


.jpg)
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, amezindua mradi wa kuhifadhi maji katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 60 na kutoa wito kwa uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha kuwa mradi huo unatunzwa ili kuufanya uwe endelevu.
Mradi huo ambao umefadhiliwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), una uwezo wa kuhifadhi lita 40,000 za maji na unatarajiwa kutosheleza mahitaji ya watu 150,000 kwa sasa.
Akizungumza na mamia wa wakazi wa Manispaa ya Moshi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo jana hospitalini hapo, Mama Pinda alisema anatambua changamoto inayoikabili hospitali hiyo ambayo mahitaji yake ya maji kwa siku ni lita 200,000.
Aliishukuru kampuni ya SBL kwa ufadhili wake na kutumia fursa hiyo kuwaomba wadau wengine ambao wanapenda maendeleo na wanaguswa na tatizo la maji katika hospitali hiyo kujitokeza na kuchangia ujenzi wa matenki ya ziada.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mtumwa Mwako, alisema upatikanaji wa maji katika hospitali hiyo haukuwa mzuri kwa sababu ya ukame na ongezeko la idadi ya wakazi katika Manispaa ya Moshi.
Alisema mahitaji ya maji kwa siku ni lita 200,000 ambazo ni sawa na lita milioni sita kwa mwezi ambayo kwa mwaka yanafikia lita milioni 72.
Pia aliishukuru kampuni ya SBL kwa ufadhili wake na kuiomba iwasaidie kukarabati chumba cha upasuaji mdogo.
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda, alisema kampuni imejikita kusaidia maeneo manne ambayo ni maji, uhifadhi wa mazingira, elimu na afya.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliahidi kuhakikisha kuwa mradi huo unatunzwa ili uendelee kuwasadia mamia ya wakazi wanaofika kwenye hospitali hiyo.