Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tanzania yalala, Uganda yafutwa netiboli Afrika

10th May 2012
Print
Comments
Timu ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens

Wakati timu ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, jana ilikumbana na kipigo cha kwanza kwenye michuano ya ubingwa wa mchezo huo Afrika baada ya kulala kwa magoli 34-30 mikononi mwa Malawi, timu ya Uganda imefutwa katika michuano hiyo kutokana na serikali ya nchi yao kuuvua madaraka uongozi wa chama cha mchezo huo  cha Uganda.

Timu ya Uganda ambayo tayari iliwasili nchini kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ambapo jana asubuhi ilitarajiwa kucheza dhidi ya Botswana, iliambiwa kabla ya mechi hiyo kwamba imeondolewa mashindanoni baada ya Baraza la Michezo la Uganda kuutoa uongozi wa chama cha mchezo huo cha Uganda na kuwaweka viongozi wapya, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya chama cha netiboli cha Uganda na kanuni za uongozi wa vyama vya michezo vilivyo wanachama wa shirikisho la mchezo huo duniani (IFNA).

Kanuni hizo zinataka vyama na timu za netiboli kuongozwa na wanachama na sio kuchaguliwa na chombo kingine.

Kwa mujibu wa barua ya Shirikisho la Netiboli Afrika (Africa Netball) iliyosainiwa na rais wake, Tebogo Lebotse, Uganda imepoteza sifa ya kushiriki mashindano yote yanayoandaliwa na shirikisho la mchezo huo Afrika na dunia (IFNA).

Katika mechi za jana, Tanzania ambayo ilianza michuano hiyo kwa ushindi wa gharika wa 57-13 dhidi ya Lesotho juzi, ililala kwa tofauti ya magoli manne dhidi ya timu kali ya Malawi inayoshika Na.5 kwa ubora duniani, katika mechi ngumu iliyocheza Alasiri.

Asubuhi jana, Zimbabwe iliwafunga vibonde Lesotho magoli 37-16, wakati Malawi iliifunga Zambia 56-33.
Katibu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Rose Mkisi alisema Taifa Queens ilijitahidi sana licha ya kipigo hicho kwani Malawi ni miamba wa mchezo huo barani Afrika na pia wanashika Na.5 kwa ubora duniani.

Alisema Queens walionyesha kiwango cha juu na wangeweza kushinda mechi hiyo lakini wafungaji walipoteza mipira mingi. Wafungaji katika mechi ya jana walikuwa ni Mwanamichezo Bora wa TASWA wa mwaka jana ambaye juzi alikuwa nyota wa mchezo kwa kufunga magoli 38, na Pili Peter.

Michuano hiyo inayoendeshwa kwa mchezo wa ligi ikihusisha mataifa sita, itaendelea tena leo asubuhi ambapo wenyeji Tanzania watawakabili Zambia, Zimbabwe itacheza na Botswana, wakati mchana vibonde Lesotho watawakabili Zambia na Malawi itacheza dhidi ya Zimbabwe. 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles