Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Hukumu ya Mnyika leo

24th May 2012
Print
Comments
  Mashahidi wa Mnyika walikuwa sita
  Ngh’umbi watatu
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka 2010.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho katika jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ngh’umbi.

Hukumu hiyo itasomwa na Jaji Upendo Msuya aliyesikiliza kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kupeleka mashahidi watatu na upande wa utetezi mashahidi sita.

Katika ushahidi wake, Ngh’umbi alidai kuwa katika fomu ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kuna idadi ya kura hewa 14,854 ambazo zilipatikana baada ya ukiukwaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutumia laptop za Mnyika na kumpa ushindi isivyo halali.

Kadhalika, alidai kuwa NEC haikuhakiki laptop hizo ambazo zilitolewa na Mnyika wakati akiwa mgombea, hivyo kusababisha madhara na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.

Pia alidai kuwa katika mkutano kipindi cha kampeni za uchaguzi huo, Mnyika alimkashifu kwa kumuita fisadi.

Wakati akitoa ushahidi wake, Ngh’umbi aliongozwa na wakili wa upande wa mashtaka, Issa Maige, na kudai kuwa baada ya kura kuhesabiwa na kujazwa fomu ya matokeo ya jimbo hilo aligoma kusaini baada ya kubaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na kura zilichakachuliwa.

Shahidi wa pili ambaye alikuwa wakala, Robert Kondela (54), alidai kuwa alimsikia Mnyika katika mkutano wa kampeni eneo la Ubungo Riverside akiwaambia wananchi kwamba wasimchague Ngh’umbi kwa sababu ni fisadi ambaye aliuza jengo la Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT).

Kondela alidai pia kuwa Mnyika aliwahutubia watu kati ya 500 na 600 ambao waliathiri ushindi wa Ngh’umbi.

Shahidi wa tatu ambaye alikuwa wakala wa CCM, Andrew Kishatu (46), alidai mahakamani kuwa Mnyika aliingia na wafuasi wake zaidi ya wanane katika chumba cha majumuisho ya kura kinyume cha taratibu.

Aidha, alidai kuwa wafuasi hao ambao ni viongozi wa Chadema walimshinikiza msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kutumia laptop za mbunge huyo kinyume cha taratibu.

Naye shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi ambaye alikuwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi jimbo hilo, Gaudensi Kiriyarara (48), aliiambia Mahakama kuwa kama wangebaini mapema dosari ya kura hewa zaidi ya 14,000 wasingesaini na kutangaza matokeo yaliyomtangaza Mnyika kuwa mshindi wa kiti cha ubunge.

Hata hivyo, Kiriyarara alidai kuwa hawakutumia laptop za Mnyika ila walitumia za Manispaa ya Kinondoni.

Mnyika ambaye alikuwa shahidi wa pili, alidai mahakamani kuwa shahidi wa kwanza upande wa serikali hakuieleza ukweli Mahakama kuhusu laptop zake nne kuwapo katika chumba cha majumuisho ya kura.

“Mheshimiwa Jaji, maelezo ya shahidi wa kwanza aliyoyatoa mahakamani hapa hayakuwa ya kweli,” alidai Mnyika alipohojiwa kuhusu maelezo ya shahidi ya kwanza kama yalikuwa ya uongo kuhusu kuingiza laptop zake katika chumba cha majumuisho.

Alidai kuwa sheria ya uchaguzi haitambui kwamba laptop ni kifaa kitakachotumika kufanya majumuisho ya kura.

Mnyika alidai kabla ya kuongeza laptop nne, mawakala wa Chadema walikuwa na laptop moja waliyotumia kufanya mahesabu ya kura za chama chao.

Katika hoja za majumuisho mahakamani hapo, Wakili wa mlalamikaji, Issa Maige, alidai kuwa walalamikiwa katika kesi hiyo walikiuka taratibu na sheria hivyo, ubunge wa Mnyika siyo halali na kuiomba mahakama iutengue.

Katika kesi hiyo, Mnyika alitetewa na Wakili Edson Mbogoro.

Hadi sasa Mahakama Kuu imekwisha kutengua matokeo ya uchaguzi katika majimbo mawili, ambayo ni Arusha Mjini lililokuwa linaongozwa na Godbless Lema wa Chadema na Sumbawanga Mjini, lililokuwa likiongozwa Hilary Aeshy wa CCM.

Majimbo mengine ambayo kesi zimeisha na wabunge wao kushinda ni pamoja na Segerea, Kasulu Vijijini, Muhambwe, Meatu, Biharamulo Magharibi, Singida Mashariki, Ilemela, Nyamagana na Kilwa Kusini.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles