Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mkandarasi atakiwa aondoe kifusi feki barabarani

23rd May 2012
Print
Comments
Ujenzi wa Barabara

Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Mbezi kwa Yusuph kwenda Boko kupitia hifadhi ya Pande jijini Dar es Salaam ametakiwa kuondoa udongo aliouweka katika barabara hiyo kwani haufai kwa kazi ya ukarabati.

Chanzo cha habari kutoka ofisi ya Wakala wa Barabara mkoa wa Dar es Salaam (Tanroads) kilisema kuwa kama hatatii maelekezo hayo, atanyang'anywa kazi hiyo.

Habari za ndani kutoka Tanroads zilisema kuwa mkandarasi huyo tayari alipewa muda mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita awe amekwisha kuuondoa udongo huo barabarani, lakini hadi jana bado alikuwa hajafanya lolote.

Habari hizo zilisema kwa mujibu wa makubaliano katika mkataba wa Tanroads na mkandarasi kazi ya kukarabati barabara hiyo ilitakiwa atumie changarawe ambazo zinakidhi viwango vinavyotakiwa na siyo udongo wa mfinyanzi aliouweka katika maeneo hayo ambao umeleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Kutokana na mkandarasi huyo kukiuka mkataba huo ametakiwa kuuondoa udongo huo kwani ulikuwa unasababisha utelezi na pia haufai kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Taarifa za ndani zinasema kuwa kama mkandarasi huyo hatafanya alivyotakiwa, Tanroads itamuondoa na kumuweka mkandarasi mwingine na atawajibika kulipa gharama za kazi hiyo kutokana na uzembe aliouonyesha katika kufanya kazi hiyo.

"Mkandarasi ametakiwa kuondoa huo udongo aliouweka ifikapo mwishoni mwa wiki hii (iliyopita) kama hatafanya hivyo Tanroads itaweka mkandarasi mwingine na aliyeondolewa atawajibika kulipa gharama hizo ambapo atafanya kazi ya kurekebisha eneo hilo lililotengenezwa kwa viwango duni," alisema.

Aidha alisema utendaji kazi wa mkandarasi huyo ni wa uzembe na katika barabara hiyo ameonyesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza kazi yake kwani alikiuka makubaliano na kuamua kuweka udongo badala ya kuweka changarawe zenye viwango.

Eneo kubwa la barabara hiyo hadi sasa limejaa mashimo makubwa, huku kifusi cha udongo wa mfinyanzi kikiwa kimerundikwa upande mmoja wa barabara na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Wiki iliyopita wakati mvua zilipochachamaa jijini Dar es Salaam, eneo hilo lilikuwa na utelezi wa kutisha kiasi cha kusababisha magari mengine kutumbukia mtaroni.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles