Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Boban, Cholo waachwa Stars

1st June 2012
Print
Comments
Haruna Moshi 'Boban'

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) iliondoka nchini jana asubuhi na kuelekea jijini Abdijan, Ivory Coast bila ya kiungo wake, Haruna Moshi 'Boban' na beki, Nassor Masoud 'Cholo' ambao walipata majeruhi katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika juzi jioni jijini Dar es Salaam.

Boban ameachwa kutokana na kuchanika nyama za paja wakati Cholo aliumia goti.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah, alithibitisha wachezaji hao kuwa hawajaondoka kutokana na kugundulika ni wagonjwa.

Osiah alisema kuwa baada ya kumalizika kwa mazoezi juzi, wachezaji wote walifanyiwa uchunguzi wa afya zao ndipo ilipogundulika nyota hao kuwa ni wagonjwa hivyo wanahitaji matibabu waweze kuwa fiti na kukabiliana na ushindani.

Timu hiyo ilisota kwa saa tano kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya baada ya ndege yao kubadilishwa na hivyo kutarajiwa kuwasili nchini Ivory Coast saa tatu usiku badala ya mchana kama ilivyotarajiwa.

Kocha wa Stars, Kim Poulsen, alisema kuwa kuchelewa huko hakutaiathiri timu yake kwa sababu wameshafanya mazoezi kwa wiki mbili.

Kikosi hicho cha Kim sasa kimekuwa na majeruhi wanne ambapo wengine walioachwa ni mshambuliaji, Thomas Ulimwengu na kiungo, Nurdin Bakari.

Stars inatarajia kushuka dimbani kesho usiku kuikabili Ivory Coast katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini Brazil.

Baada ya mchezo huo, Stars itarejea nchini Jumanne Juni 5 na kuanza maandalizi ya kuikabili Gambia ambayo wataikaribisha nchini Juni 10 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, alisema kuwa wamejiandaa vyema na lengo lao ni kupata matokeo mazuri katika mechi zote watakazocheza.

Ngassa alisema kuwa wachezaji wengi walioitwa kwenye kikosi hicho wameandaliwa kujiamini na watashuka dimbani wakifahamu kuwa Watanzania wanasubiri furaha.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment