Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kafulila amng`ang`ania Badwel

4th June 2012
Print
Comments
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),David Kafulila

Sakata la kukamatwa kwa Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh. milioni 1, limechukua sura mpya, baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kutaka kashfa hiyo ishughulikiwe kibunge ili kama mbunge huyo atapatikana na hatia, avuliwe ubunge kwa kosa la kudhalilisha hadhi na heshima ya Bunge.

Pia amemtaka Spika wa Bunge kuivunja Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kuisuka upya kwa kuwa imepoteza uhalali wa kuendelea kusimamia, kukagua na kudhibiti hesabu za serikali kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili mbunge huyo, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.

Kafulila alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mbunge huyo kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Alisema Bunge linayo mamlaka ya kumvua ubunge mbunge yeyote kwa azimio la Bunge, hivyo akasema ataiomba Kamati ya Bunge ya Maadili, ambaye yeye (Kafulila) ni mjumbe wake, kushughulikia suala hilo kibunge.

Kafulila alisema ombi hilo linalenga kuhakikisha wabunge wanakwenda na azimio katika Mkutano ujao wa Bunge ili hatua stahiki, ikiwamo kuvuliwa ubunge zichukuliwe kulinda heshima
ya Bunge na mtuhumiwa aendelee kuchukuliwa hatua za kijinai kama raia wa kawaida.

“Tunataka kufungua ukurasa mpya ili tusijikute Bunge likiwa limejaa wabunge watuhumiwa,” alisema Kafulila.

Alisema hatua ya mbunge kuvuliwa ubunge kwa azimio la Bunge, haitakuwa mpya kwa Tanzania kwani baadhi ya mabunge ya Jumuiya ya Madola, yamekwishawahi kufanya hivyo.

Alitoa mfano kuwa Bunge la Uingereza limekwishawahi kuwavua ubunge wabunge wake mara 59, wakati Bunge la India lilikwishawahi kufanya hivyo mwaka 1979 na mwaka 2005 kwa kufukuza baadhi ya wabunge kwa kuchukua rushwa.

Kafulila alisema mwaka jana, wakati akichangia hoja ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano, alitoa taarifa iliyowahusu wabunge watatu, akiwamo Badwel, Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki-CCM) na Zabein Mhita (Kondoa Kusini-CCM), kuwa wanaomba rushwa kwa watumishi wa serikali.  

“Kwa kuzingatia hoja hiyo, nina wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati hii na kuipanga upya kwa maslahi ya umma, heshima na hadhi ya Bunge letu,” alisema.

Badwel alikamatwa na Takukuru juzi kwa tuhuma za kupokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kutoka kwa kiongozi wa serikali, katika hoteli moja jijini Dar es Salaam.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment