


Sasa kufikishwa mahakamaniWanafunzi saba wanaosoma Shule ya Msingi Yombo Buza, jijini Dar es Salaam wamefukuzwa shule na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kutajwa na wanafunzi wenzao kuwa ni vinara wa kuwalawiti wenzao.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Steven Kailembo, aliithibitishia NIPASHE Jumapili kuhusu kufukuzwa kwa wanafunzi hao kufuatia uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya kushamiri kwa vitendo hivyo katika shule za msingi.
Kailembo aliwataja wanafunzi hao (majina tunayo), baadhi yao wakiwa darasa la saba na wengine darasa la sita, wakati mmoja wao anaendelea kufanyiwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
Mwalimu Kailembo alisema Kamati ya shule imeridhia kufukuzwa kwa wanafunzi hao ili usalama uweze kuwepo kwa wanafunzi waliobaki. "Tumeona tuwafukuze kwani watu wachache hawawezi kutuharibia wanafunzi waliobaki," alisema Kailembo.
Alisema kabla ya kuwafukuza wanafunzi hao walibaini kuwa mwanafunzi wa darasa la nne ambaye ni mvulana alifanyiwa kitendo cha kulawitiwa na kuharibiwa ambapo mpaka sasa bado anaendelea kupatiwa matibabu baada ya kuharibiwa vibaya.
Kailembo alisema taarifa dhidi ya tukio hilo aliliwasilisha kwa Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke ambapo katika kipindi hicho waliagizwa maafisa elimu kulishughulikia suala hilo shuleni hapo.
Alisema baada ya maafisa hao kufika shuleni hapo waliwafundisha wanafunzi kuhusu usalama wao kujitambua na kusema kitendo chochote kibaya wanachokiona au kufanyiwa.
Alisema baada ya hapo zoezi lililofuata kila mwanafunzi alitakiwa kuandika jina la mwanafunzi yeyote ambaye anajihusisha na vitendo vya kuwalawiti wenzake au kama alishawahi kufanyiwa vitendo hivyo aandike na kumtaja mtu aliyemfanyia.
Alisema zoezi hilo llilikwenda vizuri na lilianzia kwa darasa la kwanza hadi la darasa la saba.
Kailembo alisema wanafunzi 11 walitajwa katika shule nzima na kwamba walivyoendelea na uchunguzi wao dhidi ya majina ambayo yametajwa walibaini majina saba ya wanafunzi waliotajwa kuwa vinara wa kuwalawiti wenzao.
"Wanafunzi hao saba ambao wengi wao wapo darasa la saba walionekana ni vinara katika kura zilizopigwa na wanafunzi na maajabu mengine hata wanafunzi wa darasa la kwanza waliwataja katika kura walizopiga na kila darasa lilikuwa likiwataja wanafunzi hao," alisema.
Alisema wanafunzi hao walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Chang'ombe kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu sakata hilo na wanafunzi wanne walifunguliwa kesi.
Alieleza kuwa hata mwanafunzi ambaye alilawitiwa na kuharibiwa ambaye anasoma darasa la nne aliwatambua waliomfanyia kitendo hicho kati ya vinara hao saba.
Hata hivyo, alisema katika zoezi hilo kuna baadhi ya wanafunzi waliwataja ndugu zao kushiriki kuwafanyia vitendo hivyo ikiwemo kuwabaka ama kuwalawiti.
"Kuna wanafunzi wengine walieleza kufanyiwa vitendo hivyo na kaka yao, mwingine ambaye anasoma darasa la sita ameeleza anafanyiwa kitendo hicho na mjomba wake hivyo vitendo hivyo sio mashuleni peke yao hata majumbani vinatokea kwani wameeleza wanafanyiwa na ndugu zao wa karibu," alisema Kailembo.
Kailembo alisema wanafunzi hao saba wamekuwa wakiwalazimisha wenzao kufanya kitendo hicho na kwamba wanapokataa huwatishia kwa vitu vyenye ncha kali ikiwemo viwembe na matokeo yake kukubali kufanya kitendo hicho.
Alisema wanafunzi waliofukuzwa hata mahudhurio yao shuleni hayakuwa mazuri kwani walikuwa wanaishia kushinda mabondeni huku wenzao wakiendelea kusoma darasani.
Aidha, alisema wazazi walijulishwa ili wawe makini kuwafuatilia watoto wao.
Alisema Kamati ya shule iliamua kuchukua hatua hiyo ya kuwafukuza wanafunzi hao sita kwa ajili ya usalama wa wenzao waliobaki na mwingine yupo katika uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
Alieleza kuwa mpaka sasa ni mwanafunzi mmoja tu aliyefikishwa mahakamani na wengine polisi wamemjulisha wanaendelea na uchunguzi wao na utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Kailembo aliendelea kufafanua kuwa kuna eneo ambalo ni maarufu kwa jina la “pori la mhindi” limekuwa likiharibu watoto wengi wa shuleni hapo na hata wa sekondari nao wanaharibikia kupitia pori hilo.
"Hilo pori ni hatari sana kwa sasa linatumika kuwalawiti wanafunzi na kwa baadaye litatumika kwa ajili ya ujambazi kwani wanafunzi huwa wanafika hadi eneo la shule wakishampata mtu wao wanaondoka naye hadi katika bonde hilo na kumfanyia vitendo hivyo," alisema Kailembo.
NIPASHE Jumapili ilimtafuta Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke, Honorina Mumba, kuzungumzia jambo hilo, ambapo alisema kuwa kwa sasa vitendo hivyo vimeshamiri katika mkoa wa Dar es Salaam na sio katika wilaya yake tu.
Alisema jambo la msingi ambalo linatakiwa kufanyika ni kuwa karibu na watoto wao na kuwafuatilia maendeleo yao ya shule.
"Maadili kwa sasa hakuna na hata wazazi hawafuatilii watoto hao unakuta mtoto tangu ameanzishwa shule mzazi hajawahi kufika ili apate taarifa za mwanawe akishaharibika ndio unaona anakuja shuleni hayo sio malezi mazuri kwa mtoto," alisema Mumba.
Mumba alisema kuhusu shule hiyo ya Buza ni kwamba walipatiwa taarifa na kuifanyia kazi jambo hilo kwa haraka ambapo maafisa elimu aliwaagiza kuchunguza sakata hilo na kulitatua mara moja.
Alisema maafisa wake waliandaa somo kwa ajili ya wanafunzi wote wa shule ya msingi ya Buza na ya Amani na walifundishwa kuhusu usalama wao katika kujitambua na kusema.
Hata hivyo, alisema kuna mikakati ambayo wameipanga ili kudhibiti tatizo hilo ambapo wapo katika mchakato wa kujenga uzio wa shule hiyo ili wanafunzi wasitoke nje ya mazingira ya shule na pia kuwazuia watu wengine kuingia ovyo shuleni hapo.
Alisema pia walimu wa madarasa wameagizwa na maafisa elimu kuendelea kutoa elimu ya kujitambua, haki za watoto na watoto kusema mara kwa mara madarasani na hata kwenye baraza la shule kila Ijumaa.
Mumba alifafanua kuwa suala hilo lilijadiliwa katika kikao cha Waratibu wa Elimu kata na Walimu Wakuu Aprili 5, mwaka huu na kutolewa kwa ratiba ya mwanafunzi inayopendekezwa ifuatwe baina ya mzazi ama mlezi pamoja na walimu inayoonyesha mtoto anavyoamka asubuhi anachotakiwa kukifanya mpaka anapofika muda wa kulala.
Akimzungumzia mtoto aliyelawitiwa ambaye anasoma darasa la nne katika shule hiyo ya Buza, alisema mwanafunzi huyo aligundulika na wazazi wake baada ya kuiba Sh 2,000 ambapo aliulizwa na kudai kuwa ameamua kufanya hivyo ili kujinusuru kutendewa vitendo vibaya na vijana wanaojificha mabondeni.