Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Huyu ndio Patrick Mafisango

18th May 2012
Print
Comments
Aliyekuwa kiungo wa kimataifa wa Simba kutoka nchini Rwanda, Patrick Mafisango

Mwili wa kiungo wa kimataifa wa Simba kutoka nchini Rwanda, Patrick Mafisango (32) aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana unatarajiwa kuagwa leo kuanzia saa 2:00 asubuhi kwenye viwanja vya Sigara (TCC) Chang'ombe hapa jijini Dar es Salaam.

Mafisango ambaye asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alifariki dunia kutokana na ajali ya gari iliyotokea kwenye eneo la Keko (Mtaa wa Mbozi) ambapo alifariki hapo hapo baada ya gari dogo aina ya Toyota Cresta (GX 100) alilokuwa akiliendesha kutumbukia kwenye mtaro kutokana na juhudi za kukwepa guta lililokuwa mbele yake. Alikuwa akitokea katika klabu ya Maisha majira ya saa tisa usiku.

Akizungumza jana jijini, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Ngange 'Kaburu' alisema kuwa mwili wa kiungo huyo utaagwa katika eneo hilo na baada ya hapo utapelekwa kwenye uwanja wa ndege tayari kwa maandalizi ya kuelekea kwao Kinshasa kesho asubuhi kwa ajili ya mazishi ambayo yanatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili.

Kaburu alisema kuwa maandalizi ya safari hiyo jana yalikuwa katika hatua za mwisho ambapo viongozi wa klabu hiyo ya Simba walikuwa wakiyafanya baada ya kupata maelekezo kutoka kwa familia ya marehemu mchezaji huyo iliyoko mjini Kinshasa.

"Mwili utasafirishwa na ndege ya KQ ambapo kwa upande wa Simba msafara utaongozwa na Mzee Kinesi (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji) na mchezaji mmoja ambaye bado hajateuliwa," Kaburu aliongeza.

Alisema kuwa wanawaomba wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kujitokeza kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Mafisango ambapo alimueleza alikuwa ni mchezaji mwenye uzoefu wa kukabiliana na ushindani ndani ya uwanja.

"Siwezi kusema mengi kuhusiana na kifo hiki, tumepata pigo Wana-Simba, ni pengo kwa sababu tayari alikuwa kwenye mipango ya kumsajili katika msimu ujao wa ligi," alisema Kaburu.

Mafisango alitarajiwa kusaini mkataba mpya na Simba jana taarifa za kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango ambaye alijiunga na Simba akitokea Azam ya jijini Dar es Salaam.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa msiba huo ni mkubwa kwa familia ya soka kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.

Wambura alisema kuwa kifo cha mchezaji huyo ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani.

Wakati mauti unamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa katika kikosi cha Amavubi kwa ajili ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi ujao.

TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisema jana kuwa kuondokewa na mchezaji huyo ni pengo kwa ukanda huo kwa sababu uwezo wao bado ulikuwa uko juu.

Musonye alisema hilo linajidhihirisha kutokana na kuwepo katika kikosi cha kwanza cha Simba kwa muda mrefu na kurejea kwenye timu ya Amavubi.

"Nilianza kumuona akiwa kijana mdogo lakini akicheza kwa bidii, uwezo wake ndio ulisababisha Rwanda kumchukua na hakuwa akibahatisha," alieleza Musonye.

Nacho chama kisiasa cha wananchi (CUF) kilielezea kuhuzunishwa sana na kifo cha mchezaji huyo.

Taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uenezi Taifa wa chama hicho, Abdul Kambaya, ilisema CUF imekuwa ikimtambua Mafisango kama miongoni mwa wachezaji nchini walioipatia heshima kubwa Tanzania kupitia uchezaji wake mahiri, wa kujituma na umaridadi mkubwa kupitia timu mbalimbali alizowahi kuchezea nchini hasa timu yake ya mwisho Simba.

"CUF inatoa salamu za rambirambi kwa wapenzi wote wa marehemu Patrick Mafisango, viongozi na wapenzi wa timu ya Simba.

Tunaamini hili ni pengo kwa timu ya Simba na simanzi kubwa kwa ndugu jamaa na marafiki wa Patrick Mafisango lakini wote wanapaswa kujipa moyo wakati huu wa majonzi," ilisema taarifa hiyo.

TIMU ALIZOWAHI KUCHEZA
Marehemu Mafisango ambaye alizaliwa mwaka 1980 katika mji wa Goma huko DRC zamani Zaire alianza kung'aa akiwa na TP Mazembe na hapo ndipo aliposajiliwa na APR ya Rwanda.

Azam kupitia meneja wake, Patrick Kahemele, aliridhishwa na kiwango cha marehemu ambapo alipendekeza asajiliwe na klabu hiyo jambo ambalo lilifanikiwa lakini aliweza kuichezea timu hiyo kwa msimu mmoja wa 2010/ 2011.

Simba ilimchukua na kumpa mkataba wa mwaka mmoja uliomalizika mapema mwaka huu na mafanikio yake katika kuchukua ubingwa wa msimu huu wa mwaka 2011/ 2012 yamechangiwa na kiungo huyo mwenye asili ya Kongo.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, aliliambia gazeti hili kwamba jana ilikuwa wamsainishe mkataba mpya wa miaka miwili kabla ya kuanza safari ya kuelekea Kigali kujiunga na timu yake ya taifa.

KIGALI, KINSHASA WAMLILIA
Mashabiki wa mchezaji huyo walioko Kigali na Kinshasa wamekaa katika makundi mbalimbali wakisikitika kumpoteza nyota huyo ambaye alikuwa ni maarufu kwa jina la Petit.

Akizungumza na NIPASHE, mwandishi mwandamizi wa gazeti la New Times la Rwanda, Bonnie Mugabe, alisema kuwa mashabiki wa soka wa mchezaji huyo jijini Kigali wameandika mabango mbalimbali ya kumbukumba marehemu Mafisango.

Bonnie alisema kuwa wengi wao bado hawaamini kilichotokea na wamekuwa wakiendelea kuwasiliana na watu wanaowafahamu wanaoishi Dar es Salaam na miji ya jirani.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' aliyeko Kinshasa akiichezea DC Motema Pembe, alisema kuwa mashabiki wa soka wa jijini hapo wamepokea kwa majonzi taarifa za msiba huo.

Mgosi alisema kuwa katika kuomboleza msiba huo wameenda kuungana na familia yake ili kusubiri mwili utakapowasili waweze kumzika ndugu yao.

Mafisango alifunga goli la tano wakati Simba ikitoa kipigo cha aibu cha 5-0 kwa watani zao Yanga katika mchezo wa funga dimba wa Ligi Kuu ya Bara.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi, Amina.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles