
Anasema licha ya kuwa na mikakati ya kuhakikisha vifo vya akina mama vinapungua kwa kupata huduma bora, lakini bado wananchi wana hudumiwa na wakunga wa jadi wasio na elimu   na elimu ya afya ya uzazi. Hali hii inatishia usalama wa maisha ya watoto na wajawazito  huko vijijini.
 
Hali hiyo inatokana na mahitaji ya jamii ya kupata huduma ya msingi ya afya ya uzazi na kujikuta baadhi ya  akina baba wanajitolea   kuwa wakunga wa jadi vijijini, kauli inayoungwa mkono na mbunge wa jimbo la Meatu, Meshack Opolukwa anaongeza wananchi wengi wanakabiliwa na kero hiyo.
 
Mbunge huyo anasema, “tutaonekana tunafanya vizuri endapo tu,tutajielekeza na kuwatumikia ipasavyo wananchi wetu kwa kuwaondolea kero kama hizo,” 
 
Baadhi ya akina mama katika vijiji vya pembezoni mkoa wa Simiyu wanasema kuwa sababu  zinazosabisha vifo kwa wajawazito mkoani humo ni pamoja na mifumo pingamizi ya kijamii, ukiwemo kukimbilia kwa waganga wa jadi na wakunga wasio hata na elimu ya awali ya kumhudumia mjamzito, mfumo dume unaosababisha  akina mama na vijana wakiwemo wasichana kuchelewa au kushindwa kabisa kupata elimu na huduma, zikiwemo za uzazi wa mpango na kukumbwa na matatizo ya kiafya yasiyo ya lazima.
 
“Akina mama  tunaona tumesahaulika huku vijijini kwani hata hizo huduma tunazisikia kwenu tu.  Hatuna wa kushauriana na familia na kufuata maamuzi  yanayotolewa na hauwezi kupinga zaidi ya kufuata hata kama unaumia na kama unatokwa na damu,” anasema Ngwashi Maduhu wa kijiji cha Mwasengela tarafa ya Kisesa wilaya ya Meatu.  
 
Dkt John Assey ni Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Bariadi, inayohudumia  baadhi ya wananchi wa wilaya mpya za Itilima na Busega, anasema sababu zinazosabasha vifo kwa wajawazito, katika maeneo mengi ya mkoa huo kuwa, ni pamoja na kutokwa damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, uambukizo, uzazi pingamizi, fistula, upungufu wa damu, kuharibika kwa mimba licha ya kuwepo vifo vya uzazi kutokana na Ukimwi na malaria. 
 
Avelina Kyakwambala ni diwani wa halmashauri ya wilaya ya Meatu anasema, wakati umefika kwa jamii kujielekeza vijijini, na ikibidi mpango wa mfuko wa jamii uelekezwe zaidi kwa maeneo ya vijijini. 
 
“Kuna haja ya kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa tunatekeleza miradi ya maeneo ya pembezoni ikiwemo ya afya, miundo mbinu,” anasema diwani huyo ambaye kitaaluma ni Muuguzi. 
 
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu, Isaya Moses anakiri kuwepo kwa hali hiyo na  uduni katika maeneo ya pembezoni na kusema, halmashauri  zinakabiliwa na tatizo la uhaba wa fedha  katika utekelezaji wa huduma za  afya vijijini. 
 
Mkurugenzi huyo anasema, lengo ni kuhakikisha  kuwa wananchi  wanaondokana na kero, zikiwemo za afya miundo mbinu, na kuna haja ya kutoa kipaumbele katika bajeti, kukabiliana na changamoto hizo. 
 
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mabiti anakiri kuendelea kusema  kuwa moja ya mbinu ni kuhakikisha kuwa kila halmashauri ya wilaya na jamii inashiriki kwa kujielekeza katika kuondoa tatizo hilo, katika  kata 111 za wilaya tano za mkoa mpya wa Simiyu, hasa maeneo ya pembezoni yenye changamoto nyingi.
 
Mkoa wa Simiyu kama ilivyo mikoa mingine  nchini, unachangamoto nyingi zikiwemo  uhaba wa watumishi wenye taaluma, uchache wa vituo vya kutolea huduma za afya na  mgonjwa kusafiri umbali mrefu kupata huduma.
 
Changamoto nyingine  ni  mapungufu katika utoaji wa  rufaa kwa wagonjwa, matumizi kidogo ya huduma  za  uzazi wa mpango, ufinyu wa bajeti katika utoaji wa huduma mbalimbali za afya kwa jamii, hasa maeneo ya vijijini, matumizi madogo ya takwimu katika kuandaa  na kutekeleza mipango ya afya, na upatikanaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati na kwa usahihi katika ngazi mbalimbali, na sasa juhudi za pamoja zinahitajika kujielekeza huko kabla mambo hayajaharibika.
 
SOURCE: NIPASHE