Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanafunzi, wananchi wafanya vurugu kubwa

16th May 2012
Print
Comments

Wananchi na wanafunzi wamezua vurugu kubwa katika mikoa ya Mbeya, Pwani na Morogoro na kuwalazimisha polisi kuingilia kati na kutumia mabomu.

Tukio la kwanza lilitokea katika mji mdogo wa Kiwira wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya juzi, baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kupambana na wananchi waliokuwa wakiziba barabara kuu ya kwenda Malawi na kupiga magari mawe ili kushinikiza wenzao sita waliokamatwa na polisi waachiwe huru.

Vurugu hizo zilianza Jumapili majira ya saa 9:30 alasiri, wakati kundi la wananchi zaidi ya 200 kutoka kijiji cha Ilundo kuvamia kituo kidogo cha polisi cha mjini Kiwira na kuwataka Polisi kuwaachia wenzao.

Hata hivyo, Polisi waliamua kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia mabomu ya machozi na ndipo wananchi hao walipoungana na baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Kiwira na kuzua vurugu kubwa.

Kufuatia vurugu hizo, askari wa FFU kutoka jijini Mbeya walipelekwa Kiwira na kuanza kupambana nao hadi majira ya saa 5:30 usiku kisha barabara hiyo ikafunguliwa na hali ya usalama kurejea katika eneo hilo.

Mkazi wa kijiji cha Ilundo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini aliliambia NIPASHE kuwa, sababu za kukamatwa kwa wenzao ni Mwenyekiti wa kijiji chao, Michael Mwangosi, kuondoka kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kijijini hapo na wananchi kumshinikiza ajiuzulu.

Alisema katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kiwira, Laurent Mwakalebule (Chadema) na Ofisa Mtendani wa kata hiyo, Lauden Nnala, wananchi walimtuhumu mwenyekiti huyo kuwa ameuza ardhi ya kijiji zaidi ya ekari 64 pamoja na kufanya maamuzi mbalimbali bila kuwashirikisha wananchi.

Alisema pia wananchi walidai kutoelewa mapato na matumizi ya fedha za umma, hali iliyosababisha kutokuwa na imani na mwenyekiti huyo, hivyo wakaamua wote kwa kauli moja kumtaka ajiuzulu.

Alisema mwenyekiti huyo licha kukana tuhuma hizo, alikataa kujiuzulu na badala yake aliamua kuondoka mkutanoni, kitendo kilichowakasirisha wananchi na kuamua kuvamia ofisi ya kijiji na kuanza kuipiga mawe, kuvunja vioo vya madirisha, kushusha bendera ya taifa iliyokuwa imetundikwa mbele ya ofisi hiyo na kuichana vipande vipande.

Baada ya muda mfupi askari polisi waliwasili kijijini hapo na kukuta wananchi wameshatawanyika, hivyo wakaingia ndani ya ofisi na kuchukua nyaraka muhimu na kuondoka.

Alisema juzi (Jumatatu) asubuhi askari walirudi tena kijijini hapo na kuwakamata wenzao sita, kitendo ambacho wengine hawakukubaliana nacho, hivyo wakaamua kukusanyika na kwenda polisi kwa nia ya kuwashinikiza polisi wawaachie huru.

“Sisi tulikwenda polisi kuwaomba wawaachie huru wenzetu kwa amani kwa sababu hawakuwakamata kwenye eneo la tukio, lakini badala ya  kutusikiliza waliamua kutupiga mabomu na ndiyo sababu na sisi tukaamua kufanya fujo na kufunga barabara,” alisema mwananchi huyo.

Vurugu hizo jana zilisababisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mwenyekit wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kwenda kijijini hapo kuzungumza na wanachi kwa lengo la kujua kiini cha mgogoro huo.

Akizungumza na wananchi hao jana kwenye mkutano wa hadhara, Kandoro, aliwahoji wananchi kama kitendo cha kufanya vurugu na kuvunja mali ya umma ni sahihi, na ndipo baadhi yao walipokiri kuwa walifanya makosa kutokana na hasira walizokuwa nazo ambazo pia zinatokana na kero zao za  muda mrefu ambazo zinasababishwa na mwenyekiti wao.

Aidha, wananchi hao walimweleza Kandoro kuwa kero yao kubwa ni utendaji mbovu wa mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye amekuwa akifuja mali za kijiji na kukwamisha maendeleo yao.

Baadhi ya wananchi hao pia walimuomba Kandoro awaamuru polisi kuwaachia wenzao waliokamatwa.

Baada ya maelezo hayo, Kandoro, alisoma barua aliyopewa na Mwenyekiti wa kijii hicho, Michael Mwanosi, ambayo ilionyesha kuwa amekubali kujiuzulu wadhifa wake.

Kandoro alisema kuwa yeye kama mkuu wa mkoa ana mipaka ya kazi yake, hawezi kuingilia majukumu ya polisi, hivyo wananchi waliokamatwa wataachiwa kwa mujibu wa sheria.

Kandoro aliwasihi wananchi hao kufuata sheria na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa tabia hiyo ina madhara makubwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu 26 walikamatwa na polisi kwa nyakati tofauti kuhusiana na vurugu hizo na jana watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani.

Alisema baada ya kuibuka vurugu hizo, polisi ngazi ya mkoa waliongeza nguvu katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzizima bila kujeruhi mtu.

 WANAFUNZI WAASI MBELE YA WAZIRI

Wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Celina Kombani, iliyopo tarafa ya Mwaya, wilayani Ulanga Mkoa wa Morogoro wameandamana na kufanya vurugu shuleni hapo, wakishinikiza mkuu wa shule hiyo aondolewe wakimtuhumu kuwadhalilisha mbele ya Mbunge wao, Celina Kombani.

Wanafunzi hao waliandamana juzi shuleni hapo wakimtuhumu mkuu wa shule hiyo, Eliamini Matimbwi, kuwa alisoma risala isiyoridhisha mbele ya Kombani  ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma).

Katika risala hiyo, mkuu wa shule alimueleza Kombani kuwa, wanafunzi wa shule hiyo hawafanyi vizuri katika masomo yao kutokana na muda mwingi kujihusisha na masuala ya mapenzi, hali inayochangia kushuka kwa taaluma shuleni hapo.

Pia mkuu huyo wa shule alisema kuwa sababu nyingine ya kufeli kwa wanafunzi ni utovu wa nidhamu na utoro uliokithiri miongoni mwa wanafunzi, huku wazazi na walezi wakishindwa kuwakemea.

Risala hiyo ilimshtua Kombani na kuamua kususia kutoa hotuba na kuondoka, akisema anawashangaa wanafunzi hao kwa kuendekeza upuuzi wakati amewapatia vitu vyote muhimu shuleni hapo.

Vitu ambavyo Kombani ametoa katika shule hiyo ili kulienzi jina lake ni pamoja na kuwawekea umeme wa jua, mashine ya kudurufu, kompyuta, printa, maji, jenereta, luninga na video na vifaa vya maabara. Pia aliipatia walimu wa masomo ya sayansi.

Wanafunzi hao waliandamana huku wakikimbia mitaani na kumtishia mwalimu huyo. Kadhalika walikuwa na mabango yaliyosomeka kuwa ‘hatumtaki mkuu wa shule kwa kututukana mbele ya waziri.’

Polisi waliingilia kati na kuwakamata wanafunzi 21 ambao ndiyo walikuwa viongozi wa maandamano hayo na kuwahoji katika kituo kidogo cha polisi cha  Mwaya na baadaye kuwaachia baada ya kujiridhisha na maelezo yao.

Diwani wa Kata ya Mwaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya  ya Ulanga, Furaha Lilongeli, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kuwa hata yeye risala ya mkuu huyo wa shule haikumpendeza kwani alitakiwa aelezee matatizo ya msingi yanayowahusu wazazi, walimu na wanafunzi na siyo kuwakandamiza wanafunzi peke yao.

Alisema walikubaliana kuwa kabla Kombani kufika wakutane na wazazi na kuangalia nini kinachosababisha shule hiyo kufelisha wanafunzi.

MKUU WA SHULE ANUSURIKA KUUAWA

Katika tukio lingine, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Muhoro iliyopo Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, ameponea chupuchupu kuuawa na wanafunzi baada ya kukimbilia porini akikwepa kipigo kutoka kwa wanafunzi wapatao 400.

Vurugu hizo zilitokea jana asubuhi baada ya wanafunzi hao kuasi na kuzingira shule kabla ya kufunga barabara itokayo Dar es Salaa  kwenda Mtwara na kusababisha abiria kukwama kwa muda.

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja, wanafunzi hao walikuwa wanamtuhumu mwalimu wao aliyejulikana kwa jina moja la Mwita, kuwa anawalisha ugali na maharage kila siku pamoja na kushindwa kuwapa tisheti za shule licha ya kuwa wamezilipia.

Wanafunzi hao pia wanamtuhumu mwalimu huyo kwa kushindwa kuandaa mikakati ya kuwawezesha kushiriki katika michezo ya shule pamoja na kushindwa kuwapatia vitambulisho vya shule.

Shuhuda huyo alisema mwalimu huyo baada ya kuona wanafunzi wameasi na kuanza kuzingira eneo la shule, alikimbilia porini kukwepa kipigo.

Kutokana na vurugu hizo, wanafunzi wawili walijeruhiwa na hali zao ni mbaya, huku wengine 12 wakiwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika wilayani Rufiji.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilisema kuwa, baada ya abiria ambao magari yao yalizuiwa kupita walishuka na kuanza kushirikiana na polisi kuwaondoa wanafunzi hao barabarani.

Mapambano hayo yalikuwa makali baada ya wanafunzi kuanza kuchukua mawe kutoka barabarani na kuanza kuwapiga abiria, ambapo baada ya kuzidiwa walikimbilia vijijini kujificha.

Vurugu hizo zilisababisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, kufika eneo la tukio na kufanya kikao cha dharura jana jioni, ambapo aliahidi kushughulikia kero za wanafunzi hao haraka na kuzipatia ufumbuzi.

Mahiza akizungumza na NIPASHE jana jioni alithibitisha kwenda eneo la shule hiyo kutafuta suluhu ya vurugu hizo.

Mahiza alisema vurugu hizo zilimalizika na kwamba ameuagiza uongozi wa wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kushughulikia madai ya wanafunzi hao.

Hata hivyo, Mahiza alisema wanafunzi hao walikuwa na hoja, lakini hawakuwa na sababu ya kufanya vurugu na kufunga barabara.

“Hawa wanafunzi kufunga barabara na mgogoro wao na uongozi wa shule kuna uhusiano gani kama siyo ukorofi wa wanafunzi?” alihoji.

Alisema wanafunzi wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano ili kubaini vinara walioanzisha vurugu hizo.

Imeandikwa na  Emmanuel Lengwa, Rungwe; Ashton Balaigwa, Ulanga na Richard Makore, Dar.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles