Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mkapa anapokuwa `mbogo` kuhusu ubinafsishaji!

15th April 2012
Print
Comments
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa

Juzi, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, alihudhuria mazungumzo maalum ya kuhitimisha kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere.

Kwenye meza kuu iliyokuwa ndani ya ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), palipofanyika kongamano hilo, alikuwepo Mkapa, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji na Dk Kamata Mwanza.

Kama ni kutetea ikibidi ‘kulifia’ jambo unaloliamini kuwa ni sahihi, basi inampasa Mkapa katika suala la ubinafsishaji wa viwanda na mashirika ya umma, uliofanyika wakati akiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini.

Mkapa hakuona na bado hajaiona kasoro iwayo yote, kwamba ilitokea kabla na wakati wa ubinafsishaji huo unaozidi kupingwa na kukosolewa na watu wa kada tofauti, wakiwemo wanazuoni.

Kuna mambo mengi yaliyojadiliwa siku ya mwisho ya kongamano hilo, kuna michango iliyotolewa na watu wengi wa rika na kada tofauti, lakini yote hayo yalichagizwa na uwepo wa Mkapa.

Pamoja na kumpongeza, japo sina hakika kama akialikwa kwa mara nyingine ashiriki atakubali ama ‘ratiba itambana’, Mkapa alikuwa mtu muhimu sana katika kongamano na mjadala wenyewe.

Zipo sababu kadhaa zinazothibitisha umuhimu huo; mosi, alikuwa ‘C+++++haguo la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995.

Mwalimu Nyerere akitambua kwamba ni mtu safi (Mr Clean), akahakikisha Mkapa anapata nafasi ya kukiwakilisha chama hicho na kushinda. Ikawa hivyo.

Kwa hali hiyo, Mtanzania aliyesadikiwa kustahili awe wa kwanza kutetea fikra za Mwalimu Nyerere zilizojikita katika kuitazama jamii na matatizo yao ukiwemo umasikini, kisha kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kupata suluhu ya kadhia hizo, ni Mkapa.

Lakini ni Mkapa, akiwa madarakani akatenda kinyume cha matamanio ya Mwalimu Nyerere kwa kushiriki ubinafsishaji ukiwemo wa sekta nyeti kwa uchumi wa nchi, kama bima na benki ambazo (Mwalimu) alipinga kwa nguvu zote.

Hivyo kuibukia kwake katika kongamano la Kigoda cha Mwalimu, kulikuwa na maana pana kwa Mkapa. Ninampongeza.

Wapo wanaoamini kwamba Mkapa aliwekwa ‘kiti moto’, lakini kwa mujibu wa Profesa Shivji, kilichofanyika ni mazungumzo yaliyojikita kwenye ukweli wa kitafiti, ili kupata suluhu ya kero zinazoikabili jamii.

Hata hivyo, akionekana mwenye kukerwa na baadhi ya hoja hasa zilizohusu udhaifu wa dhahiri katika mchakato wa ubinafsishaji wa viwanda na mashirika ya umma yanayofikia 330 kwa ujumla wake, Mkapa akajenga hoja nyingi, mojawapo ni kwa namna gani nchi imeshindwa kuanzisha viwanda vingine mbali na vilivyobinafsishwa?

Binafsi sikutegemea hoja kama hiyo itoke kwa Mkapa, kwa maana akiwa mfano wa mzazi wa taifa hili lililojaliwa rasilimali za ‘kutupwa’ wakati wa Urais wake, ndipo mali zilizomilikiwa na umma zikapewa kwa wageni, tena kwa ‘bei ya kutupwa’.

Hapo Mkapa anajenga hoja kwamba kati ya viwanda na mashirika ya umma 330 yaliyobinafsishwa, 180 yalipelekwa kwa wazawa, 23 wakapewa raia wa kigeni na mengine yakawa kwenye ubia.

Inawezekana kwa idadi, wazawa walikabidhiwa mashirika na viwanda vingi, lakini tujiulize, yalikuwa katika hali gani wakati wa kubinafsishwa?

Nimesema sikutegemea swali la kuanzishwa viwanda vipya litoke kwa Mkapa kwa sababu kadhaa, miongoni mwa hizo ni kwamba, akiwa ‘muasisi’ wa ubinafsishaji katika nafasi ya Rais wan chi, alikiandaa vipi kizazi cha Tanzania ili kimudu umiliki wa sekta za uzalishaji?

Ama baada ya kubinafsisha, alitegemea muujiza gani utakaowatoa Watanzania katika ‘umasikini wa kutupwa’ na kuwa na uwezo wa kubuni na kuanzisha viwanda? Mpaka!

Hapo ni dhahiri kwamba yapo matatizo yaliyojitokeza kabla na wakati wa ubinafsishaji. Hayo ni pamoja na hofu ya nini kitatokea ikiwa matakwa ya kubinafsisha yaliyotolewa na ‘mabwana wakubwa’ wa nchi za Magharibi yasingefikiwa!

Pili watu waliochaguliwa na wananchi ili wawaongoze, wanaonekana kushindwa kutekeleza wajibu wao, hivyo njia pekee ni kujiuza kuwa watawala badala ya viongozi. Hoja hiyo ilijengwa kwa ufasaha na Mwanazuoni nguli, Jenerali Ulimwengu.

Kwamba inakuwa rahisi kwa wachaguliwa kuwa watawala badala ya viongozi wanaoutumikia umma, kwa vile kiuhalisia hawafanyi kazi za umma, bali kuwafurahisha ‘mabwana’ wanje, wakihofia kutengwa kiusalama, kisiasa.

Ulimwengu akashauri kwa hoja iliyo na mantiki kuu, kwamba wakati ufike kwa viongozi kurejea kwa wananchi, kukaa na wananchi, kuzungumza na wananchi na kuwa sehemu iliyo dhahiri ya wananchi.

Taifa likifika hapo, haitakuwa jambo gumu hata viongozi (watawala?) wakiushirikisha umma kubuni mikakati ya muda mrefu na muda mfupi, hata ikibidi kutumia dhana ya ‘kufunga mikanda’ ili kufikia malengo yenye sura halisi ya maendeleo endelevu.

Ni kwa hali hiyo, ninaamini kwamba Mkapa hakustahili kuwa ‘mbogo’ kujibu hoja za kushindwa kwa mpango wa ubinafsishaji uliotekelezwa akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, badala yake, angeelezea na kukiri upungufu kama anavyoshiriki kuutetea mpango mzima!

Ubinafsishaji pekee hauwezi kuwa kipimo cha utawala wa miaka 10 ya Mkapa. Kama ulishindwa lakini yapo maeneo mengi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo aliyashiriki vizuri na hilo haliwezi kupingika.

Si nia yangu kuyaainisha hapa, lakini unapoutaja utawala wa Mkapa ni dhahiri kwamba unataja kiwango duni cha mfumuko wa bei za bidhaa, unataja uimarishaji wa miundombinu kama barabara, unataja uwezo wa mwananchi kumudu gharama za maisha ikilinganishwa kwa sasa.

Pamoja na kwamba hayo yapo kwa namna tofauti, bado yanaweza kuibua mijadala, lakini kwa hili la ubinafsishaji, Mkapa hakustahili na hastahili kuendelea kuwa ‘mbogo’ kwa kuutetea. Labda iwe ni kutokana na ujasiri usiojulikana unatokana na nini!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles