Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Askofu Mokiwa asianze kuhesabu hasara; mchakato wa Katiba ndiyo umeanza

3rd June 2012
Print
Comments

Machafuko yaliyotokea Zanzibar mwisho wa wiki iliyopita yamekuwa pigo kubwa kwa Kanisa Anglikana, ambalo kwa sababu za kihistoria ndilo lenye mizizi zaidi Visiwani, hivyo si jambo la kushangaza kuwa Askofu Valentino Mokiwa, mkuu wa Kanisa hilo nchini, alifanyie kazi ya ziada.

Alichozungumza kimsingi kinafahamika, kuwa siyo mara ya kwanza uchomaji makanisa umetokea, na mara zote vyombo vya usalama Zanzibar vinapendelea suala hilo lipite lisivuruge amani. Ni wazi kuwa suala wanalochelea Zanzibar ni kuwafuatilia wanaochoma makanisa, si uchomaji wenyewe.

Hata hivyo, uchomaji huu wa sasa ni tofauti na ule wa kwanza, ambao unaendana na dukuduku la miaka mingi iwe ni kutokana na masuala ya Muungano au ugomvi ambao umefuata kila uchaguzi mkuu ulipomalizika, ambako wapinzani wanaona dola ya Zanzibar inalindwa na ile ya Muungano.

 

Jambo la kushangaza ni kuwa bila Muungano hata huo uhuru ambao unachezewa na dola ya Zanzibar usingekuwepo, labda kwa kutokea mtafaruku mkubwa halafu uingiliaji kati kutoka kokote duniani, ndipo hali itulie, nchi ielekee tena katika demokrasia. Ni uingiliaji ndiyo ulioleta utulivu uchaguzi wa 2010, yaani hofu ya The Hague.

Hili ni suala (licha ya kuwa ni la kikatiba pia) ambalo bado halijaeleweka, na ndiyo maana vijana wa Zanzibar wanapigania kuvunjika kwa Muungano, kwani hawajaanza kutafakari Zanzibar nje ya Muungano itakuwaje.

Wale walioandamana majuzi, ambao wametoa picha mpya kidogo kwa upande huo, walikuwa wamevalia rasmi, na kufuata ule mwiko muhimu wa kutenganisha waandamanaji wanaume na wanawake, hali ambayo pia iliashiria ni aina gani ya dola wanayotetea, au kupigania. Ndiyo kile unaweza kukiita ‘latest illusion,’ fikra potofu mpya Visiwani, kuwa chini ya dola hiyo kila kitu ni shwari.

Alikuwa akizungumza katika kipindi cha mahojiano TBC Radio, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia, akisema kuwa katika hali ya machafuko kama ile utalii utakwama Zanzibar, hali ambayo itaathiri uchumi wa Zanzibar.

Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kagasheki akatangaza kuwa watalii wako salama Zanzibar na kwingineko nchini, na kwa jumla kama fujo hazitaendelea, inaweza kuonekana ilikuwa ni mlipuko wa kupita tu. Tatizo ni kuwa kuna suala pana zaidi ambalo limechochea hali hiyo, na mpaka limalizike kwa njia itakayowatosheleza waandamanaji hao, bado kuna kitambo kidogo.

Wachangiaji wengine kama Dk. Benson Bana, mkuu wa idara ya taaaluma ya siasa na utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamesema kuwa kama waandamanaji hao hawautaki Muungano, mahali pake si maandamano bali ni kutoa maoni yao mbele ya Tume.

Hapo pia kulikuwa na tatizo, kwani wanaoandamana hawataki watoe mawazo halafu yamezwe na mawazo ya ‘wengi,’ yaani chama tawala na Tume yenyewe, katika uratibu na uandaaji wa mchakato wa maoni yalivyotolewa. Walichokifanya wao ni kuonyesha kuwa Muungano haufai, hautakiwi Zanzibar, na hawatasikia kauli nyingine.

Moja ya vianzio vya kuvuka kutoka uchomaji wa kanisa moja moja kutokana na vianzio tofauti vya ugomvi - kwa mfano kutaka kupora ardhi hiyo, na kwingineko chuki tu ya imani - na kuingia katika kutaka kufuta kabisa uwepo wa makanisa, ni mchakato wa Katiba mpya.

Hali hiyo imetoa suala la kuondoa Muungano kutoka katika dhana ya kundi fulani la kisiasa likijifahamu kuwa ni la wachache na watabaki hivyo wachache, kuwa hali tofauti. Sasa wanajua wanahitaji kufanya vitendo dhihirishi vya hapa na pale, ili kujengeke ushindani wa misingi hiyo ya dini, na kulazimisha suala lielekee upande huo.

Waandamanaji wa Zanzibar walijua fika kuwa ‘wanatingisha kiberiti’ kama alivyowahi kusema Commando Dk. Salmin Amour akiwa rais wa Zanzibar mwaka 1993, kipindi  cha ugomvi kuhusu kuingia kinyemela OIC kama mwangaliaji. Hivi sasa suala siyo tu kutingisha kiberiti bali ni kufanya juhudi ya ziada kufikia kile ambacho kinapatikana, ila kinahitaji kazi ngumu kukamilisha ngwe hiyo, yaani pale ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa upande huo Serikali (ya Mapinduzi) Zanzibar zimeafiki kuwa Katiba iwekwe mezani iandikwe upya.

Hiyo ni pamoja na uwepo wa Muungano; baada ya kukiri  rasmi inawezekana u-katiba wa Muungano kufutwa, wao watapigania hilo, sikutoa wazo. Kwa maana hiyo, suala hapa siyo kuwapinga na kuwalaani waliofanya maandamano na kuchoma makanisa Zanzibar ila kwenda kwenye chanzo cha ‘ujasiri’ huo.

Tatizo ni kuwa Muungano sasa ni kitu kinachoelea ambacho kikifanyiwa kazi (kama ile ya Jumamosi) kitaondolewa - halafu Zanzibar iunde dola inayoitaka, inayoendana na mavazi rasmi waliyovaa, na kutengana kijinsia.

Hawatasikiliza maonyo ya kina Mbatia kuwa utalii utaathirika, au wasifanye vurugu waingojee Tume ifikie tamati inayotaka – watavuruga mazingira kwa misingi ya dini, ila kila mwenye dini hiyo aangalie wapi amesimama.

Kwa vile maaskofu walikuwawatangulizi wa kudai Katiba iandikwe upya, ni budi wajiandae na 'midundo' hadi mchakato huu ukamilike, na kwa njia wa kuwafurahisha waandamanaji wa Zanzibar, na wengine wengi waliojificha Bara. Wasihesabu bado hasara iliyopatikana.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment