


.jpg)
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Sengerema, Mkoani Mwanza, imemtunuku hati maalumu ya shukrani, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja.
Aidha, Chama cha Mapinduzi Wilayani humo kinaandaa mapokezi makubwa pamoja na maandano ya kumpokea Ngeleja atakapokwenda jimboni humo hivi karibuni, ikiwani siku cahche baada ya kuachwa katika Baraza la Mawaziri lililotangazwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Hati hiyo ilikabidhiwa kwa Katibu wa Mbunge huyo, Peter Ngelela kwa niaba ya Ngeleja ambaye ni Mbunge wa Sengerema, jana wakati wa kikao cha wajumbe wa halmashauri kuu ya chama wilaya.
Akizungumza kabla ya kuikabidhi hati hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Magdalena Ndwete, alisema Ngeleja amekuwa mstari wa mbele kukisaidia chama (CCM) na jumuia zake zote tangu achaguliwe kuwa mbunge jimbo jilo mwaka 2005.
"Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi wilaya inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa hali na mali wa Mheshimiwa Wiliam Mganga Ngeleja kusaidia chama na jumuia zake tangu achagulilwe kuwa Mbunge wa Jimbo la Sengerema" alisema Ndwete na kuongeza kwamba:
"Amekuwa mstari wa mbele kusaidia Chama cha Mapinduzi na jumuia zake pindi anapopewa taarifa ya kufanya hivyo".
Aliyataja baadhi ya mambo yaliyofanywa na Ngeleja wilayani humu kuwa ni, kuiwezesha CCM na jumuia zake kufanya ziara katika kata zote pamoja na matawi yote kuimarisha chama tangu alipochaguliwa kuwa mbunge.
Katibu huyo aliyataja mambo mengine yaliyofanywa na Ngeleja kwamba ni utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika jimbo la Sengerema; hali ambayo imekisaidia chama hicho kuendelea kupendwa na wananchi pamoja na kuendelea kuwa na imani nacho.
Alisema Ngeleja pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba CCM na jumuia zake wilayani humo hakikwami katika kuendesha shughuli zake za kila siku.
Mbali na Katibu huyo, baadhi ya wana-CCM walijitokeza kuunga mkono uamuzi wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Sengerema kwa uamuzi huo wa kumtunuku Ngeleja, kwani pia amesababisha Jimbo la Buchosa kupata nishati ya umeme.
Wakati huohuo, Ngelela, alisema ofisi yake inaandaa mapokezi makubwa ya kumpokea Ngeleja ambaye anatarajiwa kuwa jimboni humo siku yoyote mwezi huu.
Alisema ofisi yake imeshaanza mchakato kwa ajili ya kufanikisha maandamano hayo, ambayo alisema yatakuwa ya kihistoria wilayani humo.