


.jpg)
Kikosi cha Suma JKT kimeanza ujenzi wa nyumba 36 za waathirika wa mabomu Gongo la Mboto katika eneo la Msongola lililotengwa na serikali kwa ajili ya makazi mapya ya watu hao.
NIPASHE imeshuhudia juzi ujenzi huo ukiendelea ambapo hadi siku hiyo jumla ya nyumba nane ambazo zinajengwa kulingana na ramani ya awali ya nyumba za mwathirika zilikuwa zimeshainuliwa.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wananchi wa eneo hilo alisema kuwa ujenzi huo ulianza wiki mbili zilizopita baada ya michakato mingine kukamilika.
Alisema ujenzi huo unaenda kwa kasi kutokana na idadi kubwa ya wajenzi waliojitokeza kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Hata hivyo, gazeti hili lilivyotaka kupata maelezo zaidi lini ujenzi huo unatarajia kukamilika, baadhi ya wasimamizi wa ujenzi huo kutoka Suma JKT walikataa kuzungumza hadi wapate kibali cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Sadiki alivyotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia ujenzi huo utakamilika lini, alisema kuwa, makubaliano ya ujenzi huo yalisainiwa baina ya Katibu Tawala wa mkoa (Ras), Theresia Mmbando na wakandarasi hao hivyo yeye hafahamu chochote.
"Leo (jana) nipo mapumziko ningekuwa ofisini ningeitisha mkataba wa ujenzi huu ili nifahamu walikubaliana waanze lini na kumaliza ila nachoweza kusema ni kwamba nilisisitiza sana kazi hii imalizike mapema," alisema.
Gazeti hili lilipomtafuta Ras Mmbando ili azungumzia suala hilo, simu yake ilikuwa haipatikani.
Tukio hilo la milipuko ya mabomu lilitokea Februari 15, mwaka jana katika kambi ya Jeshi la wanachi Tanzania (JWTZ) ya Gongo la Mboto na kusababisha vifo vya watu takriban 20 na majeruhi 400.
Aidha, katika tukio hilo nyumba na mali mbalimbali za wananchi ziliharibiwa na nyingine kupotea kabisa.
Kufuatia hali hiyo serikali ilifanya tathmini ya uhakiki dhidi ya uharibifu huo na kubaini nyumba 75 ndizo zinazotakiwa kujengwa upya kutokana na kuwa na uharibifu mkubwa.
Hata hivyo, baadaye serikali ilipunguza idadi ya nyumba zilizotakiwa kujengwa upya hadi kufikia 36 baada ya uhakiki mwingine kufanyika na kuonekana ndizo zilizopata athari kubwa.