


.jpg)
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni linawashikilia watu 51 waumini wa Kanisa la Efatha limaloongozwa na Josephat Mwingira kwa tuhuma za kukivamia na kuvunja ukuta wa kiwanda cha uchapaji cha Afro Plus, na kuwazuia Polisi kufanya kazi yao.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Charles Kenyela, alisema usiku wa kuamkia jana, Polisi ilipata taarifa ya kuwepo kwa moto kwenye kiwanda cha Afro Plus, na kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto walifika kwenye eneo la tukio, ambapo walinzi wa Kanisa hilo waliwazuia Polisi pamoja na Zimamoto kuingia ndani ili kuuzima moto huo.
“Jeshi la Polisi lilijaribu kuongea na walinzi hao ili wawaruhusu polisi kuingia ndani ili waweze kuuzima moto huo, lakini walikataa,” alisema.
Kenyela aliongeza kuwa licha ya walinzi hao kuwazuia Polisi kuingia ndani, walipiga risasi mbili hewani ili kuwatishia na baada ya kuona hivyo Polisi wakajipanga na kutumia nguvu na kufanikiwa kuvunja geti na kuingia ndani, ambapo waliwakuta waumini 51 wa kanisa hilo wakivunja ukuta wa kiwanda cha Afro Plus, ambao walikimbilia kanisani baada ya kuwaona Polisi.
Kenyela aliendelea alisema Polisi walikuta moto umekwisha zimika ndipo lilipoamua kuwafuatilia waumini hao na baada ya kuwakuta wamekimbilia kanisani waliwakamata walinzi wawili wa kanisa hilo waliokutwa na bunduki aina ya short gun.
Kamanda Kenyela alieleza kuwa mgogoro kati ya waumini wa kanisa hilo na kiwanja cha Afro Plis ni wa muda mrefu ambapo siku za karibuni waumini wa kanisa hilo walivamia na kuvunja ofisi za kiwanda hicho na kuvunja thamani, na hatua zilikwishachukuliwa na kesi ipo mahakamani. Alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani hivi karibuni.