


Chama cha Mapinduzi Kata ya Msigani, Dar es Salaam, kiko hatarini wanachama wake kusambaratika na kujiunga na vyama vya upinzani kutokana na viongozi wa juu wa chama hicho kuingia katika msigano mkubwa.
Msigano huo umeelezwa ni katika mbio za kuelekea chaguzi ndogo za matawi na kata wa chama hicho zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu ambako baadhi ya viongozi akiwemo diwani kuipa kisogo katiba ya chama hicho kwa kusimamia baadhi ya wagombea kwa lengo la kuwainua kwenye chaguzi hizo.
Baadhi ya wanachama wameeleza kusikitishwa na mwelekeo mbaya wa chama hicho huku wengine wakiahidi kukihama hata kabla ya uchaguzi huo kufanyika.
Kutokana na mazingira hayo, mmoja wa viongozi ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Dotto Magai, alilazimika kuvunja ukimya kwa kumuandikia barua Diwani wa Kata ya Msigani, Rogath Mbowe na Katibu wa kata hiyo Hamis Makurumlo kumuelezea hali mbaya ya siasa katika kata hiyo akiwatuhumu kuwa ndiyo chanzo huku nakala ya barua hiyo ikipelekwa kwa Makatibu wote wa Matawi, wenyeviti wa mitaa, kamati ya siasa ya kata, Katibu wa CCM wilaya na Mkoa.
Katika barua hiyo amemtuhumu diwani huyo kuwa amekuwa akipanga safu anayoitaka ya uongozi kwa kila chaguzi na kukiuka misingi na taratibu za uongozi ikiwa ni pamoja na kuipa kisogo katiba ya chama hicho.
Diwani Mbowe anatuhumiwa pia kutokuwa na maelewano na wenyeviti wa mitaa, kuwa na maamuzi yake bila kufuata ya vikao.
“Mnajua (diwani na Katibu) maeneo ya kwa Mama Six wanachama wetu wameenda Chadema, tulisema wote watatu tupange twende huko lakini mpaka leo hakuna kitu…je! Mnakitakia mema chama chetu?
“Kudhihirisha udhaifu huo, Kata kuna maduka yanaingiza fedha nyingi lakini mpaka leo hakuna taarifa yoyote ya mapato au matumizi. Hakuna ubishi nimekuwa nikiwapa taarifa za uhakika lakini hamna lolote, sasa nitawapa kwa maandishi…” alieleza Dotto katika barua yake hiyo ambayo Nipashe inayo nakala yake.
Baadhi ya wenyeviti wa matawi waliungana na kauli za Dotto wakieleza kuwa katika Kata hiyo kumekuwa na udhaifu mkubwa wa uongozi wa Diwani na Katibu wa Kata hiyo.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mbezi Msigani, Amiri Majembe, alisema Diwani huyo haambiliki, kwani amekuwa kikwazo cha maendeleo ya kata hiyo kutokana na kusigana na baadhi ya wenyeviti wa mitaa.
“Unajua huyu diwani wetu bado ni mchanga, hajakomaa kisiasa na kiuongozi, ni mara yake ya kwanza. Haya matatizo yanashughulikiwa na vikao na tumeshakaa Kamati ya Maadili, miongoni mwa mambo tuliyoyajadili ni pamoja na diwani huyu,” alisema Majembe.
Naye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mtaa wa Malambamawili, Saidi Bakari, alisema kutokana na baadhi ya viongozi hasa Diwani wa Kata hiyo kutokuwa na maadili ya uongozi, alishauri semina za mafunzo dhidi yao zifanyike mara kwa mara.
Alisema kumekuwa na maamuzi yanayotolewa kwenye vikao, lakini diwani huyu kwa kukosa maadili ya uongozi, amekuwa akikengeuka maamuzi hayo na kutoa ya kwake kichwani.
Bakari alisema hali hiyo imesababisha kutokuelewana kwa viongozi kadhaa wa CCM katika eneo hilo na hali ya mambo kwenda mrama hali inayotishia ustawi wa chama kwa wanachama kufanya maamuzi ya kukihama.
Hali kadhalika alisema Kamati ya Maadili imekwisha kukaa kujadili suala hilo, na baadaye Kamati ya siasa na Halmashauri Kuu zitakutana kwa nyakati tofauti na maamuzi yatatolewa.
Diwani Mbowe alipoulizwa juu ya tuhuma hizo kwa njia ya simu, alijibu kwa mkato, “hayo ni majungu siwezi kuzungumzia majungu, kwanza niko Arusha,” alisema ingawa baadhi ya wenyeviti wa mitaa ya Msigani walipoulizwa kuhusu kusafiri wa Diwani huyo walisema si kweli kwani siku hiyo alishiriki kwenye moja ya vikao vya CCM.
Kwa upande wake Danny Nkya, anayedaiwa kubebwa na Diwani huyo ili kushinda moja ya chaguzi zinazokuja, mbali na kupigiwa simu yake ya mkononi mara kadhaa bila kupokea, hakujibu hata ujumbe wa maandishi aliotumiwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwa Yussuf, Mariam Wenga, alisema hali ya siasa kuna wakati katika maeneo hayo inakwenda mrama, lakini kutokana na msimamo wa viongozi, masuala hayo hupatiwa ufumbuzi kwenye vikao halali.
Alisema ni kweli Diwani huwa anaweza kusimamia misimamo yake hata kama inaathari kwa jamii, lakini anapopewa ufafanuzi kwenye vikao, huwa ni mwelewa.
Alitoa mfano kuwa hivi karibuni baada ya mafuriko ya mwaka jana, waliwakataza vijana kuchimba mchanga kwenye mto Mbezi kutokana na kuathiri maeneo kadhaa ikiwemo Shule ya Msingi Msigani, lakini Diwani huyo aliwaeleza vijana hao kuendelea na kazi hiyo.
“Nilikutana na diwani nikamuelezea athari zake, alinielewa tukaenda kuwaeleza vijana nao wakatuelewa kwa mbinde, lakini tumefanikiwa. Tofauti zote huwa tunazimaliza kwenye vikao,” alisema.