


Ni Aeshy Hillary wa Jimbo la Sumbawanga Mjini
Hatiani kwa rushwa, kuzuiwa miaka mitano
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga imetengua matokeo ya wa ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshy Khalfan Hillary, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uamuzi wa kutengua matokeo hayo ulitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Bethwell Mmilla, ambaye alisikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2010 ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Norbert Yamsebo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika mwaka juzi, ulikuwa na ushindani mkubwa, Aeshi alipata kura 17,328 wakati Yamsebo alipata kura 17,132.
Katika hukumu hiyo yenye kurasa 68 iliyosomwa na Jaji Mmilla kwa saa tatu, alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji hivyo kutengua matokeo hayo kutokana na hoja mbili.
Jaji Mmilla alisema alitengua matokeo hayo kutokana na madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa na vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM wakati wa kampeni. Mlalamikaji alikuwa amewasilisha hoja 21.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi iwapo mtu atapatikana na hatia ya rushwa katika uchaguzi hataruhusiwa kugombea nafasi ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano. Adhabu kama hii ilipata kumpata Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, wakati huo akiwa mbunge wa NCCR wa jimbo la Bunda. Sasa ni mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM.
HOJA ZA KESI
Baadhi ya hoja hizo ni ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi; matokeo ya uchaguzi kupishana katika vituo vitatu vya Kizwite pamoja na vituo viwili vya Kandandala; kupinga Justus Athanas ambaye ni mtendaji wa kata kuwa msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Katandala wakati akiwa ni kada wa CCM; tukio la kucheleweshwa kwa masanduku ya kupigia kura katika kata ya Katandala na msimamizi katika kituo cha Matanga kufungua masanduku ya kura.
Hoja nyingine ni tukio la makada wa CCM kwa kushirikiana na mbunge huyo kushiriki katika ununuzi wa shahada za kupigia kura; kubadilisha wapiga kura katika vituo vya Pito na Mbalika; vurugu zilizosababisha kutofanyika kwa kampeni za Chadema katika vijiji vya Mtimbwa na Kisumba kwa siku tofauti na vitendo vya rushwa kama kugawa vifaa vya michezo pamoja na pombe katika kijiji cha Pito.
Mgombea wa Chadema pia alilalamikia kutolewa kwa rushwa ya mifuko 20 ya saruji na vinywaji katika kijiji cha Katumba; kugawa fedha na vinywaji kwa wapiga kura katika kituo cha mazoezi kilichopo Kandalamba mjini Sumbawanga na kutoa msaada wa fedha kwa Kanisa Katoliki pamoja na msimamizi wa uchaguzi kubadilisha baadhi ya vituo vya kupigia kura kupelekwa mbali zaidi kati ya kilomita tano hadi nane, hivyo kuchangia kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.
FURAHA YATAWALA MAHAKAMANI
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ya kutenguliwa kwa matokeo iliyosomwa kwa lugha ya Kingereza na kulitangaza Jimbo la Sumbawanga Mjini kuwa wazi, wafuasi wa Chadema walilipuka kwa furaha na kuipongeza Mahakama hiyo kwamba imetoa maamuzi ya haki.
Aidha, nje ya Mahakama hiyo zilibuka kelele za shanwge, nderemo na vifijo kutoka kwa wafuasi wa Chadema, hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Rukwa, Laurent Magweshi, kuwatuliza vijana hao ili watoke eneo la Mahakama na kuepuka usumbufu kwa kuwa kesi nyingine zilikuwa zinaendelea.
AESHY: NAWASILIANA NA MAWAKILI
Baada ya hukumu hiyo, aliyekuwa Mbunge Aeshy Khalifan Hillary alisema: “Nimeisikia hukumu na nitawasiliana na mawakili wangu ili kujua ni kipi watakishauri katika kesi hii na kisha nitawajulisha.”
Wakili wa Aeshy, Juma Nassoro, alisema anasubiri maamuzi ya mteja wake.
Aliongeza kuwa hukumu hiyo inakinzana na hoja zilizotolewa mahakamani hapo na kuwa atazungumza na mteja wake ili wakate rufani.
MGOMBEA WA CHADEMA: NAISHUKURU MAHAKAMA
Aliyekuwa mgombea wa Chadema, Norbeth Yamsebo, alisema kuwa ameipokea hukumu hiyo kwa mikono miwili na kuishukuru Mahakama hiyo kwa haki iliyotolewa na kusema kuwa bado anafanya mawasiliano na chama chake ili kujua ni nini kitaendelea.
CHADEMA: TUNALISUBIRI JIMBO
Mkurugenzi wa habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alijigamba kwamba Chadema kinajiandaa kuchukua jimbo hilo.
Alisema jimbo hilo lilikuwa ni haki yao, lakini ikapindishwa na kwamba baada ya hukumu hiyo ya Mahakama, chama kinajiandaa kuingia katika uchaguzi ili kulinyakua.
WAFUASI WA CCM WANYONG’ONYEA
Wafuasi wa CCM pamoja na viongozi wa chama hicho mara baada ya hukumu hiyo walionekana kupigwa na butwaa huku wengine wakibubujikwa na machozi.
NAPE: NI MAPEMA KUSEMA LOLOTE
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa maoni yake baada ya kuhumu hiyo, alisema ilikuwa ni mapema kuzungumza lolote.
Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na msimamizi wa uchaguzi wanaodaiwa kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi.
Katika kesi hiyo, mlalamikaji aliwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Mkumbe & Company ya Mbeya huku upande wa Serikali uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Shahidi.
Aeshy aliwakilishwa na jopo la mawakili watatu wakiongozwa na Ileth Mawalla kutoka S. Mawalla Law Consultant and Attorney.
Kesi zote za kupinga uchaguzi zinatarajiwa kumalizika Mei 4, mwaka huu baada ya kuongezwa muda na Waziri wa Katiba na Sheria, Selina Kombani, kutokana na kutokamilika ndani ya mwaka mmoja tangu uchaguzi kumalizika.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Mohamed Chande, hivi karibuni alisema kesi zote za uchaguzi zitamalizika Mei 4, mwaka huu.
Hiyo ni hukumu ya pili ya kutengua matokeo ya ubunge. Aprili 5, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitengua matokeo ya ubunge Jimbo la Arusha Mjini, baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, kumvua ubunge Godbless Lema (Chadema), baada ya kuridhika kuwa alikiuka maadili ya uchaguzi.