Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Madereva teksi waanzisha chuo

2nd June 2012
Print
Comments
  Ni wizi wa nembo yao iliyoghushiwa na halmashauri 3 za mkoa wa DSM
Madereva wa Teksi

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imeingia katika mgogoro mkubwa na Chama cha Madereva wa Teksi cha Tunawajali Group (TG) kwa madai ya kuwatapeli zaidi ya shilingi bilioni moja.

Kutokana na madai hayo ya Tunawajali, serikali hiyo itaburuzwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE Jumamosi, umebaini kuwa madai hayo yametokana na Halmashauri za manispaa zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke kughushi na kuitumia nembo ya teksi (mchoro wa utambuzi wa teksi) ambayo ni mali ya TG na kujipatia fedha hizo.

Nembo hiyo ambayo ina hatimiliki ya TG, hulipiwa Sh. 10,000 kwa kila teksi kwa mwaka, hivyo katika kipindi cha takribani mitatu, manispaa hizo zimekuwa zikichukua fedha hizo bila mawasiliano yoyote na TG.

Akithibitisha hali hiyo, Mwenyekiti Mtendaji Taifa wa TG, Abeid Chembe, alisema kuwa wamekuwa wakiishi kwa matumaini kusubiri labda halmashauri hizo zitatoa ufafanuzi ni kwa nini wanatumia nembo hiyo kujipatia kipato bila idhini yao kwa miaka mitatu mfululizo.

“Kama unavyotuona tuna mipango mingi lakini haitekelezeki kutokana na ukosefu wa fedha, tumebuni nembo hii na kuisajili na kuimiliki kisheria, lakini wenzetu wakatuona mazuzu wanaitumia na kukusanya fedha kutoka kwa wanachama wetu bila wasiwasi,” alilalamika Chembe.

Alitoa mchanganuo wa madai hayo kuwa manispaa ya Kinondoni yenye jumla ya taxi 11,000, wanaidai Sh. milioni 330, Ilala yenye taxi 13,000 inadaiwa Sh. milioni 390 na Temeke yanye taxi 10,000 inadaiwa Sh. milioni 300, hivyo kufanya jumla ya deni kuwa Sh. bilioni 1,020.

“Tumejaribu kuomba usuluhishi kwa Mkuu wa Mkoa bila mafanikio, hivyo tumewasiliana na wanasheria wetu, tunachosubiri ni taratibu za kiufundi ili tuwafikishe mahakamani,” alisema.

Katika kutafuta ufumbuzi huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika barua yake ya Desemba 31, 2010 iliyoandikwa na Katibu Tawala wa mkoa, Mtambo Mhina (nakala tunayo), ilimshauri Chembe kuwasiliana na wakurugenzi wa manispaa hizo.

“Napenda kukujulisha kuwa kila Manispaa ni mamlaka kamili inayotambuliwa kwa mujibu wa sheria. Pia suala la usajili wa Taxi katika kila manispaa linafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Hivyo endapo kuna suala lolote ambalo ungependa kupata ufafanuzi, maelezo au msaada, unashauriwa kuwasiliana na mkurugenzi wa manispaa husika…hakuna sababu ya kuomba mkoani,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Katika barua yake aliyowaandikia wakurugenzi wa manispaa (nakala tunayo) ya Juni 2, 2011, Chembe aliwaarifu kuwa kibali cha stika hizo kinatolewa na TG makao makuu Temeke na hakuna wakala, hivyo tax zitakazo kwenda kinyume zitakamatwa na kuchukuliwa hatua kama zimetumia stika tofauti.

Tunawajali hawakuishia hapo, waliwasiliana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kulalamikia kutapeliwa nembo yao, ambapo Mkuu wa Upelelezi katika barua yake ya Novemba 7, 2011 iliyoandikwa kwa niaba yake na ACP H.Mhakka,  TG walishauriwa kufungua kesi ya madai.

“Baada ya kukamilisha uchunguzi wa shauri, tumebaini kwamba malalamiko hayo yana muelekeo wa kimadai zaidi. Hivyo basi, ofisi hii inawashauri Tunawajali Group kufungua shauri la madai kwa mujibu wa mahusiano katika sheria za hati miliki kwa ajili ya kulipwa fidia,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ya polisi ambayo nakala tunayo.

Kwa upande wao, kampuni ya uwakili ya M/S Nassoro & Co. Advocates iliyoteuliwa na Tunawajali, iliziandikia halmashauri hizo kueleza nia yao ya kuwashitaki mahakamani ili kulipa deni hilo.

Kwa mujibu wa moja ya barua ya kampuni hiyo ya uwakili kwa manispaa ya Ilala, kitendo cha kutumia alama hiyo ni kosa kisheria na TG wanahaki ya kudai fidia na nafuu nyingine kama ambavyo itaona inafaa kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa alama za biashara na huduma.

“Hivyo basi, kwa barua hii tunaitaka Manispaa yako imlipe mteja wetu Sh. 390,000,000 pamoja na Sh. 1,000,000 ikiwa ni gharama ya barua hii. Endapo utaona kuna haja ya kuzungumza katika hili, milango iko wazi, vinginevyo hatutakuwa na njia nyingine ila kuwasilisha madai mahakamani dhidi ya manispaa,” ilieleza sehemu ya barua ya mawakili hao.

Katika kuzima jitihada hizo za Tunawajali, Manispaa ya Ilala imewaandikia barua wanachama wa TG waliopo kwenye vituo vyao vya Taxi ikiwataka kufanya uchaguzi haraka na kupata viongozi ambao ni Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina.

Barua hiyo iliyoandikwa na Ofisa Biashara wa Manispaa ya Ilala, M.R.B. Mayila ilikuwa ikikumbushia kikao cha Aprili 12, 2012 kilichohudhuriwa na maofisa biashara, Takukuru mkoa na wilaya, madereva taxi, wamiliki wa taxi na Tunawajali ambako moja ya maazimio ni kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi kwenye vituo vya taxi.

Chembe alimshangaa Mayika kwa kutoa maelekezo ya kufanyika kwa uchaguzi huo akidai kuwa si jukumu lake kwani hilo liko chini ya Tunawajali.

“Sijui nia yake hasa ilikuwa nini, ni yale yale masuala ya rushwa, wanataka kuwatambua viongozi ili wawakamate na kuendelea kuwanyonya bila wenyewe kujua.

Ofisa biashara huyo aliwaagiza madereva hao baada ya uchaguzi wawasilishe majina ya viongozi waliochaguliwa pamoja na picha na muhtasari wa kikao ili watambulike kuwa wasimamizi wakuu katika vituo vyao na wanatakiwa kufanya hivyo kabla ya Mei 15, 2012 ili kujiandaa kwa usajili wa Julai 2012/2013.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment