Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nasra: Mfanyakazi wa ndani aibukia sekondari

12th February 2013
Print
Comments
Nasra Mbwela

Nasra Mbwela ana kiu kubwa ya elimu na kumsaidia mama yake mzazi  afaulu kimaisha baada ya baba yake kufariki. Umaskini wa mama yake na ukame unaochangia kilimo chao kisiwe na tija akaamua kwenda kufanya kazi za ndani ili apate ada na kumsaidia mama yake.

Amepigwa na kunyanyaswa katika ajira hiyo.  Sasa ni mwanafunzi wa sekondari ya Zimbwini  wilayani Rufiji na anatamani kuendelea hadi Chuo Kikuu. Makala haya yaeleza zaidi.

Nasra  Mbwela, 14,  ni mwanafunzi  wa  shule ya sekondari ya  Zimbwini,  wilayani  Rufiji mkoani Pwani. Ana ndoto ya kuwa mhasibu.

Baada ya kufiwa na  baba yake mzazi mwaka 2009  amekabiliwa na  hali ngumu ya maisha yenye misukosuko mingi iliyomlazimisha kufanya  kazi  za ndani jijini Dar es Salaam. Amezaliwa wilayani  Rufiji mkoani Pwani.

Amehitimu elimu ya msingi  mwaka 2011 katika shule ya  Nyamakonge, Kibiti, wilayani Rufiji.  Ni mtoto wa kwanza kwa familia ya Mzee Mbwela.  Kwa upande wa mama yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa.Ndugu yake ambaye wamezaliwa na baba tofauti anaishi na baba yake.

Baada ya baba yake kufariki  mwaka  2009, akabaki akilelewa na mama ambaye ni  mkulima wa mazao ya mihogo, mahindi na mengineyo.

Licha ya juhudi za mama yake katika kilimo lakini  hali ya ukame ilichangia  kufanya  wapate mavuno , kwa sababu  mazao yanakauka. Hali hiyo ikachangia kuwafanya wawe na maisha magumu hata kujikuta wakishinda  na kulala na njaa katika familia yao.
 
“ Wakati mwingine tunakula au  hakuna chakula. Niliumia sana kumuona mama anateseseka.
Akanifahamisha kwamba hana  fedha za kugharamia elimu yake . Hali hiyo  baada ya kutafakari sana  nikaamua kwenda   kutafuta kazi za ndani wakati nikisubiri  matokeo ya darasa la saba. Mama alisema hata kama nikifaulu  hajui  kama nitaweza kukosomesha.Mazao yanapandwa na kukauka hana tegemeo jingine,” anasema kwa machungu na kukubujikwa machozi.
  

Alikwenda jijini Dar es salaam kufanya kazi za ndani  mwaka 2011 mara baada ya kumaliza elimu ya msingi. Lengo lake ni kutafuta ada ya kugharamia elimu yake na kumsaidia mama yake kimaisha.

Anasema mama yake  alikuwa mkulima  wa mazao ya mihogo, korosho, na mahindi aliyokuwa akiyategemea kujikimu na maisha. Hata hivyo, mavuno kidogo kutokana na ukame wa mara kwa mara ulisababisha wawe na matatizo makubwa ya kifedha.

Baada ya miezi mitatu tangu ahitimu elimu ya msingi alienda  Dar es Salaam kufanya kazi kwa mama mmoja mfanyabiashara mkazi wa maeneo ya Kigogo.  Aliahidiwa mshahara wa sh.40,000 kwa mwezi aliotarajia kuutumia  kulipia ada ya shule na kumsaidia mama yake kujikimu kimaisha.

“Nilipofika mwanzoni  mama huyo alinipokea vizuri.  Lakini  kadri muda  ulivyozidi kupita  ndivyo kazi yangu niliiona kuwa ngumu sana. Nilikuwa siruhusiwi kulala mapema na sipati muda wa kupumzika. Pia  ukikosea kidogo tu, mama huyu alikuwa ananifokea  sana  na kunipiga,  glasi  ikivunjika kwa bahati mbaya unatakiwa kulipa. Mama huyo  pia anadharau sana wafanyakazi wa ndani,” anasema.

Kama hiyo haitoshi, mama huyo  akirudi nyumbani  mathalani muda wa saa mbili usiku, hutakiwa kumsubiri ale chakula kwa muda anaoutaka hata kama ni saa mbili baadaye ili akimaliza  atoe vyombo vya chakula na kwenda kuviosha kisha ndipo aruhusiwe kwenda kulala.

“Wakati nafanya kazi kwa mama huyu  mfanyabiashara niliteseka  sana. Nilikuwa napigwa vibaya  sana.Hakuwa anafundisha au kuelekeza yeye ni kusema kwa ukali na kukutesa hata kuyafanya maisha kuwa magumu.” Anasema kwa masikitiko.

Msichana huyo,  aliendelea kufanya kazi hapo hadi Mwalimu Mkuu wa shule ya Nyamakonge alipompigia simu mama yake na kumtaarifu kuwa amechaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza katika shule  ya sekondari Zimbwini,Rufiji.

Mama yake, baada ya kupata taarifa hiyo alifurahi sana licha ya kuwa aliwaza namna ya kupata fedha za kumgharamia kijana wake. Baada ya hapo, alimpigia simu mwajiri wake  na kumfahamisha kuwa amefaulu.

Taarifa hizo zilimfikia  Nasra wakati anapiga deki na kufanya usafi ndani. Ilikuwa Machi 2012.

“ Baada ya kupata taarifa hizo nilifurahi sana kwa sababu niliona nimejitoa katika mateso  niliyokuwa  nayapata wakati nafanya kazi za ndani kwa mama huyo,” anasema.
Aliamua kuacha kazi  na kurudi nyumbani Kibiti.  Huko mama alimfahamisha kuwa hana uwezo wa kumudu gharama zake za elimu.

Hata hivyo, akapata habari njema kutoka kwa mwalimu wake mkuu kwamba kwa sababu darasani alikuwa anajimudu vyema  aliombewa msaada katika   shirika la  Camfed Tanzania linalojishughulisha na kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, yatima na wanaotoka katika familia maskini kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Mwezi April mwaka 2012 akajiunga na shule ya sekondari ya Zimbwini. Alifurahi sana kuona sasa ndoto zake za elimu zinaanza kutimia. Na ameapa kwamba ana malengo ya kufanya vizuri  shuleni hadi afikie ngazi ya chuo kikuu.

Camfed Tanzania walimfadhili  mahitaji yote ya msingi ya shule yakiwemo  sare za shule , madaftari, ada,  viatu, na fedha  za matumizi ikiwemo kuwekewa Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu na sehemu ya kulala ili  aweze kusoma vizuri pamoja na  watoto wengine yatima kutoka vijiji mbalimbali  wilayani Rufiji.

“Kwa kweli naishukuru sana Camfed Tanzania  kunifadhili elimu yangu na naahidi nitaitumia fursa hiyo  hadi nimalize vizuri elimu ya sekondari. Pia wameniahidi kunigharamia hadi ngazi ya chuo kikuu kama nitafaulu vizuri katika masomo yangu,”anasema Nasra huku akilia na kufuta machozi.

Masomo  anayopenda kusoma ni kemia, hisabati,kiingereza na biolojia.Lengo lake maishani anatamani siku moja afanye kazi ya uhasibu  ili aisaidie jamii na hasa  mama yake mzazi amwinue kiuchumi.

Mwanafunzi  huyo  anawashauri  wasichana wenzake wanaofanya  kazi za ndani, wafanye kazi kwa malengo, wawe wavumilivu na  wakiweza kujiendeleza  kielimu wafanya hivyo  kwa sababu dunia  inabadilika ,  yawezekana wazazi wakafa na kuwaacha wakiteseka  hasa kama familia hiyo haina mtu mwenye uwezo au ambaye anajua thamani ya elimu na kuwafanye wabaki wakihangaika .

Kuhusu waajiri wanaopata huduma ya wasaidizi wa ndani, Nasra anawashauri waishi nao vizuri kama watoto wao, wapatiwe mahitaji kama ndugu zao na pia wawe wanawasaidia  kufanya kazi inapobidi hiyo itawafanya wahisi kuthaminiwa na kuwa moyo wa kufanya kazi za ndani wakiwa na amani na utulivu.

Akikumbukia mazingira aliyokuwa akifanyia kazi, anasema kwamba alikuwa  hapendi kabisa kupigwa. Kero hiyo ilimfanya achukie na kujuta  kufanya kazi za ndani licha ya kwamba alikuwa na shida ya kupata  ada  ya  shule.

Shirika la Camfed linafanya kazi katika wilaya kumi  za  Kibaha, Bagamoyo na Rufiji (Pwani) , Kilolo, Iringa vijijini (Iringa) ,  Morogoro vijijini, Kilombero,(Morogoro)  Pangani na Handeni (Tanga)  kuwawezesha kielimu watoto wa kike wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima waliopo shuleni na kuwawezesha  kiuchumi wasichana wa vijijini kwa kuwapa mafunzo ya biashara na mitaji .

Mkurugenzi wa bodi ya Camfed Tanzania, Dk. Stella Bendera anasema  tangu  shirika hilo lianzishwe  mwaka 2006  wasichana 3326 wamelipiwa gharama zote za masomo kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu katika wilaya hizo.

Pia  wanafunzi 10,469 wamenufaika na mfuko wa dharura na tayari wajumbe 177 kati 189 wa Camfed wamepata mafunzo ya uhamasishaji jamii na msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaoishi  katika  mazingira hatarishi.

Wajumbe hao ni kutoka wilaya za Handeni, Pangani, Rufiji, Bagamoyo,Kilosa, Kilombero, Morogoro vijijini, Iringa na Kilolo.

Shule  193 zimepata msaada wa vitabu na walimu walezi 157 wamepata mafunzo ya msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi.

Akizungumzia  changamoto zinazowakabili katika shirika lake, anasema kuwa  baadhi ya  wanafunzi wanaofadhiliwa wanaacha shule  baada ya kupachikwa ujauzito,  ufaulu mdogo, utoro na walimu walezi waliopewa mafunzo kuhamishwa shule.

Changamoto nyingine ni  baadhi ya walimu wakuu na walimu walezi  kutumia vibaya fedha za walengwa kwa wakuu wa shule.

Mlezi wa wanafunzi katika shule ya sekondari Zimbwini , Latifa Sabuni anasema kwa sababu ya  watoto wengi kuishi vijijini katika maisha magumu na kulazimika kutembea umbali mrefu sasa wana mpango wa kupanga nyumba   watakayoishi  watoto wote wanaofadhiliwa na Camfed Tanzania katika shule yao.

Wanachosubiri sasa ni jengo hilo kuwekewa umeme ili wanafunzi waanze  kuishi na kusomea katika mazingira mazuri

Pia anawaomba  Camfed Tanzania waongeze  kutoa kiwango kikubwa zaidi  cha fedha kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi kwa sababu fedha zinazotolewa hivi sasa hazitoshelezi.

“Hebu angalia  kila  mwanafunzi analipiwa  kodi ya nyumba sh 75,000 kwa mwezi. Kwa upande wa vitu vya darasani  mathalani  madaftari, peni, mkebe wa vifaa vya kupimia wanatoa sh 15,000.Ni vyema  wangeongeza hadi sh. 30,000 kulingana na gharama za sasa,” anasema
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment