Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kauli za viongozi machakato katiba mpya lawamani

12th May 2012
Print
Comments

Kauli za baadhi ya viongozi wa juu wa serikali zimelaumiwa kutishia na kupunguza hamasa  ya wananchi kushiriki kwenye mchakato wa katiba mpya.

Madai haya yametolewa na Azaki zinashughulikia uhamasishaji washiriki  wa   umma kwenye mchakato wa uandishi wa katiba mpya, wakati wa mkutano na waandishi jana.

Asasi hizo za Jukwaa la Katiba Tanzania na Baraza la Katiba Zanzibar, aidha katika hatua nyingine,  zimesema Tume ya Katiba haiwezi kuendelea na kazi ya kukusanya maoni kabla ya kurekebishwa kwa Sheria Namba 8 ya  2011 ya kuunda tume hiyo ili iweze kutoa uhuru mpana zaidi wa ushiriki wa wananchi.

Katika mkutano huo wa pamoja na wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam , Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema katika kufuatilia maandalizi ya mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya pamoja na uteuzi wa Tume ya Katiba, wamebaini kauli zenye vitisho, vikwazo na vitendo vya viongozi vinavyotia hofu wananchi.

Akisoma tamko lililosainiwa na Jukwaa la Katiba na Baraza la Katiba Zanzibar, Kibamba alisema wameshtushwa na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa mwezi uliopita.

Alifafanua kuwa hotuba ya Rais ya Aprili 13, wakati wa kuwaapisha wajumbe wa Tume ya Katiba, alisema:
 "Huu siyo mchakato wa kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni katiba ya nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo siyo referendum of the union.

“Huu ni mchakato kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za muungano wetu. Kama una mawazo toa, sema jamani mimi nadhani hivi tunavyokwenda siyo sawa. Tukifanya hivi, tunavyokwenda siyo sawa.

tukifanya hivi, tukifanya vile kwenye hili kwenye lile Muungano wetu tutauimarisha na utakuwa mzuri zaidi”.

Kibamba alisema uchambuzi wa  wa  kauli hiyo unaonyesha kuwa, Watanzania wamepangiwa nini cha kufanya na nini wasikisema wakati wa kutoa maoni.

"Jukwaa tunasema, hivi sivyo katiba mpya ya demokrasia inavyoandikwa, Watanzania wanatakiwa waachwe watumie busara zao kujadili mambo yote wanayoona wangependa yajadiliwe kutokana na uzoefu wao." alisema.

Kauli ya pili iliyotolewa kwa mujibu wa Kibamba  ni ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani,  aliyeleza kuwa, wananchi hawapaswi kujadili Muungano.

Kibamba alisema  wanaamini kuwa, katiba bora inatokana na wananchi na itapatikana kupitia  mijadala huru na wazi yenye ushiriki mpana wa umma bila shinikizo, ubaguzi, vitisho au vipingamizi.

Kauli ya tatu aliyoinukuu na kudai ilishtua jukwaa hilo ni  ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, aliyekaririwa akisema, tume yake haitataka mashinikizo katika ufanyaji kazi wake.

 "Kauli hii ingawa inaweza kuwa ilitolewa kwa dhamira nzuri, imetafsiriwa na wananchi wengi kuwa tume itapenda iachwe, iandike katiba ya Watanzania bila kusukumwa na  yeyote, ukweli ni kwamba hakuna muafaka unaweza kujengwa bila msukumo wa wananchi," alisema Kibamba.

Aliongeza kuwa, mwana- tume yeyote ambaye hatataka mashinikizo jukwaa linamtaka ajiengue kwenye kwa sababu mashinikizo ni lazima.

Mratibu wa asasi ya HakiElimu, Robert Mihayo, aliunga mkono na kutaka , kauli iliyotolewa na Jaji Mstaafu Warioba, ifafanuliwe.

Jukwaa liliendelea kuchambua kauli nyingine za kushtua ikiwemo hotuba ya Rais wa Zanzibar,Dk. Ali Mohamed Shein, yenye  ujumbe kuwa wanaotaka fujo waondoke Zanzibar.

Kibamba alisema kauli ya Rais Shein  ya Jumanne wiki hii akiwa Koani visiwani  Unguja iliongeza kuwa , Wazanzibar wasubiri maelekezo ya tume na wasiendelee na mijadala kuhusu katiba.

Alisema kauli ya Rais huyo imeshindwa kutofautisha mijadala ya wananchi kuhusu Muungano na uvunjifu wa amani.

"Sisi tunaamini kwamba mijadala ya amani kuhusu Muungano siyo lazima imaanishe kuvunja amani wala sheria, tunaamini inawezekana kabisa kujadili Muungano bila kuvunja amani ya nchi," alisema.

Aliitaja  kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd  ya kupiga marufuku mihadhara na makongamano yakuhusu katiba iliyorudiwa na Waziri katika Ofisi ya Rais,  Mohammed Aboud kuwa nazo zimelisikitisha jukwaa.

Alisema katazo hilo limefanana na lile alilolitoa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi aliyepiga  marufuku mihadhara ya wananchi kuhusu katiba.

Kibamba alisema wananchi wa Machomanne walizuiliwa na polisi kukatana na kujadili masuala ya katiba, jambo linalochukuliwa na jukwaa kama  mwendelezo wa vitisho kwa  wananchi.

"Tumefadhaishwa na kitendo cha vitisho vya vyombo vya dola dhidi ya wale wote wenye mawazo tofauti kuhusu kuwepo kwa Muungano au aina ya Muungano unaohitajika," alisema na kuongeza:

"Pia kitendo cha kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wananchi 12 waliokuwa wakifurahia haki yao ya kikatiba kuhusu uhuru wa mawazo/ maoni kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania  ya  1977 kama ilivyorekebishwa, " alisema.

Aliongeza kuwa, kukamatwa kwa watu hao ni ukiukwaji wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa  na kuweka bayana kupitia Ibara ya 18 (1) na (2), ibara ya 19 (1) na ile ya 20 (1).

Aidha, kutokana na matukio hayo, jukwaa hilo limetoa tahadhari kwa viongozi pamoja na vyombo vya dola na kuwataka waache kuweka mazuio na makatazo kwa mijadala huru na ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika mchakato huo wa katiba.

Kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya mwaka 2011, Kibamba alisema endapo itaachwa bila kurekebishwa, itawanyima na kuwabana wananchi wasitoe mawazo yao kwa uhuru na kupunguza ushiriki.

Alisema jukwaa hilo pamoja na Baraza la Katiba Zanzibar linapendekeza vipengele vya sheria hiyo virekebishwe au kufutwa kabisa.

Alivitaja kuwa ni cha 18 (6), 20 (2), 21 (1)- (4) ambavyo jukwaa hilo limesema Tume ya Katiba haiwezi kuendelea na kazi ya kukusanya maoni kabla ya kurekebishwa kwa sheria hiyo.

"Kutokuwepo kwa mkutano mkuu wa katiba na kuwa na Bunge Maalum la Katiba linaloshirikisha wabunge wa sasa wa Jamuhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni upungufu katika upatikanaji wa katiba mpya," alibainisha.

Pia alisema tume hiyo ni lazima itambue mchango wa wanahabari katika mchakato mzima wa uundaji wa katiba mpya na kuhakikisha makosa ya kuwasahau hayajirudiia tena.

Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff kwa upande wake, alisema ikiwa viongozi hawataki kujadili Muungano, wanaona hakuna haja ya kuwa na katiba mpya.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Raia ya Kufuatilia Utendaji wa Bunge (CPW), Marcossy Albanie, alisema serikali haina nia ya dhati ya kuwa na katiba mpya.

Marcossy ambaye pia ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya Siasa, Jamii na Utawala alisema kuendelea na mchakato huo bila kubadili vipengele vya sheria hiyo ni kuzalisha katiba isiyokidhi matakwa ya wananchi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles