


.jpg)
Serikali imewaagiza makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kuwachukulia hatua wale wote waliotajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serakali (CAG) pamoja na kamati za kudumu za Bunge na kuonya kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo watajumuishwa katika kundi hilo.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alipokuwa akifungua kikao cha makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wa fedha wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT).
Kikao hicho cha siku tatu kinalenga kujadili matokeo ya ukaguzi wa CAG kwa mwaka 2009/2010.
“Wahusika wote waliosababisha kuwepo kwa hoja wachukuliwe hatua stahiki kutokana na asili ya makosa waliyoyatenda. Yale ya jinai yafikishwe kwenye vyombo vya dola kwa haraka na yale ya nidhamu yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na mamlaka husika ya nidhamu,”alisema Waziri Ghasia.
Ghasia alitaka taarifa za ukaguzi kupitiwa na kufanyiwa tathmini na masuala yaliyojitokeza yafanyiwe kazi katika muda mahsusi kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria na Kanuni za Utendaji.
Alisema taarifa za CAG na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinaonyesha kuwa hakuna mfumo wa udhibiti madhubuti wa ndani kuhakikisha uendeshaji wa halmashauri unaelekezwa katika kuleta tija na kupunguza hasara zisizo za lazima.
Alitoa mfano wa zabuni za ujenzi kupewa kampuni zisizokuwa na uwezo kwa misingi ya kujuana au kwenye mazingira yanayoashiria vitendo vya rushwa.
“Taarifa zinazotolewa na halmashauri siyo tu hazikidhi viwango vya kimataifa vya uhasibu, bali hazitoi habari muhimu kwa wananchi ambazo zingewezesha kuelewa juhudi za serikali katika kuwaondolea kero zao,” alisema.
Waziri Ghasia aliyekuwa ameongozana na Naibu Waziri wake, Kassimu Majaliwa, ambaye anashughulikia Elimu.
Ghasia aliwataka viongozi wa ngazi zote kuweka katika mbao za matangazo fedha zote zinazoingia katika ngazi husika ili wananchi waweze kujua na kuhoji juu ya matumizi yake.